China yanadi fursa za uhandisi kwa wanafunzi Baobab

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Kampuni ya Ujenzi na Mawasiliano ya China (CCCC) imewahamasisha wanafunzi wa Shule ya Sekondari Babobab iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani kusoma masomo ya sayansi na kujiendeleza katika fani ya uhandisi ambayo ina fursa nyingi kwenye sekta ya ujenzi.

Akizungumza Julai 26,2024 baada ya kutembelea shule hiyo, Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya CCCC hapa nchini, Liyuliang, amesema wamevutiwa kuwafundisha wanafunzi hao na kuwapa vitabu ili wapende fani ya uhandisi kwa kuwa wataalam hao wanahitajika kwa wingi ndani na nje ya nchi.

Aidha amewataka wanafunzi kuchagua kozi zitakazowasaidia kupata maarifa na ujuzi kama za uhandisi ambazo wanaweza kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.

Mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika shule hiyo, Amar Bayumi, amesema elimu waliyoipata imewapa mwanga wa kuzidi kuipenda taaluma ya ujenzi.

“Tumejifunza njia nyingi za kutengeneza madaraja ambayo yatapita juu ya bahari au juu ya ardhi ambayo imepata dhoruba ya kimazingira, pia tumejifunza mashine ambazo tutazitumia wakati wa ujenzi wa barabara, madaraja na vitu vingine…nina ndoto ya kuwa injinia na nitakwenda kusoma,” amesema Bayumi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Baobab, Mwalimu Venance Hongoa, amesema wanawahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi na wengi wamekuwa na ufaulu mzuri katika masomo hayo.

“Tunaipongeza Kampuni ya CCCC kwa uwekezaji wao na namna inavyotenga muda kuwafikia wanafunzi ambao ni walaji watarajiwa, wamewahamasisha wanafunzi wetu kusoma masomo ya sayansi na faida wanazoweza kuzipata. Tumefurahi watoto wetu walivyouliza maswali na wamewatia moyo katika usomaji wao,” amesema Mwalimu Hongoa.

Ofisa Elimu Taaluma kutoka Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Juma Yusuph, amesema mafunzo hayo yataongeza chachu kwa wanafunzi hao kupenda fani ya uhandisi.

“Ni jambo jema kuhamasisha watoto wetu waweze kuingia katika tasnia ya uhandisi ujenzi na mawasiliano kwa sababu tunahitaji wataalam wengi, maendeleo mengi yanakuja kutokana na ufanisi katika masuala ya sayansi hivyo, itasaidia vijana kuhamasika na kuzidi kufanya vizuri katika masomo ya sayansi,” amesema Yusuph.

Related Posts