KATIKA wimbo wa Bongo Dar es Salaam wa Profesa Jay wa mwaka 2001 ndani ya albamu ya Machozi, Jasho na Damu, mkali huyo wa mashairi alihadithia ujanja ujanja wa kimjini unaopatikana Dar es Salaam karne ya 21.
Profesa Jay ambaye alitoka kubadilisha jina kutoka Nigger Jay, aliimba maneno yafuatayo kuelezea mikasa ya kimjini iliyokuwa ikiendelea Dar es Salaam:
“Ngoma inakuwa nzito mnapokutana matapeli
Akili kumkichwa ukilemaa umeachwa ferry
Aliyeuziwa cheni katoa hela bandia
Aliyepokea hela naye kauza cheni ya bandia.”
Hiki ndicho kinachoendelea kwenye usajili wa Klabu ya Simba. Klabu hiyo inayotaka kujijenga upya kuelekea msimu mpya wa 2024/25 baada ya kuyumba kiasi ndani ya misimu mitatu iliyopita imekutana na mkasa wa mustakabali wa masupastaa wa Bongo kama alivyosema Profesa Jay.
Simba wamewachukua wachezaji wa timu zingine kiujanja janja kama yule aliyetoa hela bandia baada ya kuuziwa cheni.
Valentino Mashaka wa Geita Gold alikuwa bado ana mkataba na klabu hiyo, Simba ikadaiwa kwamba bila kufanya mazungumzo nao wakamsajili na kumtangaza.
Lameck Lawi wa Coastal Union alitangazwa na Simba kama usajili mpya huku ikidaiwa wakijua fika kwamba hawakufanya kama walivyokubaliana na Coastal Union kwenye mauziano ya mchezaji huyo.
Awesu Awesu wa KMC alitangazwa na Simba kama usajili mpya ilhali mchezaji huyo akidaiwa bado ana mkataba na klabu yake.
Wakati Simba SC wakidaiwa kuyafanya hayo, watu wengine wakapita nyuma yao na kuwapiga tukio kama hilo. Nyota wao Kibu Denis maarufu kama Kibu Mkandaji au Kibudenga akapotea kimaajabu na taarifa za ‘kiintelijensia kutonya kwamba kaenda Norway.
Hapo Simba wakawa wamepewa cheni bandia baada ya kuwa nao walitoa hela bandia. Hata hivyo, mwisho wa siku hakuna atayefanikiwa katika hawa kwa sababu usajili wa ujanja ujanja haupo tena miaka hii. Hayo mambo yaliwezekana katika zama za giza wakati ule wachezaji hawana mikataba, bali makubaliano ya maneno.
Yaliwezekana nyakati zile ambazo hakukuwa na mifumo ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ya usajili na badala yake makaratasi ya Chama cha Soka Tanzania (FAT) tu pale Karume, Dar es Salaam.
Kwa mfano, mwaka 1982 Simba iliamua kufanya kama safari hii kujenga upya kikosi baada ya kile kilichotawala kutwaa ubingwa mfululizo kuanzia 1976 hadi 1980 kuzeeka.
Wakasajili vijana wengi kutoka timu ya taifa ya vijana wakiwemo kina Zamoyoni Mogella ambao walitoka Norway kwenye kambi maalumu ya mwaliko. Hata hivyo wakati ule timu iliruhusiwa kusajili wachezaji 25 tu, lakini Simba ilisajili zaidi ya 30.
Majina yakapelekwa FAT kwa ajili ya kupata leseni za kuchezea msimu mpya, lakini FAT wakawaambia wapunguze kwanza wachezaji hadi wabaki 25 ndipo wapate leseni.
Simba wakarudisha idadi ileile bila kupunguza hata jina moja. FAT wakawarudishia tena, na wakafanya hivyo mara tatu. Baada ya hapo FAT wakawaona Simba wakaidi, hivyo wakachukua hatua.
Wakahesabu kuanzia moja hadi ishirini na tano wakapiga mstari mwekundu. Waliozidi wakawaachwa. Bahati mbaya Simba wenyewe hawakuweka orodha yao kutokana na umhuhimu bali shagharabaghara.
Kwa hiyo ule mstari mwekundu wa FAT ukawakuwata wachezaji wengi nyota na muhimu wakiwa nje ya orodha iliyopitishwa.
Mechi ya kwanza ya msimu Simba wakacheza na CDA ya Dodoma wakafungwa mabao 6-1.
Simba wakawa wakali kwamba FAT imewahujumu kwa kuwakata wachezaji wao muhimu, wakaenda kulalamika kwa waziri mwenye dhamana ya michezo, naye akayafuta matokeo yale na kuamuru ligi isianze kwanza hadi usajili wa Simba ushughulikiwe.
Lakini hayo ni mambo ya zaidi ya miaka 40 iliyopita. Hivi sasa hayawezi kuruhusiwa kutokea. Hakuna tena ujanja ujanja, na kwa taratibu waziri hawezi kufanya vile tena.
Wachezaji kama Kibu Denis na klabu kama Simba kwa pamoja wanatakiwa kufuata taratibu za uhamisho kwa hawa wachezaji.
Mchezaji akisema yuko huru msimuamini kwa maneno yake, bali lazima awaonyeshe barua ya kuachana na klabu yake ya awali (release letter).
Mustakabali wa masupastaa wa Bongo hauwezi kupata nafasi tena kwenye mpira wa sasa. Ukitoa hela bandia utakamatwa na ukiuza cheni bandia utakamatwa.