Dar es Salaam. Kuongezeka kwa kipato kwa baadhi ya Watanzania kumetajwa kuwa moja ya sababu ya kutokupenda kula vyakula vya jamii ya mikunde na kuona chakula hicho ni maalumu kwa watu duni.
Kuongezeka kwa kipato kumekuwa kukiwafanya watu kuona kula nyama ndiyo sawa, huku wakiona kula vyakula jamii ya mikunde ni kuwa na hali duni.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu Julai 29, 2024 katika mjadala wa X Space (zamani Twitter) ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) ikiwa na mada inayosema ‘Fahamu faida za kiafya za ulaji vyakula jamii ya kunde, karanga na mbegu za mafuta.’
Mtaalamu wa Lishe kutoka Shirika la Chakula Duniani (FAO), Stella Kimambo amesema: “Vyakula hivi vina ubora katika afya zetu na vinaliwa na watu wote, unakuta hata watoto wanapenda, imefika hatua mtu akipata mgeni akikuta amepika choroko, maharage anasikitika, anatamani ampikie kuku.”
Amesema uandaaji pia ni changamoto inayowafanya wengi wasile mboga za aina hiyo, kwani huchukua muda mrefu kuzipika, huku akitolea mfano maharage, hivyo kumfanya mtu kuona bora apike chipsi mayai atakayotumia muda nfupi.
“Pia kuna matatizo ya kiafya ambapo wengine wakila wanapata hali ya gesi, tunashauri vyakula kama maharage kama vinawasumbua wamwage maji mara ya kwanza na pili, ili waweze kula bila kupata matatizo,” amesema.
Stella amesema vyakula hivyo ni muhimu katika ukuaji wa ubongo wa mtoto na kuimarisha ukuaji wa ufahamu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mimea Jamii ya Kunde Tanzania (TPN), Zirack Andrew amesema mazao hayo yamesahaulika kwa miaka mingi, licha ya kuwa ndiyo ya asili na maharage yaliyozoeleka ni zao la nje.
Amesema asili ya kunde na mbaazi licha ya kuliwa sana na nchi za mbali, lakini asili yake ni Afrika Mashariki.
“Maharage kwa asili yake yameletwa na ushawishi wa tawala za kikoloni, kabla wakoloni hawajaja tulikuwa tunakula zaidi mtama, ulezi na kunde, lakini wakoloni walipokuja waligundua uzalishaji wake si mkubwa wa kukidhi mahitaji, jambo ambalo lilifanya waanze kuagiza mahindi na maharage kutoka Mexico kwa ajili ya kulisha wanafunzi, manamba na wanajeshi,” amesema Andrew.
Amesema hali inayoonekana sasa ni matokeo ya ukoloni ulioletwa Tanzania, hivyo sasa wanajaribu kutoa elimu kwa wadau watambue mazao haya si ya kigeni, bali ni ya Tanzania.
Mhariri wa jarida la afya gazeti la Mwananchi, Herrieth Makwetta amesema kwa watu wasiokula nyama au wana uwezo mdogo kujipatia nyama, mbegu za jamii ya mikunde zinatosheleza mahitaji ya protini.
“Vyakula vyote vya jamii ya kunde ni nafuu na vitamu vikiwa na kiwango kikubwa cha protini na hivyo kuweza kutumiwa mbadala ya nyama,” amesema Makwetta.
Amesema aina zote za kunde zina lishe bora, vitamini nyingi, mafuta kidogo na bei nafuu ikilinganishwa na nyama, lakini katika ulaji umezoeleka kwa baadhi ya wazazi wanawapatia watoto mchuzi wa maharage au kunde na si maharage yenyewe, hii ni changamoto.
Hivyo, mikunde ni muhimu na ndiyo sababu imewekwa kwenye makundi matano ya vyakula, ikiwemo vyakula vya nafaka mizizi na ndizi, matunda, mboga mboga, jamii ya mikunde na vyenye asili ya wanyama, mafuta na sukari bila kusahau maji safi ya kunywa.
Ofisa Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (Tari), Theresia Jacob amesema, ili mkulima avune kwa tija wanatakiwa kuacha masalia ya mazao ya jamii ya mikunde shambani, ili kusaidia udongo kuwa na rutuba.
“Kuacha masalia shambani ni moja ya namna bora ya kuboresha udongo na kuurutubisha ambao unamfanya mkulima kulima kwa tija na kupata mazao ya kutosha,” amesema Theresia.
Mbali na hilo, amesema miongoni mwa changamoto zinazowakumba wakulima wa mazao ya jamii hiyo ni mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha ukame, mafuriko, wadudu na magonjwa mbalimbali yanayosababisha kuathiri mimea ikiwa shambani,” amesema.
Naye, Mtafiti na Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi na Chakula kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dk Analice Kamala amesema pamoja na faida zote za jamii ya mikunde, karanga na mbegu za mafuta sumukuvu bado ni changamoto ambayo huathiri zaidi karanga na mbegu za mafuta, wakati mikunde ina uwezo wa kujipambania yenyewe.
Amesema zipo sumukuvu za aina nyingi na hutegemeana na aina ya mazao, huku akiitaja aflatoxin inayozalishwa na fangasi wanaoota kwenye mazao yaliyokauka na zinakuwa na athari za moja kwa moja katika ini, pia huingilia mfumo wa ukuaji wa watoto.
“Katika hili kuna madhara ya muda mrefu na muda mfupi, ya muda mrefu ndiyo yenye changamoto sana husababisha saratani ya ini na udumavu kwa watoto wa miaka mitano, kwani inapunguza kinga ya mwili na kufanya wapate magonjwa ya mara kwa mara,” amesema Dk Kamala.