KIKOSI cha Simba jana usiku kilikuwa uwanjani kucheza mechi ya pili ya kirafiki ikiwa kambini, jijini Ismailia, Misri huku mshambuliaji mpya wa kikosi hicho, Mganda Steven Mukwala akifichua namna alivyofurahishwa na maandalizi ya timu hiyo, akiahidi kuwafanyia sapraizi mashabiki wa klabu hiyo.
Mshambuliaji huyo alijiunga na Simba, hivi karibuni akitokea timu ya Asante Kotoko ya Ghana na kuwa mmoja ya wachezaji waliofika mapema kambini Misri kujiandaa na msimu mpya wa mashindano na taarifa zinasema amekuwa akionyesha vitu adimu mazoezini kiasi cha kuvutia makocha wa timu hiyo.
Hata hivyo, akizungumza na Mwanaspoti kutoka Misri, Mukwala alisema, licha ya ugeni wake ndani ya timu hiyo na kutozoeana na wachezaji wenzake, amefurahia namna walivyompokea jambo linaloonyesha watafanya vizuri.
“Kwa sasa sitaki kuwaahidi mashabiki jambo lolote kwani msimu haujaanza ila wajue kabisa nina sapraizi yao na watambue mambo mazuri yanakuja, uwepo wangu na wachezaji wenzangu hapa ni ishara tosha tunapaswa kuipambania timu ili ifanye vizuri zaidi ya msimu uliopita.”
Mukwala aliongeza kucheza kwake ndani ya kikosi hicho anajisikia kama yupo nyumbani kwa sababu ya mapokezi mazuri ambayo ameyapata kutoka kwa wachezaji wenzake, viongozi na benchi la ufundi kiujumla hivyo atapambana kadri awezavyo.
“Kila kitu kinaenda vizuri na viongozi wamekuwa nasi bega kwa bega kuhakikisha tunatoa kilicho bora kwa mashabiki wetu, naamini msimu ujao utakuwa ni mzuri kwani jambo linalonifanya kuamini ni kila mmoja wetu anavyopambana mazoezini.”
Kwa upande wa aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ alisema, hana shaka na uwezo wa mchezaji huyo na ikiwa ataaminiwa na kupewa muda zaidi atakuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Simba.
Mukwala ni mshambuliaji wa kati mwenye miaka 24 na urefu wa futi 5.6 ambaye amezaliwa mjini Makindye kwao Uganda mwaka 1999, huku akisifika zaidi kwa kasi na nguvu awapo uwanjani na uhodari wake wa kufunga mabao mengi kwa kutumia kichwa.
Nyota huyo ametua Simba huku akikumbukwa zaidi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 14 akiwa na kikosi cha Asante Kotoko ya Ghana nyuma ya kinara mshambuliaji wa Berekum Chelsea, Stephen Amankonah aliyefunga mabao 16, akiichezea timu hiyo.
Pia aliibuka mchezaji bora wa Ligi ya Ghana Desemba mwaka jana akiwa na kikosi hicho cha Asante Kotoko alichojiunga nacho Agosti 2022 akitokea URA ya Uganda na katika msimu wa kwanza alifunga mabao 11 na asisti tano.
Akiwa URA, Mukwala alicheza kwa misimu mitatu kuanzia mwaka 2020 ambapo msimu wa kwanza wa 2019/2020 aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda akifunga mabao 13 na msimu wa 2020/2021, akafunga 14 kisha 2021/2022 akatupia tena kambani mabao 13.
Straika huyo alianza soka la ushindani mwaka 2017 alipojiunga na Vipers akitokea Masaza FC, kisha akatua Maroons FC na akarejea Vipers na baadaye URA, pia amepita kwenye timu zote za taifa za Uganda kwa vijana na sasa ni tegemeo kwa Uganda Cranes.