WINGA Mkongomani Ellie Mpanzu tayari yuko Ubelgiji, anakotaka kujiunga na klabu ya KRC Genk, lakini hapa Tanzania kaziacha klabu mbili kwenye mataa zikibaki na fedha zao.
Iko hivi. Hapa nchini, klabu za Simba na Singida Black Stars ndizo zilizokuwa zikipigana vikumbo kumwania winga huyo na kila moja ikiweka nguvu yake ya fedha.
Simba ndio iliyoanza na ofa ya dola 50,000 (Sh 133.3 milioni), huku ikitaka kumlipa mshahara wa dola 5,000 (Sh 13.3 milioni) kwa mwezi, huku ikitaka kumpata mkataba wa miaka miwili aitumikie klabu hiyo.
Hata hivyo, uongozi wa winga huyo, ukagomea ofa hiyo wakitaka walipwe dola 150,000 (Sh340 milioni) ambazo zilitakiwa kugawanywa kwa makundi mawili, klabu yake ya zamani na AS Vita.
Baada ya ofa ya Simba, Singida nao wakaingilia dili hilo na kumpa ofa ya kufuru winga huyo wakitaka kumsajili kwa miaka mitatu kwa ofa ya jumla ya dola 235,000 (Sh627 milioni).
Ndani ya ofa hiyo dau hilo lilitakiwa kulipwa kwa awamu tatu, ambapo Mpanzu angepokea Dola 65,000 (Sh173.3 milioni ) kwa mwaka wa kwanza wa mkataba huo.
Mwaka wa pili Mkongomani huyo, angepokea awamu ya pili ya malipo ya Dola 70,000 (Sh187 milioni) kisha mwaka wa mwisho angepokea dola 100,000 (Sh267 milioni).
Achana na mkwanja huo wa ada ya usajili, mshahara wa winga huyo kwa Singida nao ulikuwa ni kufuru nyingine ambapo mwaka wa kwanza angeanza na dola 8,000 (Sh21.3 milioni) kwa mwezi.
Mwaka wa pili wa mkataba wake pia mshahara wake ungekuwa unaongezeka angechukua dola 9,000 (Sh24 milioni) kisha mwaka wa mwisho angepokea dola 10,000 (Sh 27 milioni) kwa mwezi.
Hata hivyo, Singida ilimbana winga huyo ikimtaka kuzingatia kiwango chake ambapo endapo angekuwa na kiwango cha kawaida ongezeko hilo lisingeweza kufanyika.
Ofa hiyo ya Singida ndio iliyowatibulia Simba, ikiwashtua mabosi Wakongomani hao wakiona kumbe Tanzania kuna pesa za kutosha na kuamua kuwapandishia Wekundu hao dau na kutaka hadi Dola 250,000 (Sh667 milioni) hatua ambayo ikaweka ugumu kwa vigogo hao kukubaliana na hilo.
Licha ya Singida kulazimika kutumia ushawishi huo wa nguvu ya fedha ili imnase Mpanzu, lakini Mkongomani huyo alionyesha kushawishika kwa fedha tu za Singida, lakini alikuwa hataki kwenda kwa matajiri hao wa Singida, akiona afadhali akacheze Simba akiona ni klabu kubwa nchini.
Lakini wakati akiwa na hesabu hizo, viongozi wake wakaweka tamaa na hapo ndipo familia yake ikaingilia kati na kumtaka atimkie Ulaya alikokuwa akikuota kwa muda mrefu (kama alivyonukuliwa na Mwanaspoti la jana).
Kitu cha ajabu wakati Simba na Singida zikikimbizana, Yanga na Azam wao walikaa mbali na dili hilo ingawa Wakongomani hao walikuwa wakitamani vigogo hao nao wapige hodi ili kumpandisha thamani winga huyo.