NAMBA hazijawahi kudanganya. Na waliobuni msemo huo wala hawakukosea. Hii ni baada ya Barbara Gonzalez aliyewahi kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, kuchomoa kibabe mbele ya watendaji wengine wa klabu hiyo na watani wao Yanga katika kipindi cha kushikilia nafasi hiyo Msimbazi.
Ndio. Simba juzi kati imemtambulisha Mtendaji Mkuu (CEO) mpya, Uwayezu Francois Regis kuchukua nafasi ya Imani Kajula anayemaliza muda wake klabuni hapo.
Kama hujui ni kwamba, Simba na Yanga tangu ziingie katika mchakato wa mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji, zilianza kuwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) waliochukua nafasi zilizokuwa zikifanywa na Katibu Mkuu wa kuchaguliwa. Nafasi hii kwa sasa ni ya kuajiriwa kama ilivyo kwa Mhasibu au Ofisa Habari.
Simba ilikuwa ya kwanza kufanya hivyo, mwaka 2018 ambapo katika Mkutano Mkuu wa Klabu uliofanyika mwezi Novemba, ikamteua Crescentius Magori ambaye alikuwa CEO wa kwanza. Safari yao ikaanzia hapo na hadi sasa wamekuwa nao watano.
Hivi karibuni, uongozi wa Simba umemtangaza Uwayezu Francois Regis, raia wa Rwanda kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, akichukua nafasi ya Imani Kajula anayejiandaa kumaliza mkataba wake mwishoni mwa mwezi huu.
Francois, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa APR ya Rwanda na amewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Rwanda (FERWAFA).
Hii ni mara ya pili kwa Simba kuwa na CEO kutoka nje ya nchi, kwani awali iliwahi kumuajiri, Senzo Mbatha Mazingisa kutoka Afrika Kusini ambaye baadaye alijiondoa na kutua Yanga kabla ya kurithiwa na Mzambia, Andre Mtine aliyewahi kuhudumu ndani ya TP Mazembe ya DR Congo.
Ujio wa CEO mpya wa Simba kutoka Rwanda, unamfanya bosi huyo kuwa katika mitihani kadhaa ndani ya klabu hiyo kupitia cheo chake hicho.
Kati ya mambo anayopaswa kuyasimamia ili apimwe kufanikiwa au kufeli kwake ni kusimamia maendeleo ya soka la vijana, wanawake na wakubwa. Kutekeleza mikakati ya muda mrefu kwa ajili ya mafanikio ya timu kuanzia michuano ya ndani hadi kimataifa. Katika mafanikio hayo ni kubeba makombe lakini pia timu kufikia malengo ya kucheza nusu fainali michuano ya kimataifa baada ya kuwa na wimbo huo kwa muda mrefu lakini timu inaishia robo fainali.
Wakati Mnyarwanda huyo anatua Simba, kuna watangulizi wake ndani ya klabu hiyo ambao Mwanaspoti linakupitisha kwa kila mmoja muda aliokaa katika cheo hicho na mafanikio yake.
Mbali na Simba, pia upande wa Yanga ambao nao walianza mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu mwaka 2021, mpaka sasa imeongozwa na CEO wawili ambao wote ni raia wa kigeni.
Novemba 4, 2018, Magori alichaguliwa kuwa CEO wa Simba katika mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika Dar es Salaam. Magori alikuwa CEO wa kwanza Simba baada ya klabu hiyo kuingia katika mfumo mpya wa uendeshaji kutoka mikononi mwa wanachama hadi uuzaji wa hisa.
Kiongozi huyo alikaa katika kiti hicho kwa takribani miezi sita hadi mwisho wa msimu 2018-2019. Akaondoka.
Katika kipindi chake cha kuwa CEO ndani ya Simba, alishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara moja msimu wa 2018-2019, kisha kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kupoteza kwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya TP Mazembe.
Ndiye alikuwa mrithi wa Magori ndani ya Simba baada ya Septemba 7, 2019 kutambulishwa kuwa CEO klabuni hapo. Akahudumu hadi Agosti 9, 2020 alipoamua kujiuzulu nafasi yake hiyo, kisha akatambulishwa Yanga.
Ndani ya msimu mmoja aliokaa Simba, Senzo alishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2019-2020, Kombe la FA 2019-2020. Kimataifa Simba haikutoboa kwani iliishia hatua ya awali katika Ligi ya Mabingwa Afrika 2019-2020.
Septemba 2, 2020, Simba ilimteua Barbara kuwa CEO wa klabu hiyo na kuweka rekodi ya kuwa Mtendaji Mkuu wa kwanza mwanamke katika soka la Tanzania.
Mwanamama huyu ambaye alichukua nafasi ya Senzo, alikaa ndani ya Simba hadi Desemba 10, 2022 alipotangaza kujiuzulu.
Mpaka sasa unaweza kusema yeye ndiye CEO aliyefanikiwa zaidi ndani ya Simba huku pia akiwa amedumu katika nafasi hiyo kwa muda mrefu kuliko wengine.
Msimu wa kwanza akiwa CEO ndani ya Simba 2020-2021, timu hiyo ilishinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ikacheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo katika msimu huo, iliongoza Kundi A mbele ya vigogo wa soka Afrika, Al Ahly baada ya kukusanya pointi 13. Al Ahly walimaliza wa pili na pointi 11. Wengine waliokuwa katika kundi hilo ni AS Vita (7) na Al Merrikh (2).
Simba iliifunga AS Vita nyumbani na ugenini kwa jumla ya mabao 5-1, ikaichapa Al Ahly nyumbani 1-0 ugenini ikafungwa idadi kama hiyo, kisha ikapata ushindi wa 3-0 dhidi ya Al Merrikh nyumbani na ugenini ilikuwa 0-0.
Robo fainali ikakutana na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Simba haikuwa kinyonge kwani licha ya ugenini kuruhusu mabao 4-0, nyumbani ilicharuka na kushinda 3-0, lakini hazikutosha na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-3.
Ukiachana na hilo, Simba ikashinda Kombe la FA kwa kuifunga Yanga bao 1-0.
Msimu wa 2021-2022 Barbara aliuanza vibaya kwa kupoteza taji la Ngao ya Jamii ambalo Simba ilikuwa bingwa mtetezi, Yanga ilishinda 1-0 kwa kuichapa Simba. Hakumaliza msimu, akaondoka Desemba 2022.
Kutoka Januari 26, 2023 alipotambulishwa kuwa CEO wa Simba hadi Agosti Mosi, 2024 anapoondoka, Kajula ameiongoza Simba katika wakati mgumu sana lakini hajatoka patupu.
Ni kipindi ambacho timu hiyo imepitia misukosuko ya hapa na pale kuanzia ndani ya uwanja hadi nje, mwisho wa yote anaondoka akiwa ameshinda Ngao ya Jamii 2023 na Kombe la Muungano 2024.
Pia Simba imecheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2023-2024, Kumbuka hatua ya makundi iliishangaza Wydad Casablanca baada ya kuifunga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa upande wa Yanga, nafasi hiyo ya Mtendaji Mkuu ilianza kutumika tangu enzi za ufadhili Yusuf Manji alipokuwa Mwenyekiti, ambapo mwaka 2016 alimuajiri Jerome Dufourg, raia wa Ufaransa kushika nafasi hiyo kwa mkataba wa miaka mitatu kabla ya kumfuta kazi mwaka mmoja baadaye kwa kushindwa kazi.
Kisha wakapita viongozi kadhaa wa kushika nafasi hiyo akiwamo Mwanasheria Patrick Simon, lakini kwa ajira kipindi hiki Yanga ikitaka kuingia katika mfumo wa kisasa wa kuendeshwa kama kampuni, imeajiri watu wawili tu katika nafasi hiyo ambao wote wana rekodi zao, lakini hawafikii mafanikio ya Barbara.
Alipoondoka Simba Agosti 9, 2020, muda mfupi baadaye akatambulishwa ndani ya Yanga. Mwanzoni hakuwa CEO bali alipewa jukumu la kusimamia mabadiliko ya utawala ndani ya klabu hiyo akiwa mshauri.
Baada ya kudumu kwa mwaka mmoja, Agosti 31, 2021 Uongozi wa Yanga ukamtangaza Senzo kuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) kufuatia utekelezwaji wa mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu.
Katika majukumu ya CEO katika msimu wa 2021-2022, Senzo akawa kwenye mafanikio ya klabu hiyo kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Ngao ya Jamii akiifunga Simba 1-0. Aliondoka klabuni hapo Julai 31, 2022. Kimataifa msimu huo Yanga iliishia hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Rekodi zinaonyesha Senzo hana upepo na michuano ya kimataifa tangu awe CEO wa Simba na Yanga kwani mara zote timu hizo zimeishia hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Alitambulishwa kuwa CEO wa Yanga Septemba 27, 2022 akichukua nafasi ya Senzo. Katika kipindi cha misimu miwili kimekuwa na mafanikio makubwa sana kwake.
Mtine raia wa Zambia, msimu wa kwanza 2022-2023, ameshinda Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, huku timu ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kufanya hivyo.
Msimu wa pili 2023-204, moto umeendelea kuwa uleule kwani Mtine ndani ya Yanga ameshinda Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita takribani miaka 25. Rekodi mpya ameiweka.