Othman aeleza mbinu ya watu kujiajiri, kuajiriwa

Pemba. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud amesema Serikali haina ajira bali ‘ujanja wa kuajiri watu’ ni kutengeneza uchumi imara ili wajiajiri.

Pia, amewataka vijana wasirubunike na wajitafakari mara mbili pindi wanapoletewa kadi wakiahidiwa ajira.

Othman ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Julai 29, 2024 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Shule ya Laurent Chakechake Pemba katika mwendelezo wa mikutano ya chama hicho.

Amesema wananchi wasichukulie harakati za chama hicho kama mkumbo au siasa kwa kuwa, dhamira yake ni kuiweka Zanzibar katika sura ya kimataifa na kutengeneza uchumi imara utakaowaondoa katika umaskini.

“Ahadi ya chama chetu, mmetupa kazi na tunatafakari kila siku tuwaombe na ninyi msiige mambo haya mkasema mnafuata mkumbo yatafakarini, ukiletewa kadi tafakari, ukiambiwa utapewa ajira jiulize ajira hiyo itapatikana wapi kwa kuwa Serikali haijiri, ujanja wa kuajiri watu ni kutengeneza uchumi, watu wakapata kuajiriwa na ndio dunia ya leo inavyokwenda,” amesema. 

“Naomba niwaambie sisi tumedhamiria na tumelichukua jambo hili kwa dhati, kwa sababu linatuuma sisi wengine tumepoteza umri wetu kwa kupambania nchi hii.”

 Amesema iwapo mtu akitaka kufanya jambo hususani katika ulimwengu wa sasa lazima atafakari na ajijue yupo katika misingi ipi na akishajua hivyo hatadanganywa tena.

 “Maana utajua kwa nini unaamini katika jambo fulani, kwa sababu unachotaka cha kwanza ni nchi yako.”  

Amesema amekuwa katika Tume ya Pamoja ya Fedha kwa kipindi cha miaka 10 wakipambania haki za Zanzibar na walitoa ripoti mwaka 2006 namna haki za Zanzibar na Bara vipi zigawane lakini kwa sasa hakuna kinachoendelea.

 Othman ambaye alikuwa mkurugenzi wa mashtaka kwa miaka 10, amesema katika utawala wa Rais wa Awamu ya Sita, Amani Abeid Karume aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara Utawala Bora na walimshauri kuanzisha ofisi huru ya mashtaka.

 Amesema Karume alikubali akaunda ofisi hiyo huku akimteua Othman kuwa mkurugenzi wa kwanza kuendesha ofisi hiyo iliyozaa matunda, kwa kuwa kwa mara ya kwanza waliwashtaki watu waliodhani hawawezi kufanywa chochote baada ya kuchoma hoteli mchana kweupe.

Jambo lingine walimshauri kuanzisha Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ijitegemee kutoka Wizara ya Fedha kwa sababu kulikuwa na ufisadi mkubwa, pia Karume alilitekeleza huku akiunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

 Amesema Karume alifikia hatua hiyo baada ya Rais wa Awamu ya Pili Hayati Ali Hassan Mwinyi kumshauri kiongozi huyo kwamba Zanzibar imeumizwa kwa muda mrefu kwa hiyo anatakiwa kuiponya na atekeleza ushauri huo.

 “Huu ndio uungwana, alishauriwa akatekeleza na matunda yake tuliyaona, lakini kwa nini wengine wanapata kigugumizi, lakini kikubwa hapa ni kwamba watu hawana wivu wala uchungu na nchi hii,” amesema.

 Hata hivyo, amesema iwapo ACT- Wazalendo ikishinda hawatakaa wakazungumza, bali mazungumzo yataishia kwenye sanduku la kura.

 Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Ismail Jussa amewataka Wazanzibari kuendelea kumuunga mkono na kumpa ushirikiano Othman kwa kuwa ni kiongozi mwenye nia na msimamo wa kweli katika kuwatetea Wazanzibari.

Pia, amesema ana ni ya Zanzibar kutimiza dhamira ya chama hicho ya kuleta mabadiliko ya kweli kimaendeleo.

Awali, mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Mansour Yousuf Himid aliwataka Wazanzibari kutohadaika kwa kutegemea kupatiwa ajira na mafanikio na kwamba ni muhimu kuwa na mamlaka ili kuudhibiti uchumi wa Zanzibar uweze kuwanufaishi wananchi wenyewe.

Related Posts