PAZIA la Tanzania kwenye michezo ya Olimpiki linafunguliwa leo kwa judoka, Andrew Mlugu kuchuana katika hatua ya 32-Bora.
Mlugu kama atashinda hatua hiyo atatinga hatua ya 16-bora leo leo na akifanya vizuri ataendelea hivyo hadi fainali na mabingwa kuvikwa medali leo.
Mwanajudo huyo aliye kundi C katika hatua ya 32-bora ataanza kwa kupambana na Tai Tin William wa Samoa.
Akizungumza na gazeti hili kutoka Ufaransa inapofanyika michezo hiyo, Mlugu amesisitiza ushindi akibainisha kwamba pambano lake la kwanza linahitaji ufundi zaidi na mbinu.
“Nimemsoma mpinzani wangu, ubora wake na rekodi zake si za kutisha sana, ni kama ubora wa judoka wa nchi hiyo na sisi vinaendana tu,” alisema.
Mlugu ambaye kama atapenya katika hatua zote tano hadi fainali atakuwa amecheza kwa dakika 20.
Kocha wa judoka huyo, Innocent Mallya alisema kila hatua atakayofika, Mlugu atacheza kwa dakika nne kutafuta tiketi ya kucheza hatua inayofuta.
Alisema jana Jumapili, Judoka huyo alipima uzito ya afya tayari kupanda ulingoni leo kwenye ukumbi wa Champs-De-Mars kuanzia saa 5 asubuhi ya Tanzania.
Alisema wameshajipanga namna ya kupambana na mpinzani ambaye wamemsoma ni judoka wa darakalama a Tanzaa, “naye ni daraja letu hapo kushindana ni akili zaidi.
“Mipango yetu ni kufika finali kesho (leo) tutakuwa na mchezo wa kutumia akili nyingi, mbinu na nguvu kidogo.”
Akimzungumzia kiufundi, kocha Mallya alisema kambi ya mwaka mmoja, Ufaransa imemjenga zaidi mchezaji huo.
“Kambi yake imekuwa na tija, imeleta mabadiliko makubwa kwa mchezaji, kuanzia katika vifaa, mazoezi yake na hata mpangilio wa vyakula na sasa yuko tayari kwa mashindano.
Mbali na Judoka huyo, kesho Jumanne muogeleaji Collins Saliboko atakuwa akichuana katika mita 100 free style.
Saliboko aliliambia gazeti ili kwamba hana hofu, amejiandaa na ndoto yake ni kufanya vizuri kwenye michezo hiyo.
Nyota mwingine, Sophia Latiff atachuana Ijumaa ijayo katika mtindo wa mita 50 freestyle.
Mlugu, Saliboko na Latiff wote wanashirki Olimpiki hiyo kupitia nafasi za upendeleo baada ya kutofuzu kwa wanamichezo hiyo katika mashindano ya mashirikisho yao ya kimataifa.
Wengine waliofuzu Olimpiki ya msimu huu ni wanariadha Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri na Jackline Sakilu ambao watachuana kwenye mbio ya marathoni Julai 10 na 11 kwa wanaume na wanawake.