Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepongeza jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) katika kuendeleza sekta ya afya hapa nchini kupitia huduma za kibenki pamoja program zake mbalimbali zinazolenga kuboresha sekta hiyo muhimu.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa pongezi hizo mapema leo alipotembelea banda la maonyesho ya huduma za benki hiyo mahususi kwa wadau wa sekta ya afya lililopo kwenye kongamano la Afya Kitaifa lililoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) katika ukumbi wa JNICC dar es salaam.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusino ya Umma wa benki ya NBC Bw Godwin Semunyu kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo kwenye sekta afya, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali inathamini mchango mkubwa unaofanywa na benki hiyo pamoja na wadau wengine katika kusaidia sekta hiyo muhimu.
“Ni juzi tu nimetoka kuongoza mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika huko Dodoma ambapo jumla ya milioni 300 zilikusanywa na benki ya NBC kwa ajili ya kusaidia jitihada mbalimbali za kiafya hususani kuokoa Maisha ya mama na mtoto. Huko Zanzibar pia wamekuwa wakifadhili huduma za uchunguzi wa bure kwa wanawake wajawazito kupitia huduma ya kliniki inayotembea pamoja na jitihada nyingine nyingi…hongereni sana NBC,’’ alipongeza.
Akiwa kwenye banda hilo pia Waziri wa Afya , Ummy Mwalimu aliipongeza benki hiyo kwa jitihada hizo kwenye sekta ya afya huku akiahidi kuendelea kushirikiana na benki hiyo katika kutekeleza miradi mbalimbali kwenye sekta ya afya hususani ile inayolenga afya ya mama na mtoto.
Awali akizungumzia jitihada mbalimbali za benki hiyo kwenye sekta ya Afya, Bw Semunyu alisema ikiwa kama mdau muhimu kwenye sekta hiyo, benki ya NBC mbali na kutoa huduma za kibenki kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo ikiwemo mikopo ya ujenzi wa majengo na miundombinu mbalimbali ya afya na ununuzi wa vifaa vya afya pia imekuwa ikifadhiri na kuendesha program mbalimbali za kiafya hapa nchini.
“Mbali na NBC Dodoma Marathon ambayo tumetoka kukusanya milioni 300 kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kina mama sambamba kufadhili masomo ya wakunga 100 kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa pamoja na ujenzi wa chumba cha upasuaji Hispitali ya Taifa Muhimbili pia tumekuwa tukishirikiana na makampuni ya bima katika utoaji wa bima ya afya.’’ Alitaja.
Zaidi Semunyu alitaja jitihada nyingine za benki hiyo kwenye sekta ya afya kuwa ni pamoja na ufadhili wa mali za biashara ambapo benki hiyo inatoa mikopo bila dhamana kwa watoa huduma za afya pamoja na kutoa misaada ya vifaa vya matibabu kwa hospitali katika mikoa mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa tatu kulia) akimsikiliza akipokea taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusino ya Umma wa benki ya NBC Bw Godwin Semunyu (wa pili (kushoto) kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo kwenye sekta afya wakati alipotembelea banda la maonyesho ya huduma za benki hiyo mahususi kwa wadau wa sekta ya afya lililopo kwenye kongamano la Afya Kitaifa lililoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) katika ukumbi wa JNICC dar es salaam leo. Wengine ni pamoja na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu (Kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamini William Mkapa Foundation Dkt Ellen Senkoro (Katikati).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa (wa nne kulia) akimsikiliza Waziri wa Afya, Ummy
Mwalimu akizungumza kuhusu mchango wa benki ya NBC kwenye sekta ya afya
alipotembelea banda la maonyesho ya huduma za benki hiyo mahususi kwa
wadau wa sekta ya afya lililopo kwenye kongamano la Afya Kitaifa
lililoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) katika ukumbi wa
JNICC dar es salaam leo. Wengine ni pamoja na Waziri wa Afya Afya
Zanzibar Nassor Ahmed Mazurui (Kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya
Benjamini William Mkapa Foundation Dkt Ellen Senkoro (Katikati) na Mkuu
wa Idara ya Mawasiliano na Mahusino ya Umma wa benki ya NBC Bw Godwin
Semunyu (alieshika kipaza sauti)
Maofisa
wa Benki ya NBC wakiwahudumia wadau mbalimbali wa sekta ya afya
waliotembelea banda la benki hiyo lililopo kwenye kongamano la Afya
Kitaifa lililoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) katika ukumbi
wa JNICC dar es salaam leo