DC Arumeru awaangukia watafiti kuhusu madini ya flouride kwenye maji

Arusha.Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda, amewataka watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti ya Nelson Mandela inayoshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia Afrika, kufanya utafiti wa upatikanaji wa uchujaji wa maji ili kupunguza madini ya flouride yenye madhara kwa watumiaji.

Amesema miongoni mwa madhara wanayopata wananchi kutokana na matumizi ya maji hayo yanayodaiwa kuwa na flouride kwa wingi ni kupinda viungo hasa miguu, mikono na migongo.

Pia, amesema wajawazito hujifungua watoto wenye vichwa vikubwa na kwa watu wazima meno yao hudhoofika.

Kaganda amesema hayo leo Jumanne Julai 30, 2024, kwenye mkutano wa wanafunzi wa utafiti wa mifumo ya maji taka na kilimo, uliofanyika katika Chuo cha Nelson Mandela kilichopo Arumeru, Mkoa wa Arusha na mkutano huo umehudhuriwa na watafiti kutoka Tanzania na Ubelgiji.

Amesema wananchi wa Arumeru hasa wa kata za Oldonyosambu na Oldonyowasi, ni waathirika wakubwa wa maji hayo wanayotumia kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha flouride.

Hivyo, ametoa wito kwa watafiti kutoka Tanzania na Ubelgiji kuwekeza nguvu kwenye utafiti huo ili kuokoa kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema tafiti nyingi zimefanyika kuhusu tatizo hilo, lakini bado familia nyingi zina uwezo wa kuchuja maji kwa kiwango kidogo.

Lakini pia amesema tatizo bado kubwa kwenye maeneo ya umma kama shule, hospitali na sehemu za mkusanyiko mkubwa wa watu ikiwamo sokoni.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Nelson Mandela, Profesa Anthony Mshandete anayeshughulikia taaluma, utafiti na ubunifu, amesema wamekubali ombi la mkuu huyo wa wilaya na watalijadili kama wanataaluma.

“Leo amekuja kufunga mkutaba wetu wa ushirikiano kati ya Chuo cha Sayansi na Teknolojia Afrika cha Nelson Mandela na wataalamu wa utafiti kutoka vyuo vikuu vya Ubelgiji,” amesema Profesa Mshandete.

Amesema kwa kuwa mkuu huyo wa wilaya  ameibua suala jipya la madini hayo ya fluoride, watalazimika sasa kukaa na kutafakari kipi kifanyike ili kufanikisha utafiti huo.

“Tukikubaliana tutatembelea maeneo yenye madhara na kukusanya sampuli mbalimbali,” amesema.

Related Posts