Pwani. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali Jacob Mkunda amesema ushirikiano wa kijeshi kati ya Tanzania na China unaongeza umahiri wa majeshi hayo, kukuza diplomasia na ushirikiano kati ya mataifa hayo.
Amesema miaka 60 iliyopita, Tanzania na China zimekuwa pamoja katika nyanja mbalimbali, ikiwemo za kiuchumi, afya, miundombinu, uwekezaji, kilimo, ujenzi pamoja na kijeshi.
“Kwa wale wasiofahamu, uhusiano wa JWTZ na PLA hauelezeki na vifaa vingi vya jeshi letu vimetengenezwa China. Ujenzi wa ngome ya kamandi ya maji Kigamboni, ngome ya anga Ngerengere, CTC Mapinga na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) kuna mkono wa China,” amesema.
Jenerali Mkunda ameeleza hayo leo Jumatatu Julai 29, 2024 katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi CTC Mapinga kilichopo wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wakati akizindua mazoezi ya medani kati ya JWTZ na PLA.
Mazoezi hayo yanayohusisha kamandi za nchi kavu, angani na wanamaji. “Tunashukuru wote waliofanikisha mazoezi haya yaliyopewa jina la Amani Umoja 2024, ambapo tunaongeza ujuzi na maarifa kati ya majeshi yetu haya, hakika mmeacha alama isiyosahaulika,” amesema.
Mkunda ameongeza kuwa, “Mazoezi ya mwaka huu ni zaidi ya yale yaliyopita tangu majeshi hayo yaanze kuwa pamoja yakiwa na lengo la kuwezesha amani na usalama wa dunia kama ilivyo malengo ya kimataifa.”
Amesema mazoezi hayo yatachukua siku 14 kukamilika, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya nchi hizo na miaka 60 ya JWTZ yatakayofanyika Septemba mosi, 2024.
Katika hilo, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo, Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema mazoezi yatafanyika maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Mtwara, Lindi pamoja na Pemba na Unguja.
“Kwa upande wa pili, mazoezi haya yatafanyika eneo la nchi kavu, ikiwemo Mapinga kama ilivyokuwa katika mazoezi yaliyopita,” amesema.
Aidha, Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China PLA, Meja Jenerali Ye Dabin amesema mbali na kujifunza umahiri kati ya askari wa nchi hizo, uhusiano wa kidiplomasia unaongezeka.
Awali, wanajeshi wa JWTZ pamoja na wenzao wa PLA wakiwa katika makundi tofauti walikuwa na nyuso za bashasha wakiimba na kucheza tayari kwa ufunguzi wa zoezi hilo.
Alipofika CDF Mkunda alihutubia mamia ya wanajeshi pamoja na viongozi wengine wa kijeshi, kabla ya kukabidhi bendera kwa mkuu wa zoezi kuonyesha ishara ya kuanza kwa zoezi hilo la medani.
Kisha, Mkunda akiambatana na wanajeshi wengine walikwenda kutazama silaha, teknolojia za kisasa pamoja na magari ya kivita yaliyoandaliwa Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China.
Hii ni mara ya nne kwa Jeshi la Wananchi la Tanzania na Jeshi la Ukombozi wa watu wa China kufanya mazoezi ya pamoja na kubadilishana uzoefu, ikiwa ni moja ya njia ya kuboresha ushirikiano.
Kwa mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2014, kisha 2019, 2020, 2023 na mwaka huu 2024.