Mambo ya kukumbuka kwa Kinana

Dar es Salaam. Abdulrahman Kinana, ameamua kupumzika siasa za majukwaani. Ni baada ya kukitumikia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi mbili za juu.

Alianza akiwa Katibu Mkuu akaomba kupumzika. Aprili mosi, 2022 wajumbe wa mkutano mkuu wakamchagua kwa kishindo kuwa Makamu Mwenyekiti-Bara wa chama hicho.

Kinana (71), amemwandikia barua Mwenyekiti wake wa chama, Rais Samia Suluhu Hassan ya kuomba kujizulu nafasi hiyo.

Taarifa ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla imeeleza Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia ameridhia ombi la Kinana aliyeomba kupumzika.

Makalla amemnukuu Rais Samia akisema: “Ni kweli nilipokuomba utusaidie kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti nilikuahidi utakaa muda mfupi kama ulivyoomba na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia, lakini kwa kuwa umeomba sana na ahadi ni deni nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujizulu kwako.”

Pia, Makalla amesema Mwenyekiti wa CCM amesisitiza chama kitaendelea kutumia uzoefu na maarifa ya Kinana kila itakapohitajika na chama kinamshukuru kwa mchango wake mkubwa.

Kinana ameondoka katika nafasi hiyo akiwa ameacha kivuli kitakachomfanya akumbukwe katika mambo mengi, lakini hapa tunaangazia machache ya kukumbukwa.

Ingawa tangu mwaka 2016 alionekana kuwa kimya, utendaji wake wa awali tangu alipoteuliwa mwaka 2012, umeendelea kumbeba na kumfanya kuwa mwanasiasa wa kipekee.

Kutokana na utendaji huo, Kinana anaelezwa na makada kuwa si rahisi kuvaa viatu vyake, huku mjadala mkubwa juu yake ukiwa umejikita katika kuipa CCM uhai, kutoa nafasi kwa vijana, kuweka mfumo bora wa utumishi, kurudisha chama kwa wanachama, kuisimamia Serikali, kuinusuru CCM 2015 na kuwa kinara wa kampeni.

Akiwa ameshika nafasi nyeti ya ukatibu mkuu mwaka 2012, kipindi ambacho CCM ilikuwa na wakati mgumu kujibu mapigo ya wapinzani, Kinana anakumbukwa kwa kazi kubwa aliyofanya na kufanikiwa kurejesha uhai wa chama.

Ilikuwa baada ya Uchaguzi Mkuu 2010, vyama vya upinzani, hususan Chadema, ndiyo walikuwa wamebeba ajenda za kisiasa, huku baadhi ya wanaCCM wakiona aibu hata kuvaa sare za chama hicho.

Kilikuwa ni kipindi ambacho aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete aliwataka wanachama wake kujibu mapigo ya upinzani bila kutegemea Jeshi la Polisi.

“Mnaishia kulalamika tu kila siku, eti wanatukana halafu mnaishia kusema ndiyo kawaida yao … au utasikia mtu anasema eti Serikali haipo! Kazi ya Serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa maana hao ndio wenzenu.

“Sasa mnataka wakisema Serikali ya CCM haijafanya kitu polisi wawafuate, au wakisema Kikwete nchi imemshinda, polisi wakawakamate? Kama wakisema hatujafanya kitu ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu, waonyesheni barabara, shule na mambo mengine.

“Nataka mfahamu ndugu zangu kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu, tutakwisha na tutakwisha kweli,” alisema Kikwete.

Katika mazingira hayo, Kinana aliingia ofisini na mitaani akipigana kubadili taswira hiyo. Akiongozana na Katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi wa wakati huo, Nape Nnauye, Kinana alizunguka nchi nzima kujenga chama ambacho kilikuwa kimeporomoka na kurejesha heshima yake. Nape alielezea hali hiyo kuwa sawa na kukitoa chama shimoni.

Hayati John Magufuli (kulia) enzi za uhai wake akisalimiana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana (kushoto) ambaye amejiuzulu wadhifa huo leo Julai 29, 2024. Picha na Mtandao

Kwa staili yake ya kuiwajibisha Serikali, Kinana alionekana kama anafanya kazi ya upinzani na kukosoa utendaji wa mawaziri na watumishi wengine wa umma.

Aliwaita baadhi ya mawaziri mizigo na kuwataka kwenda kwa wananchi kufafanua utekelezaji wa ilani ya chama. Pia alionyesha kukerwa na tabia ya wabunge wa CCM kusifia na kuunga mkono kila kitu kinachopelekwa na Serikali bungeni.

“Jambo jema likiletwa lipitisheni, jambo la hovyo likiletwa, kataeni. Siyo kila kinacholetwa na Serikali ya CCM mnakiunga mkono, hata kama cha hovyo,” alisema.

Nje ya ulingo wa siasa, ndani ya chama Kinana anatajwa na watumishi wa chama kwa kuweka mfumo bora wa utumishi, kuongeza thamani kwa watumishi na kuwapa muda wa mapumziko kwa kuwa awali hakukuwa na likizo.

Kwa mujibu wa watumishi hao, Kinana ndiye alisema kila mtumishi anastahili kupumzika, ili kuja na nguvu mpya.

Kama haitoshi, Kinana anatajwa kupenda kusikiliza watu wa ngazi zote akitumia falsafa kwamba ‘katika kila ujinga mwingi kuna werevu kidogo’.

Pia alikuwa hatoi fursa kwa wapika majungu na ingetokea mtu akampelekea majungu ama alimrudisha au alimuita mhusika kusikiliza.

Wakati wa ziara, kwa kutopenda kujikweza alikula, kulala na kufanya kazi na watu wa aina tofauti bila kujali tofauti zao.

Kwa kauli za watendaji na makada wengi wa CCM, mwaka 2015 ilikuwa chupuchupu kung’olewa madarakani, lakini kazi kubwa ya wanaCCM chini ya Kinana ilifanikisha kuendelea kushikilia madaraka ya nchi. Pamoja na hatua hiyo, baadhi ya viongozi wa chama ambao hawakutimiza wajibu wao walinyooshewa vidole, waliokisaliti walikemewa na wengine kung’olewa, ili kuhakikisha chama hicho kinabaki kwenye mstari.

Ukisoma maandiko au kusikiliza ushuhuda wa watumishi waliokuwa chini yake, ni dhahiri Kinana aliwapa fursa vijana kuonekana. Vijana kama Nape, January Makamba na vijana wengine wanashuhudia suala hili.

Nape alisema Kinana alikuwa mwalimu aliyebadili mtazamo wake juu ya siasa na utumishi kwa umma na hivyo ‘amepanda mbegu na itaota.’

Si jambo la kawaida kumpata kiongozi aliyeongoza kampeni za urais kwa marais watatu, mara moja akiwa Katibu Mkuu na mara mbili akiwa Meneja wa Kampeni.

Ni Kinana pekee aliyehakikisha Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa anashinda mara mbili, Kikwete wa awamu ya nne anashinda mara mbili na awamu ya kwanza ya Rais John Magufuli.

Related Posts