SIMBA ni wajanja sana. Wanafahamu kwamba wapinzani wao wa jadi, Yanga watakutana nao Agosti 8 kwenye Ngao ya Jamii, wakaamua kufanya sapraizi ambayo wanaamini itawalipa.
Leo Jumanne, Simba ambao wanatimiza wiki ya tatu kamili tangu waanze mazoezi katika kambi nchini Misri, wakiwa huko wamepata akili mpya kuelekea Simba Day ambayo itafanyika siku tano kabla ya kucheza dhidi ya Yanga.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kambi yao iliyopo Mji wa Ismailia nchini Misri, benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids wameziba mianya kuanzia kambini hadi mazoezini hawataki kuona siri zao nyingi za ndani zikivuja.
Mtoa taarifa huyo amebainisha kwamba, usiri unaofanyika kambini ni katika kuhakikisha wanajenga kikosi kitakachofanya vizuri msimu ujao kwa kuanza na ushindi Kariakoo Dabi.
“Kuna usiri mkubwa sana kambini, ndiyo maana unaona mpaka sasa watu wengi hawafahamu ishu nyingi zinazoendelea huku kambini.
“Viongozi wameamua kufanya hivyo kwa sababu kocha amehitaji ili wachezaji kuwa na utulivu unaotakiwa kipindi cha kujiandaa na msimu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Habari zinabainisha kwamba, Simba kuficha silaha zao hawataishia kambini Misri pekee, bali hata wakirejea Dar es Salaam mwendo utakuwa ni uleule.
Mtoa taarifa huyo aliendelea kubainisha kwamba, hata katika mechi ya Simba Day, kocha atafanya ujanja ambao wapinzani wakiangalia mechi hawawezi kupata kitu cha maana sana.
“Timu ikirejea Dar Jumatano, itaendelea na kambi kama kawaida ikiwa kwenye uangalizi maalum, hali hiyo itaendelea hadi tutakapocheza Ngao ya Jamii.
“Hii yote ni katika kuelekea kusaka matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wetu kwenye mechi za kimashindano.
“Tunafahamu kwamba tuna mechi ya kirafiki katika Simba Day na mashabiki wetu wanataka kuwaona wachezaji wao. Wasijali watawaona lakini itakuwa tofauti.
“Unajua mpaka sasa kocha tayari ana kikosi chake cha kwanza, hiyo siku ya mechi katika Simba Day atawachanganya lakini anaweza kuwapa muda mchache wa kucheza ili kulinda wasiumie,” alifichua mtoa taarifa huyo.
Katika hatua nyingine, imeelezwa kwamba Kocha Fadlu anaridhishwa sana na kiwango cha kipa Hussein Abel ambaye msimu uliopita alipata nafasi ndogo ya kucheza kikosini hapo chini ya Kocha Roberto Oliveira na Abdelhak Benchikha.
Kipa huyo ambaye huu utakuwa ni msimu wake wa pili ndani ya Simba, Fadlu anaamini ana uwezo wa kuisaidia timu hiyo katika kusaka matokeo mazuri uwanjani.
“Fadlu ameonekana kuridhishwa na uwezo wa Hussein Abel na amepanga awe kipa wake namba moja, tutaona mbele ya safari itakuwaje lakini kwa sasa ndiyo chaguo lake,” alisema mtu huyo ambaye anafahamu mambo mengi ya benchi la ufundi la Simba.
Ikumbukwe kwamba, Simba imeenda Misri na makipa watatu ambao ni Ally Salim, Hussein Abel na Ayoub Lakred wakati Aishi Manula akiachwa Dar.
Kwa sasa Ayoub inaelezwa ni mgonjwa na anatarajia kukaa nje ya uwanja kwa muda kidogo, hivyo jukumu ya kukaa golini litabaki kwa Salim na Abel watakaokuwa wakishindania nafasi ya kwanza.
Msikie Fadlu kuhusu timu yake
Licha ya kikosi chake kuibuka na ushindi kwenye mechi mbili mfululizo za kirafiki, Fadlu amelia na washambuliaji kushindwa kutumia nafasi.
Simba ilianza kucheza na Canal SC ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 na juzi Jumapili ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Telecom Egypt. Jana ilikuwa na kibarua cha kukabiliana na Al-Adalah FC kutoka nchini Saudi Arabia.
“Hadi sasa nimewini maeneo mawili kuanzia utimamu na kuwajenga kisaikolojia, shida iliyopo ni namna ya kutumia nafasi tu lakini hilo sio gumu kwani kama wanaweza kutengeneza kutumia ni suala la muda,” alisema na kuongeza.
“Wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi lakini wanashindwa kutumia hilo halinipi shida sana kwani licha ya kuzikosa bado wanakuwa kwenye maeneo sahihi kupambana.
“Timu imeimarika kila eneo na wachezaji tayari wameanza kuingia kwenye mfumo, shida ya kutofunga ni sehemu ndogo ambayo inaweza kuisha kwa muda mfupi kwani wachezaji wamekuwa wakijitenga vizuri kwenye nafasi.”
Kocha huyo ambaye ametua Simba kuchukua nafasi ya Abdelhak Benchikha, amesema kwa muda waliokaa Misri tayari ameshuhudia mabadiliko makubwa kikosini na anaamini hadi wakirudi Dar, atakuwa amejenga kikosi bora.