Maboresho mifumo ya kodi yanukia

Dar es Salaam. Machungu yanayowakabili wafanyabiashara huenda yakapata mwarobaini, baada ya Serikali kutangaza mpango wa kuunda kamati ya maboresho ya mifumo ya kikodi.

Kamati hiyo itakayoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhusisha wajumbe kutoka sekta ya umma na binafsi, inatarajiwa kuja na mapendekezo yatakayofumua mifumo ya kikodi itakayohusisha sera na sheria.

Msingi wa kuundwa kwa kamati hiyo, ni kile kilichoelezwa na wafanyabiashara juu ya mifumo iliyopo, wakilalamikia kufungiwa akaunti za benki, kuchukuliwa fedha bila utaratibu sahihi na kufungiwa kwa mashine za EFD.

Malalamiko hayo yalisababisha migomo kwa wafanyabiashara nchini kuanzia Julai 24 mwaka huu maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam kisha kusambaa mikoa ya Mbeya, Arusha, Kigoma, Mtwara, Dodoma, Morogoro, Kagera, Ruvuma na Iringa.

Hatua hiyo ilisababisha Serikali kutangaza kusitisha kwa muda matumizi ya risiti za EFD wakati ikitafuta suluhu ya kumaliza mgomo huo. Baadaye ufumbuzi ulipatikana kwa Serikali kuahidi kuzitafutia ufumbuzi kero za utitiri wa kodi za TRA.

Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni Rais Samia kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri Julai 1, 2024, kwa kuwabadilisha wizara mawaziri.

Dk Seleman Jafo alitoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kwenda Viwanda na Biashara, kuchukua nafasi ya Dk Ashatu Kijaji aliyepelekwa kumrithi Dk Jafo.

Pia, Rais Samia alimteua Yusuf Mwenda kuwa Kamishna Mkuu wa TRA akichukua nafasi ya Alphayo Kidata aliyeteuliwa kuwa msaidizi wa Rais Ikulu. Mwenda alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

Mifumo ya kikodi pia imewahi kulalamikiwa na wawekezaji kutoka nchi 10 waliowekeza nchini, ambao Juni 26, 2024 waliomba kikao na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Miongoni mwa malalamiko waliyoyaibua  katika barua ya ombi la kikao hicho, ni makadirio ya kodi yanayozidi uhalisia kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ( TRA),  hali inayosababisha baadhi yao kupata changamoto katika uendeshaji wa biashara.

Wawekezaji hao ni kutoka mataifa ya Marekani, Uingereza, Uholanzi, Ufaransa, Ubelgiji, Canada, Korea, Sweden, Ujerumani, Ireland. Aliyekuwa Waziri, January Makamba alikubali kikao hicho.

Katika hali ya kujibu changamoto hizo, Rais Samia ametangaza kuunda kamati ya maboresho ya masuala ya kikodi itakayohusisha wadau mbalimbali.

Rais Samia ametangaza kuunda kamati hiyo leo Jumatatu Julai 29 jijini Dar es Salaam jana  katika mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), uliofanyika Ikulu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi.

Baadhi yao ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mawaziri na makatibu wakuu.

Katika maelezo yake, Rais Samia amesema: “Serikali imedhamiria kuondosha changamoto tutaunda kamati, itakayoshirikisha wajumbe kutoka serikalini na sekta binafsi, mpitie kwa undani halafu mtuletee mapendekezo na ushauri mtakaouona unafaa kwa nchi yetu kwenda na mfumo huo wa kodi.”

Kamati hiyo kwa mujibu wa mkuu huyo wa nchi, haitaishia kuangalia mifumo ya kikodi pekee, bali itagusa hata sheria na sera za kikodi.

Upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza uwezo wa kuuza bidhaa za Tanzania nje ya nchi, ni majukumu mengine yanayotarajiwa kutekelezwa na kamati hiyo itakayoundwa.

“Wengi wamefurahia kwamba Serikali imetambua hata yale mazao yaliyokuwa yanaitwa ya chakula sasa yote yanaitwa ya biashara,” amesema.

Taarifa ya kuundwa kwa kamati hiyo ilichochewa na malalamiko ya wafanyabiashara yaliyowasilishwa na mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Ali Suleiman Amour katika mkutano huo.

Katika taarifa yake hiyo, amesema kuna upungufu katika usimamizi wa sheria ya usimamizi wa kodi inayosababisha changamoto kwa wafanyabiashara.

Baada ya TPSF kukaa na wafanyabiashara, amesema walibaini walikuwepo ambao hawakuwa na madeni kabisa ya kodi.

Kwa mujibu wa Amour, makosa yalibainika kwa TRA hasa katika utunzaji wa kumbukumbu.

“Upungufu katika uthaminishaji wa mizigo bandarini na kamata kamata zilizokuwa zinaendelea Kariakoo ulishinikiza utoaji wa risiti Kariakoo. Tunatarajia utaratibu mpya utasimamiwa vema,” alisema.

Sambamba na hayo, amesema taasisi hiyo imebaini kuongezeka kwa biashara za magendo na bandia ambazo kimsingi zinaathiri ushindani nchini.

Ameeleza kufurahishwa na uanzishwaji wa ofisi ya msuluhishi wa malalamiko ya kikodi tangu mwaka 2019 na mwaka 2022 ilianza kufanya kazi.

Lakini, amependekeza itoke chini ya TRA kwa kuwa itashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kwa kuwa inasimamiwa na yule yule anayetoza kodi.

Hoja nyingine aliyoiibua ni sekta binafsi kwa sasa kuratibiwa na wizara zaidi ya moja, akitaka kuwepo moja itakayotambulika kwa ajili yao.

Amour pia, amependekeza umuhimu wa kuongeza wigo wa walipakodi akitaka angalau wafikie milioni 6.1, badala ya milioni mbili wa sasa.

“Katika hao milioni mbili ni robo yake ndiyo waadilifu na wanaolipa hiyo kodi,” alieleza.

Upatikanaji wa dola ni changamoto nyingine iliyoibuliwa na Amour, akisema unaathiri biashara, ununuzi wa malighafi za viwandani na hata upatikanaji wa mafuta.

Ametaka matumizi ya dola hasa kwa Serikali yapungue kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini na sio kila mwaka kununua magari mapya kwa watumishi.

Pamoja na mapendekezo hayo, ametaka wafanyabiashara wasigeuzwe maadui, kutengenezewa alichokiita mizengwe na figisu pale wanapotoa ripoti ya masuala ya rushwa na upotevu wa mapato.

Amelieleza hilo akirejea tukio alilodai lilitokea mkoani Arusha kwa mfanyabiashara mmoja mwanachama wa  TPSF, akifafanua kuwa hata hivyo,  Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda alilishughulikia hilo kwa ukamilifu.

Akisoma maazimio ya mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk Godwill Wanga amesema pamoja na azimio la kuundwa kwa kamati hiyo, pia wamekubaliana kuondoa urasimu.

Ameeleza kila wizara na idara ya Serikali imeazimiwa kutekeleza falsafa ya R4 kwa viongozi wa umma kuhakikisha wanakuwa wawezeshaji wa biashara na sio vikwazo.

R4 hizo ni Reconcilation (Maridhiano), Resilience (Ustahamiliivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga Upya).

Azimio lingine, amesema ni kukamilisha sera ya Wafanyabiashara wa Chini na Wadogo (SME) na kujengeana uwezo na kuanza kutekeleza nishati jadidifu.

Kwa mujibu wa Dk Wanga, iliazimiwa pia kila risiti inayotolewa na TRA iambatane na bahati nasibu, akieleza jambo hilo linahitaji kuangaliwa zaidi.

Kuboreshwa kwa mpango wa kurahisisha mazingira ya biashara wa kila mwaka ni azimio lingine lililosomwa na Dk Wanga katika mkutano huo.

Pia, mkutano huo uliazimia kuboresha mfumo wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Kutokana na maazimio hayo, Rais Samia ameeleza kila waziri na katibu mkuu kuhakikisha anachukua linalomuhusu na kupanga muda wa kukaa na sekta binafsi kwa ajili ya kutafutia ufumbuzi.

Amesisitiza maazimio hayo yafanyiwe kazi haraka ili kitakapofika kikao cha mwakani itolewe taarifa ya utekelezaji wake.

“Kamati zitakazoundwa wakimaliza mambo yao hatua zichukuliwe ili tutakapokutana mwakani tuseme Serikali imefanya hivi na sekta binafsi imefanya hivi,” amesema.

Hata hivyo, amesema ni azma ya Serikali kujenga uhusiano mzuri na wenye manufaa na sekta binafsi ili kuongeza mapato kupitia biashara.

Sambamba na hayo, mkuu huyo wa nchi amesema anafahamu uwepo wa changamoto katika maeneo mbalimbali na kwamba ataendelea kuyafanyia kazi.

Kwa mujibu wa Rais Samia, anafahamu uwepo wa baadhi ya watendaji serikalini wasiofahamu dhamira ya kuwezesha biashara na uwekezaji.

“Nafahamu changamoto ya uratibu kati ya sekta moja na nyingine, gharama za stempu za kodi, ucheleweshaji wa vibali mbalimbali na wakati mwingine kutoshirikishwa (kwa wafanyabiashara) kwenye baadhi ya mabadiliko,” amesema.

Anaamini ufumbuzi wa changamoto mbalimbali utapatikana na kwamba dhamira itaeleweka.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia alieleza Serikali imekuja na mageuzi ya kuondoa ukiritimba katika uendeshaji wa shughuli za reli, ili kuwapa fursa zaidi waendeshaji binafsi.

“Niwataarifu tukiongozwa na falsafa ya R4, Serikali imekuja na mageuzi ya kuondoa ukiritimba katika uendeshaji wa shughuli za reli.

“Tumerekebisha sheria ya reli, ili kuruhusu waendeshaji binafsi kutumia miundombinu hiyo kutoa huduma za usafishaji,” amesema.

Amesema kanuni zipo tayari na aliitaka sekta binafsi ichangamkie fursa hiyo.

Pamoja na hilo, alitangaza Agosti 1, mwaka huu atakwenda kuzindua safari za treni ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi,  amesema Serikali ina matarajio makubwa juu ya mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kupitia mkutano huo, alisema imedhihirika wafanyabiashara wapo tayari kulipa kodi na tozo mbalimbali kwa mujibu wa sheria kwa kufahamu hakuna nchi inayoweza kuendelea bila kupata kodi.

“Matumaini yangu maazimio ya mkutano huu yatakuwa dira ya kutatua changamoto zinazokabili shughuli za biashara nchini na kuwa muongozo kwa Serikali, watendaji na wafanyabiashara katika kuhakikisha tunafungua ukurasa mpya wa kuwa na mageuzi ya kidigiti ili kuongeza fursa za ukuaji wa uchumi,” amesema.

Sambamba na hayo, amesisitiza umuhimu wa kila mmoja kutekeleza maazimio ya mkutano huo,  ili katika mkutano ujao wazungumzie mafanikio na utekelezaji.

Related Posts