MTALII mmoja amefariki dunia na wengine sita wamejeruhiwa katika ajali gari iliyotokea jana Jumapili saa 10 jioni kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu na Afisa Uhusiano Mkuu Kitengo cha mawasiliano kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Catherine Mbena amesema gari hilo la watalii lenye namba za usajili T603 DCL mali ya Kampuni ya Yonda Africa lilipata ajali likiwa njiani kurudi hotelini kilomita moja kutoka Lobo Wildlife Lodge.
Amesema katika gari hiyo ilikuwa na watalii saba wenye asili ya China na dereva raia wa Tanzania.
“Mgeni mmoja alifariki dunia, na wengine sita walipata majeraha. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Mugumu na majeruhi sita waliendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo.
“Uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka zingine ili kubaini chanzo cha ajali hiyo,” amesema.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Nyerere, Edgar Muganyizi amewaeleza waandishi wa habari kuwa kati ya majeruhi hao sita, watano wamepewa rufaa kwenda Nairobi kwa ajili ya matibabu.
Amewataja majeruhi waliopata rufaa ni Yong’Jun Zhou, Chen Bei’Zhen, Guang Chen Xin, Yan Yan Chen na Bu Ke Li na kuongeza kuwa watasindikizwa kwa gari la wagonjwa hadi Uwanja wa ndege wa Sasakwa kwa ajili ya kusafirishwa kwa ndege maalum kwenda Nairobi kwa matibabu zaidi.