Baada ya kikao chao cha siku ya Jumatatu (Julai 29) mjini Tokyo, mwenyeji wa mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Japan, Yoko Kamikawa, alisema wana wasiwasi sana na hali ya mtafaruku inayoshuhudiwa sasa na wanapingana vikali na mabadiliko yanayofanywa na upande mmoja kwa kutumia nguvu.
Akiwa na wenzake wa Marekani, Australia, na India, na bila kuitaja kwa jina China, mawaziri hao walitaja kwenye tamko lao la pamoja kile walichokiita “utumiaji wa nguvu za kijeshi kwenye maeneo yanayozozaniwa, na luteka zinazoogofya na kutisha kwenye Bahari ya Kusini ya China.”
Mataifa kadhaa ya eneo hiloo yanazozana na China inayodai umiliki wa eneo lote la Bahari ya Kusini ya China, eneo ambalo lina njia muhimu za kibiashara na uwezekano wa akiba kubwa ya mafuta na gesi.
Beijing pia inakichukulia kisiwa cha Taiwan kuwa miliki yake, na imekuwa ikisema kuwa itakivamia na kukitwaa kwa nguvu ikibidi.
Ushirikiano wa masuala ya usalama
Kwenye mkutano huo wa pande nne, mawaziri hao wa mambo ya kigeni wamekubaliana kushirikiana kwenye hatua kadhaa kukabiliana na mashambulizi ya mitandaoni, kuhakikisha usalama wa baharini na kushughulikia suala la habari za uzushi.
Vile vile walitangaza kutanuwa operesheni zao kuyasaidia mataifa mengine ya eneo hilo, vikiwemo visiwa na mashariki kusini mwa Asia na Pasifiki, ili viweze vyenyewe kujilinda.
Mawaziri hao wamepanga kuzinduwa jukwaa la majadiliano juu ya mizozo ya baharini litakalojikita kwenye sheria za kimataifa za baharini.
Walisema wamedhamiria kuchangia kwenye kuimarisha na kuendeleza mfumo huru na wa wazi wa baharini unaokwendana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa juu ya Sheria za Bahari kwenye Bahari za Hindi na Pasifiki, sambamba na kuimarisha ushirikiano na uratibu kwenye bahari hizo.
Bahari ya Hindi yajumuishwa
Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Kamikawa, mataifa hayo manne yameamuwa kuutanuwa ushirikiano wao na kuijumuisha Bahari ya Hindi ili kuimarisha uwelewa juu ya udhibiti wa njia hizo muhimu kwa biashara na usalama wa dunia.
Miradi waliyoipanga ni pamoja na ule wa kuweka mtandao wa mawasiliano ya simu kweye kisiwa cha Palau na kuwajengea uwezo maafisa wa usalama wa India na Ufilipino ili waweze kukabiliana na uhalifu unaofanyika kupitia mitandao.
Waziri wa Mambo wa Nje wa Marekani, Antony Blinken, alisema na hapa namnukuu: “Tumedhamiria kuwekeza nguvu na rasilimali zetu kwenye kufanya kazi ya kuwafaidisha watu wa pande hizi.”
Kuhusiana na makombora yanayorushwa na Korea Kaskazini na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, Kamikawa alisema hali inazidi kuwa mbaya.
Vyanzo: AFP, AP