Moto wateketeza bweni sekondari ya Mugeza, chanzo hakijafahamika

Kagera. Moto ambao chanzo chake hakijafahamika umeibuka na kuteketeza bweni la sekondari ya Mugeza iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Moto huo unadaiwa kuibuka leo Jumatatu Julai 29, 2024, saa 5:45 asubuhi na kuteketeza mali vikiwemo vitanda, magodoro na madaftari ya wanafunzi zaidi ya 120 waliokuwa wakilala ndani bweni hilo.

Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Mzamilu Hassan amethibitisha bweni hilo kuteketea kwa moto, huku akidokeza kuwa hadi sasa bado chanzo hakijafahamika.

Hassan amesema hakuna madhara kwa binadamu yaliyosababishwa na moto huo, zaidi ya mali za wanafunzi kuteketea  na kusema uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika kubaini chanzo cha moto huo.

“Ni kweli bweni hilo limeteketea na wanafunzi wote zaidi ya 100 wako salama kwa sababu wakati linateketea walikuwa darasani. Hakuna aliyedhurika,” amesema Hassan.

Akisimulia tukio hilo, mwanafunzi wa shule hiyo aliyekuwa analala katika bweni hilo, Happiness Zawadi amesema mali zake zote zimeteketea.

Mwanafunzi huyo katika shule ya mchanganyiko ya Mugeza ameiomba Serikali na mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha moto huo kwa kile alichodai matukio ya moto shuleni yamekuwa yakijirudia.

“Siku chache tu zilizopita tulisikia kuna moto uliibuka ndani ya nyumba na kusababisha vifo vya watoto wawili huko Kemondo, leo tena tunaona umeibuka hapa kwetu tunaomba mamlaka kufanya uchunguzi wa kina wa matukio haya,” amesema Happiness.

Kwa upande wake, mkazi wa Kata ya Kahororo ilipo shule hiyo, Happiness Joas ameeleza kushtushwa na tukio hilo kwa kile alichodai endapo moto huo ungeibuka usiku huenda watoto wake wawili wanaosoma shuleni hapo wangedhurika.

“Kutokana na tukio hili la leo watoto wangu wanaonekana kujawa hofu kwa sababu hili ni tukio la pili la moto kuibuka na kuteketeza majengo. Watoto wetu wameanza kujawa hofu juu ya usalama wao, tunaomba Serikali ifuatilie matukio haya,” amesema Happiness.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Manispaa ya Bukoba, Francis Nshaija amesema baada ya bweni hilo kuteketea, wazazi wanatakiwa kuwachukua watoto wao, ili wasome kwa kutwa hadi pale ukarabati ama ujenzi wa bweni jipya utakapofanyika.

Pia amewataka wenye taarifa za chanzo cha moto huo kutoa ushirikiano kwa vyombo vya uchunguzi, ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.

“Naomba mchukue hatua za kuwafichua wote hata kama ni mwalimu, hapa hakuna jini linaloweza kuja na kuchoma mabweni haya nahisi kuwa chanzo cha moto huu mnakijua. Kama kuna anayefahamu mhusika njoo unipe taarifa tuchukue hatua za kisheria.” amesema Nshaija.

Related Posts