Kanisa lamsamehe aliyekamatwa akiondoka na ekaristi takatifu kanisani

Ifakara. Kanisa Katoliki Jimbo la Ifakara, limemsamehe Enock Masala (19), aliyetaka kutoroka na ekaristi takatifu kanisani.

Kijana huyo alikamatwa jana Jumapili Julai 28, 2024, wakati wa misa ya kwanza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Andrea, Jimbo Katoliki la Ifakara, baada ya kukomunika, aliificha ekaristi takatifu na kuondoka nayo bila kuitia mdomoni.

Hata hivyo, walinzi wa kanisa hilo walimkamata na alipohojiwa na kamati ya ulinzi ya kanisa hilo, alikiri kwamba yeye sio Mkatoliki, hajabatizwa wala hajapata mafundisho yoyote, hivyo hajui utaratibu wa ibada wala wa kanisa hilo kwa ujumla.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu jana usiku baada ya kijana huyo kusamehewa, Paroko wa kanisa hilo, Padri Marcus Mirwatu amesema baada ya kijana huyo kuhojiwa na kuomba msamaha, kanisa limemsamehe.

Hata hivyo, amesema kanisa linaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusiana na matukio ya aina hiyo.

“Hili ni tukio la nne kutokea kwenye kanisa letu. Mwaka jana, kuna vijana wawili walichukua ekaristi na kutaka kuondoka nazo. Hata hivyo, tuliwakamata na kuwahoji, kisha kuwasamehe baada ya kudai hawakuwa wanafahamu taratibu za uchukuaji wa ekaristi hiyo,” amesema Padri Mirwatu.

Amesema tukio lingine lilitokea Jumapili ya wiki iliyopita, Julai 21, 2024 wakati waumini wanakwenda kukomunika (kupokea mwili wa Kristu), kijana mmoja aliingia kanisani akaenda moja kwa moja kupanga foleni ya kwenda kushiriki na alipomfikia padri akampatia ekaristi, lakini hakuitia mdomoni na badala yake aliiweka mfukoni na kuondoka nayo.

Padri Mirwatu amesema baada ya kuondoka alirejea tena kwenye foleni na kuchukua nyingine, hali iliyowatia wasiwasi waumini na watumishi wa kanisa, hivyo walimkamata na kumuhoji sababu ya kuchukua ekaristi zaidi ya mara moja.

“Tukio la leo (jana) pamoja na kwamba tumemsamehe yule kijana, bado tunaendelea na uchunguzi kujua hizi ekaristi zinachukuliwa na kupelekwa nje ya kanisa kwa lengo gani? Likitokea tukio lingine kama hili, sasa tutahakikisha wahusika tunawafikisha polisi maana hatujui zinatumikaje huko nje ya kanisa,” amesema Padri Mirwatu.

Aidha, amesema baada ya matukio hayo, kamati ya ulinzi ya kanisa imeanza mikakati ya kuimarisha ulinzi wakati wa ibada na nyakati nyingine, ili kubaini vitendo hivyo na vingine viovu vinavyofanyika kanisani hapo.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu baada ya kusamehewa na kuachiwa, kijana Masala amesema yeye ni mgeni na amefika Ifakara kutafuta maisha, kwani alikuwa akiishi jijini Mwanza.

Hata hivyo, amesema pamoja na kwamba yeye si Mkatoliki, baada ya tukio hilo amependa kuwa Mkatoliki na yuko tayari kubatizwa na kupata mafundisho yote, ili awe muumini wa kanisa hilo.

“Mi nilijua ile (ekaristi) anapewa kila mtu anayekuja kusali kanisani, ndiyo maana nikaenda kuchukua, sikujua kwamba ni makosa, nimewaomba msamaha, wamenisamehe,” amesema Masala.

Related Posts