Serikali kutafuta mwarobaini changamoto mifumo ya kikodi

Dar es Salaam. Huenda changamoto za mifumo ya kikodi kwa wafanyabiashara nchini zikapata ufumbuzi, baada ya Serikali kutangaza kuunda kamati itakayochunguza na kubaini changamoto za utekelezwaji wa sera na sheria katika mifumo hiyo.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kamati hiyo itakayohusisha wajumbe kutoka serikalini na sekta binafsi, itapendekeza mfumo stahiki wa kikodi unaoendana na Tanzania.

Uamuzi huo unafanywa wakati ambao kumekuwa na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu changamoto katika mifumo ya kikodi ambayo imekuwa shubiri kwa wafanyabiashara.

Kabla ya Rais Samia kutangaza hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Ali Suleiman Amour alieleza kufungiwa kwa akaunti za benki, kuchukuliwa fedha bila utaratibu sahihi na kufungiwa kwa mashine za EFD kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazoshabihiana na mifumo ya kikodi.

Rais Samia ametangaza kuundwa kwa kamati hiyo leo Jumatatu Julai 29, 2024 alipohutubia mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambalo yeye ni mwenyekiti wake, Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Serikali imedhamiria kuondosha changamoto, tutaunda kamati itakayoshirikisha wajumbe kutoka serikalini na sekta binafsi, mpitie kwa undani kisha mtuletee mapendekezo na ushauri mtakaouona unafaa kwa nchi yetu kwenda na mfumo huo wa kodi,” amesema.

Kwa mujibu wa Rais Samia, ni adhima ya Serikali kujenga uhusiano mzuri na wenye manufaa na sekta binafsi, ili kuongeza mapato kupitia biashara.

Ameeleza anachokitaka ni kuona sekta ya umma inawezesha sekta binafsi, ikiwemo kupatikana kwa rasilimali watu wenye ujuzi.

Sambamba na hayo, mkuu huyo wa nchi amesema anafahamu uwepo wa changamoto katika maeneo mbalimbali na kwamba ataendelea kuzifanyia kazi.

Amesema pia anafahamu uwepo wa baadhi ya watendaji serikalini wasiofahamu dhamira ya kuwezesha biashara na uwekezaji.

“Nafahamu changamoto ya uratibu kati ya sekta moja na nyingine, gharama za stempu za kodi, ucheleweshaji wa vibali mbalimbali na wakati mwingine kutoshirikishwa (kwa wafanyabiashara) kwenye baadhi ya mabadiliko,” amesema na kuongeza kuwa anaamini ufumbuzi wa changamoto mbalimbali utapatikana na kwamba dhamira itaeleweka.

Changamoto za wafanyabiashara

Akizungumza katika mkutano huo, Amour amesema wafanyabiashara wengi waliozungumza nao wanalalamikia kufungiwa akaunti za benki, kuchukuliwa fedha zao bila utaratibu sahihi na kufungiwa kwa mashine za EFD.

Amesema vitendo hivyo vinatia doa uhusiano kati ya wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kwamba kinachosababisha ni upungufu katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438.

Baada ya TPSF kukaa na wafanyabiashara, amesema walibaini walikuwepo ambao hawakuwa na madeni ya kodi na hivyo matumizi ya agency notice haikuwa sahihi kwao.

Kwa mujibu wa Amour, makosa yalibainika kwa TRA hasa katika utunzaji wa kumbukumbu.

“Upungufu katika uthaminishaji wa mizigo bandarini na kamata kamata zilizokuwa zinaendelea Kariakoo zilishinikiza utoaji wa risiti. Tunatarajia utaratibu mpya utasimamiwa vema,” amesema.

Sambamba na hayo, amesema taasisi hiyo imebaini kuongezeka kwa biashara za magendo na bandia ambazo zinaathiri ushindani nchini.

Ameeleza kufurahishwa na uanzishwaji wa ofisi ya msuluhishi wa malalamiko ya kikodi tangu mwaka 2019 na mwaka 2022 ilianza kufanya kazi.

Lakini, amependekeza itoke chini ya TRA kwa kuwa itashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuwa inasimamiwa na yuleyule anayetoza kodi.

Hoja nyingine aliyoiibua ni sekta binafsi kwa sasa inaratibiwa na wizara zaidi ya moja, akitaka kuwepo moja itakayotambulika kwa ajili yao.

Amour pia amependekeza umuhimu wa kuongeza wigo wa walipakodi akitaka angalau wafikie milioni 6.1, badala ya milioni mbili wa sasa.

“Katika hao milioni mbili, ni robo yake ndiyo waadilifu na wanaolipa hiyo kodi,” ameeleza.

Upatikanaji wa Dola za Marekani ni changamoto nyingine iliyoibuliwa na Amour, akisema unaathiri biashara, ununuzi wa malighafi za viwandani na hata upatikanaji wa mafuta.

Ametaka matumizi ya Dola za Marekani hasa kwa Serikali yapunguzwe kwa kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini na si kila mwaka kununua magari mapya kwa watumishi.

Pamoja na mapendekezo hayo, ametaka wafanyabiashara wasigeuzwe maadui, kutengenezewa mizengwe na figisu pale wanapotoa ripoti ya masuala ya rushwa na upotevu wa mapato.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe WhatsApp: 0765864917

Related Posts