Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, jijini Dar es Salaam imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi ya ukahaba inayowakabili washtakiwa 17 kutokana na washtakiwa watatu kutokuwepo mahakamani, wawili kati yao bila ya kuwapo taarifa.
Kutokana na hali hiyo, Mahakama imeamuru mshtakiwa, Zainabu Hamis akamatwe kwa kushindwa kufika mahakamani kwa zaidi ya mara moja kwa nyakati tofauti bila kutoa taarifa.
Hii ni mara ya pili kwa mshatakiwa huyo kuamuriwa kukamatwa kwa sababu hiyo, lakini mbele ya mahakimu wawili tofauti.
Hata hivyo, wakati Mahakama ikitoa amri ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo, imetoa msamaha kwa mshtakiwa, Jenifer John kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kushindwa kufika mahakamani, huku ikitoa onyo kwa washtakiwa wote kwa mwenendo huo wa utoro.
Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka leo Jumatatu, Julai 29, 2024, baada ya kukamilika usikilizwaji wa awali uliofanyika Julai 10, 2024, ambapo washtakiwa walisomewa maelezo ya awali ya kesi.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka wa kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Mwasiti Ally ameieleza Mahakama kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya usikilizwaji na kwamba upande wa mashtaka walikuwa tayari na mashahidi wawili.
Hata hivyo, amesema wana taarifa washtakiwa wengine hawapo mahakamani na hawana taarifa za kuridhia kwa mawakili wao kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo bila wao kuwepo.
Hivyo, amesema kifungu cha 197 (b) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) kinazuia kuendelea na kesi bila mshtakiwa kuwepo, hivyo kuomba amri ya kukamatwa kwa washtakiwa hao pamoja na wadhamini wao.
Akijibu hoja hiyo, wakili wa utetezi, Maria Mushi amesema hawana mawasiliano na washtakiwa hao ambao hawakuwepo, isipokuwa Elizabeth Michael aliyetuma mdhamini wake kutoa taarifa kuwa ana msiba.
Kuhusu hoja ya amri ya kukamatwa kwa washtakiwa wengine, wakili Maria ameiomba Mahakama iwasamehe na kutoa onyo akidai hawajawahi kukosa kufika mahakamani, bali ni mara ya kwanza.
Hata hivyo, wakili Mwasiti amesema hata mara ya mwisho, wakati washtakiwa hao waliposomewa maelezo ya awali ya kesi, Julai 10, 2024, hakuwepo.
Akitoa uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Mkazi, Francis Mhina anayesikiliza kesi hiyo ametoa msamaha kwa mshtakiwa Jenifer, lakini akaamuru mshtakiwa Zainabu akamatwe.
“Mshtakiwa wa 16 (Jenifer) anapewa nafasi ya kujirudi, lakini akija atueleze alikuwa wapi na huyu wa 17 (Zainabu) Mahakama inaamuru akamatwe,” ameamuru Hakimu Mhina.
Pia Hakimu Mhina amewaonya washtakiwa hao kuhusu mwenendo wa tabia ya utoro unaokwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo na kwamba kama wana changamoto watoe taarifa.
“Vinginevyo nitawakamata na nikiwakamata nikawapeleka kule (mahabusu) sitawatoa mpaka miezi sita,” ameonya Hakimu Mhina.
Pia Mahakama imewataka mashahidi wawili wa upande wa mashtaka waliokuwa wameitwa wafike mahakamani tarehe ijayo, huku akiutaka upande wa mashtaka kuongeza idadi ya mashahidi kufikia watatu kwa siku ama wanne. Upande wa mashtaka unatarajia kuwa na mashahidi 10.
Hakimu Mhina ameahirisha kesi hadi Agosti 5, 2029 itakapoendelea kusikilizwa kwa siku mbili mfululizo.
Hii ni mara ya pili kwa Mahakama kuamuru washtakiwa katika kesi hiyo wakamatwe kutokana na kutokufika mahakamani bila taarifa.
Mara ya kwanza ilikuwa Julai 4, 2024, ambapo Hakimu Mfawidhi, Lugano Kasebehe aliamuru washtakiwa watano wakamatwe kutokana na kutokufika mahakamani bila taarifa. Washtakiwa hao ni Aisha Iddi, Sabrina Gabriel, Recho Kindole, Diana David na Zainabu Hamis.
Mbali na washtakiwa hao, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Amina Ramadhani, Mariana Sia, Mwajuma Hamza, Mariamu Hassan, Najma Hamisi, Mariam Kitamoga, Rosemary John, Jackline Daniel, Mwajuma Bakari na Recho Bakari.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya, kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.
Wanadaiwa Juni 14, 2024 maeneo ya Sinza Mori, jijini Dar es Salaam, walikutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.
Walidaiwa kukamatwa na askari polisi na kupelekwa Kituo cha Polisi Mburahati kwa ajili ya mahojiano na baada ya mahojiano Juni 24, 2024 walifikishwa mahakamani na kusomewa shtaka lao.
Hata hivyo, washtakiwa hao baada ya kusomewa maelezo hayo walikubali taarifa zao binafsi (utambulisho wao), lakini wakakana maelezo mengine kuhusiana na shtaka linalowakabili.
Mbali na kesi hiyo, pia kuna kesi nyingine inayowakabili washtakiwa watano.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya, kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.
Washtakiwa ni Mariam Yusufu Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.
Wanadaiwa Juni 17, 2024 eneo la Manzese Tiptop, jijini Dar es Salaam, walikutwa wakifanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa kusimama hadharani, wakiwa wamevaa mavazi yasiyo ya heshima kwa lengo la kufanya umalaya.
Jumla ya mashahidi wanne wa upande wa mashtaka kati ya 10 wanaotarajiwa kutoa ushahidi wameshatoa ushahidi wao.