Unguja. Chama cha ACT- Wazalendo kimeeleza mambo ambayo yakifanyika, yanaweza kuharakisha maendeleo na ukombozi visiwani Zanzibar.
Mambo hayo ni kuendesha nchi hiyo katika misingi ya kistaarabu, kupata mamlaka kamili na kuwa na Serikali iliyotimiza masharti na matakwa ya wananchi
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud leo Jumanne, Julai 30, 2024 alipokuwa akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mpika Tango Mkoani, Mkoa wa Kusini Unguja katika mwendelezo wa mikutano ya hadhara ya chama hicho kisiwani humo.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesema:
“Tunachosema kazi yetu na kazi yenu kama hatujapigania mambo mawili makubwa: Nchi ikawa na mamlaka kamili ikaendeshwa kwa ustaarabu kwa misingi halali, tukawa na Serikali ya kweli, hatuwezi kwenda mahala tutazidi kudhalilika na kudidimia na kuendelea kuwa fukara.”
Amedai kuwa kwa utaratibu uliopo sasa wa wizi na ufisadi wa mali za umma, hautakwisha kwa sababu ya watu huingia kwenye madaraka kwa kumwaga damu.
Amesema njia bora ya kumaliza hayo ni kutengeneza mazingira ili uchaguzi wa mwaka 2025 uwe huru na wa haki.
“Kama umeleta maendeleo, unasema umejenga kila pahala sasa unamuogopa mwananchi kwa nini wakati umemletea maendeleo. Kwa kumuogopa mtu huyo maana yake unasema hukushinda, hakuna nchi itakayokwenda kwa kutumia dhulma, tuingie ulingoni kushindana,” amesema.
Kauli ya Othman imekuja kufuatia kauli za baadhi ya viongozi wa CCM, akiwamo Naibu katibu Mkuu-Zanzibar, Dk Mohamed Dimwa na Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM), Khamis Mbeto, ambao kwa nyakati tofauti walisema kupitia ilani ya chama hicho, nchi sasa imejengwa kila mahali na kwamba kuna maendeleo makubwa.
Mbeto alisema utekelezaji wa miradi hiyo umewafanya wapinzani wao kukosa hoja, huku akisema wanasubiri katika uchaguzi mkuu ujao wananchi ndio wataamua kwa vitendo.
Othman amesema suala la kupigania mamlaka ya Zanzibar lipo ndani ya Katiba na ni wajibu wa kila Mzanzibar kufanya hivyo, japo kuna watu wanapuuza kwa ajili ya masilahi binafsi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho upande wa Zanzibar, Ismail Jussa amesema chama cha siasa sio hoja, muhimu ni safari ya ukombozi wa Zanzibar ambayo kwa sasa haina mbadala bali viongozi wa ACT ndio wenye maono hayo.
Amesema mamlaka za Serikali za mitaa zinapaswa kuwashirikisha wananchi wakati wanapotekeleza miradi, badala yake hawashirikishwi na miradi mingine haileti tija kwao.
Ametolea mfano mradi wa masoko ambayo yamejengwa likiwemo la Kipitacho, lakini wananchi wameshindwa kulitumia kwa sababu ya ukosefu wa huduma na kuwa mbali na makazi ya watu.