Bima ya Afya ya Jubilee yaanzisha huduma kwa vikundi vidogo

Dar es Salaam. Kampuni ya Bima ya Afya ya Jubilee, imeanzisha huduma ya afya kwa wafanyabiashara na vikundi vidogo vidogo.

Huduma hiyo ijulikanayo kama FBiZ imezinduliwa leo Jumanne Julai 30, 2024 jijini Dar es Salaam ikitoa fursa kwa watu kuanzia watatu kujisajili kupata huduma ya afya.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Uendeshaji wa Bima ya Afya ya Jubilee, Shaban Salehe amesema FBiZ inampa fursa mteja kuchagua huduma na kiwango cha gharama anachotaka.

“FBiZ ina uchaguzi tofauti ipo ya kuanzia gharama ndogo ya Sh10 milioni hadi kubwa ya Sh100 milioni.

“Tumeileta kutokana na mahitaji yake kuwa ni mengi huku pia vikundi vidogo vidogo na wafanyabiashara ndogo ndogo nao wasijione kama wameachwa katika huduma za bima zilizopo sokoni,” amesema.

Kuhusu ufanyaji kazi wa huduma hiyo, Gwakisa Mwankesa aliyemwakilisha mkuu wa kitengo cha biashara amesema huduma hiyo itawahusisha wana kikundi kuanzia watatu hadi 15.

“Tumekuja na hii bidhaa ili kuzipa fursa kampuni nyingine ndogo ndogo ambazo zinawafanyakazi watatu, wanne na kuendelea ambao hawa awali tuliwaweka kwenye bidhaa ya mtu mmoja mmoja,” amesema.

“Pia, vikundi na wafanyabiashara ndogo ndogo kuwa kwenye huduma za bima,” amesema.

Amesema FBiZ itatoa huduma kulingana na mahitaji ya mteja na itakuwa ikifanya kazi katika nchi ya Tanzania pekee, na si Afrika Mashariki na India kama ilivyo kwa huduma yao ya J Biz inayopatikana Afrika Mashariki na India.

“Bidhaa ya FBiZ ni bidhaa inayoendana na mahitaji ya soko letu la bima, uhitaji ulikuwa mkubwa na mapokeo yamekuwa chanya,” amesema.

Meneja mawakala wadogo, Valentino Mkenda amesema hiyo ni moja ya bidhaa za Bima ya Afya ya Jubilee inayokwenda kuleta suluhisho hususani kwenye huduma za afya.

“Tupo kuhakikisha Watazania wanapata huduma bora za afya kupitia Bima ya afya ya Jubilee,” amesema.

Related Posts