Ng’ombe 20 wa supu kuchinjwa Jangwani

UONGOZI wa Yanga unatarajia kuchinja ng’ombe 20 kwa ajili ya kugawa supu kwa mashabiki wa timu hiyo kabla ya tamasha la Wiki ya Mwananchi, Agosti 4 mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Mwananchi ambapo ametaja matukio manne watakayoyafanya kabla ya tamasha hilo.

Kamwe amesema wanatarajia kuanza kwa kufanya usafi kwenye Hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam, siku ya Jumatano na Alhamisi watachangia damu kwa watu wenye uhitaji.

“Tulikuwa kimya, leo sasa ndio tumezindua rasmi Wiki ya Mwananchi tamasha maalumu kwa ajili ya kutambulisha kikosi chetu cha msimu kwa kufanya matukio hayo muhimu,” amesema.

Pia amesema Ijumaa watafanya dua maalumu kwa ajili ya kuwaombea watu wote waliotangulia mbele za haki, kuiombea timu, wachezaji, viongozi na mashabiki.

“Siku ya Jumamosi kutakuwa na tukio kubwa ambalo litakuwa maalumu kwa ajili ya kurudisha nguvu za wanachama na mashabiki zetu tukianza na kukimbia na baadaye Jangwani kutakuwa na supu,” amesema.

“Kwa taarifa nilizonazo nimesikia ng’ombe 20 watachinjwa Wananchi tutakunywa supu tayari kwa ajili ya siku yenyewe ya Jumapili ambayo itakuwa ni sikukuu yetu ‘Wiki ya Mwananchi’.”

Related Posts