TMX yawezesha kupatikana zaidi ya Shilingi Bilioni 490, fahamu zaidi

Kiasi cha fedha Zaidi ya Shilingi Bilioni 490 kimepatikana kupitia mauzo ya zao la ufuta kiasi cha tani 125,00 msimu 2024/2024 kupitia minada iliyoendeshwa na vyama vikuu vya Ushirika vipatavyo 10 katika mikoa saba inayolima ufuta nchini.

Hayo ni kwa mujibu wa Afisa usimamizi fedha soko la bidhaa Tanzania (TMX) Bw. Prince Philemon wakati akizungumza baada ya kukamilika kwa manada wa mwisho wa ufuta uliosimamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU na kufanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Mtwara Julai 26, 2024

Prince ameeleza kuwa mafanikio hayo makubwa yaliyofikiwa katika minada ya msimu huu, yametokana na utayari wa wakulima pamoja na vyama vyao kutoa ushirikiano uliowezesha mfumo mpya wa mauzo kuendeshwa bila vikwazo vyovyote.

Amewashukuru wadau wote pamoja na serikali kwa kuonesha utayari wa kushirikiana na wataalam wa soko la bidhaa nchini, hali ambayo imepelekea kufanyika kwa minada katika mikoa saba, huku chama kikuu cha MAMCU pekee kikiendesha minada saba kwa mafanikio makubwa.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara Mwinyi Ahmed Mwinyi, amesema kuwa msimu wa ufuta 2024/2025 umekuwa wenye mafanikio makubwa, na Serikali ya wilaya inawapongeza waukilima, Vyama vya Msingi, watumishi wa Serikali pamoja na MAMCU.

Kuhusu uzalishaji amesema umeongezeka kwa Zaidi ya tani elfu 10, kutoka wastani wa tani 17,000 msimu wa 2023/2024 hadi tani Zaidi ya 27,000 msimu 2024/2025 likiwa ni ongezeko la kiwango cha juu ndani ya msimu mmoja.

Afisa Masoko wa MAMCU Bi.Neema Honoris ameishukuru Serikali pamoja na viongozi wa Ushirika kwa juhudi za kuhakikisha kuwa zao la ufuta linazidi kupata thamani na kuwanufaisha wakulima katika wilaya zote zinazohudumiwa na MAMCU.

.
.
.
.

Related Posts