Dar es Salaam. Shahidi wa kwanza wa utetezi katika kesi ya mkopo tata baina ya kampuni ya Kahama Oil Mills Limited na wenzake dhidi ya Benki za Equity Tanzania Limited (EBT) na Equity Kenya Limited (EBK), amehitimisha ushahidi wake uliohusisha nyaraka mbalimbali zinazohusiana na mkopo huo.
Shahidi huyo, Michael John Kessy kutoka EBT, amehitimisha ushahidi wake huo leo Jumatatu Julai 29, 2024, baada ya kujibu maswali ya dodoso kutoka kwa wakili wa wadai, Frank Mwalongo pamoja na majibu ya ufafanuzi kutoka kwa wakili wa utetezi, Zaharani Sinare.
Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara, Tanzania na kampuni za Kahama Oil Mills Limited na Kamahama Import & Export Commercial Agency Limited, zinazodaiwa kukopeshwa fedha hizo na benki hizo.
Wadai wengine katika kesi hiyo namba 78/ 2023 ni wadhamini wa mkopo unaobishaniwa; Kom Group of Companies Limited, Shinyanga Royal Pharmacy (2015) Limited, Royal Supermarket (2008) Limited na Mhoja Nkwabi Kabalo, mkurugenzi wa kampuni hizo.
Kesi hiyo ni mwendelezo wa kesi zilizofunguliwa dhidi ya benki hizo na kampuni zinazodaiwa kukopeshwa na benki hizo mabilioni ya fedha, kisha zikazifungulia kesi benki hizo zikipinga kudaiwa kwa madai hazikukopeshwa na benki hizo au zimeshalipa mkopo.
Kampuni hizo zilifungua kesi hiyo baada ya kuandikiwa barua na benki hizo zikiwataka kulipa zaidi ya Dola milioni 46.6 za Marekani (zaidi ya Sh122.54 bilioni).
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Profesa Agatho Ubena, iko hatua ya utetezi ambao umeanza kutoa ushahidi wake baada ya upande wa wadai kufunga ushahidi wake kupinga kukopeshwa na kudaiwa na benki hizo.
Katika hatua hiyo, benki hizo zinazowakilishwa na wakili Zaharani Sinare kupitia mashahidi wake zinatoa ushahidi unaolenga kupangua hoja na madai ya wadai kuwa hazikuwakopesha fedha hizo na kuthibitisha madai yake kinzani kuwa zilizikopesha kampuni hizo kiasi hicho cha fedha na zimekataa kurejesha.
Kwa mujibu wa shahidi Kessy, kiasi hicho ambacho benki hizo zinadai kuwa zinazidai kampuni hizo kinajumuisha deni la msingi la mkopo wa Dola milioni 32 (zaidi ya Sh84 bilioni) ambao benki hizo zinadai zilizikopesha kampuni hizo pamoja na riba.
Katika ushahidi wake, Kessy alianza kufafanua mambo machache katika maelezo ya ushahidi wake aliouwasilisha awali mahakamani hapo kwa njia ya maandishi pamoja na nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa kama vielelezo vya ushahidi, huku akiongozwa na wakili Sinare.
Baada ya hatua hiyo ndipo alipoanza kuhojiwa maswali ya dodoso na wakili wa wadai, Mwalongo kuhusiana na ushahidi wake.
Baada ya kumaliza kuhojiwa maswali ya dodoso, akaongozwa na wakili Sinare kuhitimisha ushahidi wake kwa maswali ya ufafanuzi wa baadhi ya majibu yaliyotokana na maswali ya dodoso.
Katika kuhitimisha ushahidi wake huo, huku akirejea baadhi ya nyaraka hizo shahidi huyo alisisitiza maelezo ya ushahidi wake wa maandishi na maelezo ya ufafanuzi wa msingi kuwa benki hizo zilizikopesha kampuni hizo, lakini kampuni hizo hazikurejesha mkopo huo.
Baada ya shahidi huyo kuhitimisha ushahidi wake, wakili Sinare aliieleza Mahakama hiyo kuwa kesho Jumanne, Julai 30,2024 wataleta shahidi mwingine kuendelea na utetezi.