Ni Yanga na Red Arrows Yanga Day

Ni Rasmi klabu ya Yanga imethibitisha kuwa itacheza na timu ya Red Arrows ya Zambia, kwenye kilele cha Mwananchi Day kitakachofanyika Jumapili Agosti 4, mwaka huu.

Red Arrows, mabingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame 2024) watacheza na Yanga ambayo pia imetoka kutwaa ubingwa wa Toyota Cup Afrika Kusini.

Akizungumza na wanahabari, Mhamasishaji wa Yanga, Haji Manara amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuishuhudia timu yao iliyojitengenezea ukubwa kutokana na kikosi bora ilicho nacho.

“Yanga imemfunga Kaizer Chiefs mabao manne na mashabiki wa timu iliyofungwa walijaza uwanja. Naomba mashabiki wetu pia Jumapili mjitokeze kwa wingi kuiona Yanga iliyojengeka,” amesema na kuongeza:

“Ni aibu kwa wanayanga kushindwa kuujaza uwanja wa Mkapa licha ya kuwa na kikosi bora ambacho kimejengwa na uongozi sambamba na benchi la ufundi kwa ajili ya kutoa raha kwa wananchi.”

Manara amesema amejipanga siku hiyo kuwa na sapraizi ambazo hajawahi kuzifanya kwa misimu yote iliyopita na kwamba amewaandalia mashabiki wa timu hiyo kitu kikubwa. Hata hivyo hakikukitaja ni kitu gani.

Mwaka jana Yanga iliialika Kaizer Chiefs kwenye tamasha kama hilo na kuifunga bao 1-0 lililofungwa na Kennedy Musonda.

Related Posts