Mwandishi Wetu, Dodoma.
DIWANI wa Kata ya Tambuka Reli jijini Dodoma Juma Mazengo amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kikamilifu hivyo kuyagusa makundi yote.
Mazengo aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika kata ya Tambuka Reli.
Alisema kutokana na kazi nzuri anazofanya Rais Dk.Samia makundi yote yanamkubali.
“Rais Dk.Samia anafanya kazi nzuri ya utekelezaki wa Ilani ya CCM ikiwemo ujenzi wa shule, zahanati na barabara na makundi yote yanamkubali,”alisema.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa ilani katika kata hiyo alisema serikali imetoa sh.milioni 70 kwaajili ya ujenzi wa soko lenye visimba 43.
Alisema kukamilika kwa soko hilo kutasaidia wafanyabiashara kufanya shughuli zao pasipo usumbufu wowote.
“Serikali imetoa sh.milioni 50 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa zahanati ya kata ambapo ujenzi wake umefikia hatua ya lenta,”alisema.
Akizungumzia utekelezaji wa ilani katika sekta ya elimu alisema katika mwaka wa fedha uliopita wamefanikiwa kufanya ukarabati wa madarasa chakavu matatu katika shule ya msingi Dodoma Mlimani.