Muda mfupi baada ya Tume ya Uchaguzi ya Venezuela kumtangaza Maduro kama mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata asilimia 51 ya kura, akimshinda mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez ambaye alipata asilimia 44 ya kura katika matokeo yaliotangazwa hapo jana Jumapili upinzani umeyapinga matokeo hayo ukisema kulikuwa na udanganyifu mkubwa.
Tume ya Uchaguzi CNE ilisema matokeo hayo iliyoyatangazwa yalikusanywa kutoka asilimia 80 ya vituo vya kupigia kura ikiashiria mwelekeo usioweza kutenguliwa.
Ikumbukwe kwamba tume hiyo ya uchaguzi ambayo inadhibitiwa kwa kiasi kikubwa na wafuasi watiifu kwa Maduro, haikutoa idadi rasmi ya matokeo kwa kila kituo cha kupigia kura ambapo kwa jumla kulikuwa na vituo 15,797 kwa nchi nzima, hatua ambayo inazorotesha jitihada za upinzani kuweza kuyapinga matokeo kisheria.
Muungano wa upinzani wa taifa hilo la Amerika ya Kusini ulidai kupata ushindi wa kishindo, baada ya kampeni za uchaguzi zilizozongwa na madai ya vitisho vya kisiasa na hofu ya udanganyifu.
Soma pia:Rais Maduro wa Venezuela achaguliwa kwa muhula wa tatu
Wachambuzi wa wafuatiliaji wa siasa nchini humo wakiashiria kwamba Maduro angelishindwa katika uchaguzi huo lakini isingilewezekana kwake kukubaliana na matokeo baada ya zaidi ya muongo mmoja madarakani.
Kiongozi wa Muungano wa Upingani Venezuela Maria Corina Machado amesema kwa mujibu wa taarifa walizokusanya ikiwa ni pamoja na asilimia 40 ya karatasi zinazoorodhesha hesabu jumla za kura zinaonesha wamepata ushindi katika uchaguzi huo.
“Sijui matokeo mengine yalitoka wapi. Tunazo tunazo karatasi zote za kujumlisha matokeo. Na kulingana na taarifa hii. Edmundo Gonzalez Urrutia alipata asilimia 70 ya kura katika uchaguzi huu na Nicolas Maduro alipata asilimia 30 ya kura na huu ndio ukweli.”
Kupitia ukurasa wake wa X Gonzales ambaye ni mwanadiplomasia wa zamani mwenye umri wa miaka 74 aliandika na hapa namnukuu “mapambano yetu yanaendelea, na hatutapumzika hadi wanbachokitaka watu wa Venezuela kipatikane,” huku akisisitiza kwamba hakuna haja ya maandamano.
Jumuiya ya kimataifa yapata wasiwasi matokeo ya uchaguzi
Kumekuwa na mutikio mseto kutoka jumuiya ya kimataifa kuhusu matokeo hayo yaliomtangazia ushindi Rais Maduro, kwa upande wake Rais wa Costa Rica Rodrigo Chaves aliyaita matokeo hayo rasmi kuwa ni ya “udanganyifu.” Nayo Peru ilitangaza kuwa imemwita balozi wake kwa mashauriano kuhusu matokeo.
Soma pia:Venezuela yakataa kuwaalika waangalizi wa EU katika uchaguzi wake wa rais
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alionyesha “wasiwasi mkubwa” kwamba matokeo hayaakisi matakwa ya Wavenezuela huku Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell akitoa wito kuhakikisha “uwazi katika mchakato wa uchaguzi.”
Hata hivyo washirika wa karibu wa Venezuela ikiwemo China, Cuba, Nicaragua, Honduras na Bolivia walimpongeza Maduro kwa ushindi huo.