Manabii Tanzania wamkana Kiboko ya Wachawi

Dar es Salaam. Baraza la Mitume na Manabii Tanzania (Bacct) limesema halimtambui Mchungaji, Dominique Dibwe maarufu Nabii Kiboko ya Wachawi na kueleza kuwa si mwanachama wao.

Pia limesema walipojaribu kumtafuta kwa simu baada ya taarifa za kanisa lake la Christian Life kufungwa na Serikali, waliambiwa na watu wake wa karibu kuwa amekwishaondoka nchini.

Kiboko ya wachawi ambaye ni Raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, alikuwa akiendesha huduma zake Buza Kwalulenga Mtaa wa Kidagaa, kabla ya taarifa ya kufungiwa kwa kanisa lake kutolewa Julai 25, mwaka huu.

Barua ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia, ilimuelekeza Mwenyekiti wa Kanisa hilo na Mchungaji Dominique Kashoix Dibwe kufunga tawi la kanisa hilo.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kudaiwa kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha matakwa ya kifungu cha 17 cha Sheria ya Jumuiya, Sura ya 337 kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Namba 3 ya Mmwaka 2019.

Vitendo hivyo vimesababisha kanisa hilo kufutiwa usajili wake na kuondolewa kwenye rejista ya jumuiya za kiraia zilizosajiliwa.

Miongoni mwa sababu za kufungwa kwake zimetajwa ni kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume cha maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.

Madai mengine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, kutoa mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa lake kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina. 

Barua hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha imetolewa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa imesema, madai hayo yanakwenda kinyume na imani ya Kikristo, Katiba na kanuni za kanisa hilo, ikiwamo kuweka kiwango cha Sh500,000 kwa waumini  kupata huduma ya maombezi.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatatu Julai 29, 2024, Rais wa BacctNabii Joshua Mwantyala amesema wanamfahamu kama nabii aliyekuwa akifanya kazi jijini hapa lakini si mwanachama wao.

“Na sisi tumeona tu barua kuwa amefungiwa kanisa lake na tumefuatilia tumeambiwa kuwa amesharudi nchini kwao,” amesema nabii huyo.

Amesema ili mtu awe mwanachama anatakiwa kujaza fomu yenye vigezo kikiwamo kigezo cha uadilifu na kuhubiri Injili inayoendana na Neno la Mungu.

Amesema muombaji akikamilisha ujazaji wa fomu hiyo, hupatiwa kadi anayotakiwa kuanza kuilipia ada Sh50,000 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa nabii huyo, wana wanachama wa aina mbili, wa kwanza wa madhahebu 227 wa pili ni wale ambao ni manabii, wachungaji na mitume, ambaao  idadi yao ni zaidi ya 12,000.

“Kuwa nabii ni suala la Mungu, kwa sababu  yeye ndiye anayemuita mtu na yeye ndiye anayejitambua kuwa anatakiwa kutoa huduma fulani kama ni ya kinabii au kitume. Yeye hatujawahi kumshawishi ajiunge wala hajawahi kukataa kujiunga kwa sababu kujiunga kwetu ni hiari ya mtu,” amesema.

Wakati hayo yakisemwa, kanisani kwa Kiboko ya Wachawi, Mwananchi lilifika leo na kuwakuta waumini wakiendelea na maombi ya kilio na kuomboleza wakitaka uamuzi wa Serikali utenguliwe.

Mmoja wa wauminu kanisani hapo akiwapa taarifa wenzake alisema tayari mchungaji wao ameshaanza kupita katika baadhi ya ofisi ili kurejesha huduma hizo na ngazi iliyobakia ni wizarani pekee.

Licha ya kuwa huduma zimesitishwa, bado waumini kutoka ndani na nje ya Dar es Salaam wameendelea kufika kanisani hapo huku baadhi wakisema hawana taarifa za kufungwa kwa kanisa hilo.

Mwandishi alipojaribu kumuuliza mmoja wa watumishi kanisani hapo kuhusu huduma nyingine kama maji na mafuta zinaendelea kutolewa.

“Hizo zipo lakini tatizo huduma zimesitishwa na Serikali na unapotoa vifaa hivi hujui unamuuzia nani inaweza kuwa shida,”amesema.

Related Posts