Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo ameongoza washiriki zaidi ya 12,000 wa mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma huku akiwapongeza waandaaji wa mbio hizo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kufanikiwa kukusanya fedha kiasi cha sh milioni 300 zitakazoelekezwa katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.
Katika mbio hizo zilizohusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, ilishuhudiwa washiriki kutoka Tanzania, Kenya na Uganda wakichuana vikali kwa kuibuka washindi kwenye mbio tofauti hususani zile za km 10, km 21 na km 42. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa na viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali walioshiriki kwenye mbio za KM 5.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi na wadau mbalimbali wa mbio hizo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa mafanikio hayo, alionyesha kuguswa na ongezeko kubwa la washiriki wa mbio hizo kutoka washiriki 1,500 mwaka 2020 hadi kufikia washiriki 8,000 waliojiandikisha rasmi kushiriki mbio hizo mwaka huu.Hatua hiyo alisema inasadifu mwamko mkubwa wa wananchi kushiriki katika michezo hatua ambayo itasaidia katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo, kisukari na figo.
“Mchango wa Benki ya NBC katika kuinua sekta ya michezo nchini upo wazi sana ambapo wametenga fedha zaidi ya bilioni 36 katika kufanikisha udhamini wa michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu. Kupitia mchezo huu wa riadha mbali na kuchochea mwamko wa mchezo husika kwa jamii, kwa mwaka huu pekee wamefanikiwa kukusanya fedha kiasi cha sh milioni 300 zitakazoelekezwa kufanikisha juhudi mbalimbali za kiafya kupitia agenda ya msingi ya kuokoa maisha ya mama na mtoto…hongereni sana NBC,’’ alipongeza.
Alisema hatua ya benki hiyo, inaunga mkono jitihada za serikali kupitia azma ya Rais Samia Suluhu ya kuimarisha sekta ya afya nchini. Aliitoa wito kwa taasisi mbalimbali binafsi na zile za umma kuhakikisha wanabuni matukio mbalimbali ya kimichezo ili wayatumie kujenga afya za wananchi sambamba na kufanikisha agenda mbalimbali za kijamii.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw Hamis Mwinjuma pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kuwa mdau mkubwa wa sekta ya michezo hapa nchini kupitia jitihada zake mbalimbali, alisema ukubwa wa mashindano hayo ya NBC Dodoma Marathon unatoa fursa kwa mamlaka zinazosimamia mchezo huo kutumia washindi mbalimbali waliopatikana kwenye mbio hizo kuliwakilisha taifa kwenye mashindani mbalimbali ya kimataifa yakiwemo mashindano ya Olympics na yale ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi alisema kiasi cha mil 300 kilichokusanywa kupitia mbio kitaelekezwa katika kufanikisha malengo ya mbio hizo ambayo ni ukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pamoja na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga kupitia Taasisi ya Benjamin Mkapa lengo kuu likiwa ni kuboresha afya ya mama wa mtoto.
“Zaidi pia sehemu ya fedha hii itaelekezwa katika kufanikisha ujenzi wa chumba cha upasuaji wagonjwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mafanikio haya yanachochewa na dhamira yetu kama benki ya kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii tunayoihudumia. Pia nawapongeza sana wadau mbalimbali waliojitokeza kufanikisha mbio hizo wakiwemo Kampuni ya Bima ya Sanlam ambao ni wadhamini wakuu wa mbio hizo sambamba na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom waliodhamini mbio za km 21 pamoja na wadhamini wengine wote waliotuunga mkono,’’ alisema.
Katika mbio hizo ilishuhudiwa Mwanariadha kutoka Uganda Akanswa Mingichi akiibuka mshindi wa kwanza mbio za km 42 (Full Marathion) kwa upande wa wanaume baada ya kutumia muda wa saa 2 na dakika 13 akifuatiwa na Mwanariadha Eyenali Paul kutoka Kenya alietumia muda wa saa 2 na dakika 14 huku kwa upande wa wanawake mbio hizo ilishuhudiwa Mwanaridha Angelina Yumba akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 2 na dakika 33 akifuatiwa na Chopsiriri Tufena kutoka Kenya alietumia muda wasaa 2 na dakika 34.
Washindi wa kwanza kwenye mbio hizo za km 42 waliondoka na zawadi ya fedha taslimu Tsh milioni 11.5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote huku washindi wa pili wakiondoka na Tsh Milioni 5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote mbili.
Kwa upande wa mbio za km 21 wanaume ilishuhudiwa Mwanariadha kutoka Kenya Peter Mwangi akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 1:2:23 akifuatiwa na Mwanariadha Joseph Panga kutoka Tanzania alietumia muda wa saa 1:02:35 huku kwa upande wa wanawake mbio hizo ilishuhudiwa Mwanaridha Sarah Makera akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 2 na dakika 10 akifuatiwa na Suzana Chembui kutoka Kenya alietumia muda wa saa 1 na dakika 11.
Washindi wa kwanza kwenye mbio hizo za km 21 waliondoka na zawadi ya fedha taslimu Tsh milioni 5.5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote huku washindi wa pili wakiondoka na Tsh 2.5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote mbili.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Tsh milioni 100 Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage iliyotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya kuchangia mapambano ya Saratani ya shingo ya kizazi kwa kina mama kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika leo kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw Hamis Mwinjuma (wa tatu kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa pili kulia) na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (Kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani
ya Tsh milioni 50 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili Prof. Mohamed Janabi iliyotolewa
na Benki ya NBC kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa chumba cha upasuaji
kwenye hospitali hiyo kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika
leo kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw Hamis Mwinjuma (wa tatu
kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa pili
kulia) na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (Kushoto) akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani
ya Tsh milioni 100 Mwakilishi wa Taasisi ya Benjamin Foundation
iliyotolewa na Benki ya NBC kwa ajili ya kuchangia kutoa ufadhili wa
elimu kwa wakunga kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika leo
kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni pamoja na Naibu
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw Hamis Mwinjuma (wa tatu
kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (wa pili
kulia) na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (wa tatu kulia) akimkabidhi mfano wa hundi yenye
thamani ya Tsh milioni 11.5 kwa mwanariadha Angelina Yumba kutoka
Tanzania baada ya kuibuka mshindi wa kwanza mbio za km 42 NBC Dodoma
Marathon zilizofanyika leo jijini Dodoma zikilenga kuchangia mapambano
ya Saratani ya shingo ya kizazi kwa kina mama.Wanaoshuhudia ni pamoja na
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw Hamis Mwinjuma (wa pili
kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (kushoto)
na viongozi wengine kutoka serikalini na wadau wa mbio hizo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (katikati) akionyesha medali aliyokabidhiwa na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Bw Theobald Sabi (Kushoto) ili
amfikishie Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni ishara ya benki hiyo
kutambua mchango wa Rais Samia katika kuasisi mbio hizo wakati wa msimu
wake wa kwanza uliofanyika mwaka 2020 ambapo Rais Samia aliziongoza
akiwa kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wanaoshuhudia ni pamoja na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Bw Hamis Mwinjuma (kulia), na viongozi wengine kutoka serikalini na
wadau wa mbio hizo.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akiwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo wa
kitaifa na viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali walioshiriki
kwenye mbio za KM 5 za NBC Dodoma Marathon leo
Katika
mbio hizo zilizohusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi,
ilishuhudiwa washiriki kutoka Tanzania, Kenya na Uganda wakichuana
vikali kwa kuibuka washindi kwenye mbio tofauti hususani zile za km 10,
km 21 na km 42.