Elimu ya amali, mwanga mpya wa elimu Tanzania

Katika ulimwengu wa sasa, ambapo mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya soko la ajira yanabadilika kwa kasi, uwekezaji katika elimu ya ujuzi unakuwa na umuhimu mkubwa kuliko elimu ya nadharia.

Tanzania imeamua kubadilisha mtalaa wake ili kuendana na mahitaji haya, jambo ambalo lilipongezwa na wadau mbalimbali akiwamo Mbunge wa Kahama, Jumanne Kishimba, aliyejipambanua kama mtetezi wa mabadiliko kwenye mfumo wa elimu nchini.

Kwa mujibu wa Kishimba, mabadiliko haya yanahakikisha vijana wanapata ujuzi wa vitendo unaohitajika kwenye soko la ajira, na hivyo kuwawezesha kujitegemea na kuchangia zaidi katika maendeleo ya Taifa.

Hatua hii aliiona muhimu kwa kuwa inamarisha mifumo ya elimu kwa kuzingatia mafunzo ya vitendo na ujuzi wa kisasa, badala ya kuendelea kushikilia nadharia ambazo haziendani na hali halisi ya soko la ajira.

Hivi sasa katika kuhakikisha elimu ujuzi inachukua nafasi, Serikali imeanzisha mtalaa wa elimu ya amali, hasa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka mageuzi kwenye mfumo wa elimu.

Rais Samia ndiye aliyeanza kuchokoza mjadala wa kitaifa kwa kuagiza kufanyike mapinduzi ya mfumo wa elimu nchini na hatimaye watendaji wake kuingia kazini na kufanya maboresho ya mtalaa wa elimu ya msingi na sekondari.

Kutoka hapo maneno elimu ya amali yakashika chati. Ni sawa na kusema ndio gumzo kwa sasa katika duru za kielimu na hata kwenye vilinge vya wadau wa elimu.

Elimu ya amali inalenga kuimarisha uwezo wa wanafunzi katika stadi za kivitendo, ili kuwapa maarifa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kisasa.

Hata hivyo, dosari inakuja pale wazazi na walezi wanapodhani watoto wao kusomea elimu ya amali ni sawa na kuwafanya wawe mafundi ambao hawatafaidi matunda ya elimu yao.

Waziri wa Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alitoa ufafanuzi kuhusu elimu ya amali Oktoba 10, 2023.

Alisema kuwa lengo la elimu hiyo ni kuwapatia wanafunzi ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuajiriwa.

“Kwenye elimu hii ya amali tutakuwa na michezo, kilimo, pamoja na ufundi ambapo mtoto atakapomaliza kusoma atapata cheti chake alichosomea,” alieleza Profesa Mkenda, akiwataka watu wenye uwezo wa kutoa elimu hiyo kuwasiliana na Serikali ili kuboresha mazingira ya kufundishia.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo aliwahi kusema:

“Napenda kuona wanafunzi tunaowapatia ujuzi wanakuwa na ubora wa kimataifa ambapo wataweza kufanya kazi mahali popote pale duniani,”

Kwa upande wa Zanzibar, Serikali ilianza mchakato wa kujenga vituo vya mafunzo ya amali Unguja na Pemba, ili kuwasaidia wanafunzi wanaokosa sifa za kujiunga na elimu ya juu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, anabainisha kuwa Serikali inaendelea na hatua za kupata vifaa vya kujifunzia na kufundishia na kuzindua mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya lazima.

Paskal Malimi, fundi maarufu wa kompyuta Kariakoo, ni mfano wa jinsi elimu ya amali inavyoweza kutoa ujuzi wa vitendo.

“Sikuwahi kumaliza shahada ya ufundi wa kompyuta, bali nilijifunza kutoka kwa kaka yangu ambaye alifungua chuo cha kompyuta mtaa wa Kamata hapa Kariakoo mwaka 1998,” anasema Malimi, akionyesha umuhimu wa kuunganisha elimu rasmi na mafunzo ya vitendo.

Hata hivyo, suala hili limeibua mkanganyiko. Watu wengi wamekuwa wakijiuliza iwapo elimu ya amali ni tofauti na elimu ya ufundi, ambayo imekuwa ikitolewa kwa muda mrefu kupitia vyuo vya Veta.

Kwa mfano, mtalaa wa elimu ya amali unajumuisha fani kama umeme, uhandisi mitambo, uhandisi ujenzi, uhandisi magari, ukarimu na utalii, biashara, sanaa za ubunifu, Tehama na michezo.

Fani hizi zinafanana na zile zinazotolewa katika vyuo vya ufundi, na hivyo kuzua maswali kuhusu uhalisia wa tofauti kati ya programu hizi mbili.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilianza mchakato wa kujenga vituo vya mafunzo ya amali Unguja na Pemba, ili kuwasaidia wanafunzi wanaokosa sifa za kujiunga na elimu ya juu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alibainisha kuwa Serikali inaendelea na hatua za kupata vifaa vya kujifunzia na kufundishia, na kuzindua mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya lazima.

Wakati Serikali ikihamasisha uwekezaji katika elimu ya amali, changamoto kubwa ni mtazamo hasi wa wazazi wengi ambao wanaona elimu hiyo itawaandaa watoto wao kuwa mafundi badala ya wataalamu wa ofisini.

Hata hivyo, mtazamo huo unapingwa na Martin Lutahakana, Mtanzania anayeishi Uingereza, anayeeleza:

 “Katika nchi zilizoendelea, waliosomea stadi za elimu ya amali wako mbali kiuchumi, maana huhitajika kwa wingi kufanya kazi za watu wa kipato cha kati na cha juu.’’

Soko la ajira kwa wahitimu wa elimu ya amali katika nchi zilizoendelea ni kubwa, na wahitimu hao wanahitajika sana kwenye kazi za vitendo.

Kinachoweza kuikwaza elimu hii kwa hapa nchini, ni uchache katika uwekezaji wa vifaa na rasilimali kwa ajili ya elimu hiyo.

Hata awali katika vyuo vya Veta, vijana wanakosa ujuzi wa kutosha, na mara nyingi wanapata mafunzo ya vitendo kutoka kwa mafundi ambao hawakusoma katika mifumo rasmi.

Akizungumzia uwekezaji, Fredy Mwambafula, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika uhandisi wa umeme katika Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza, anasema uwekezaji mkubwa unapaswa kufanyika ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na ujuzi wa kimataifa.

“Katika vyuo vya Ulaya, mitihani mingi ni ya vitendo, ambayo inawafanya wahitimu kuwa na uwezo mkubwa wa kushindana katika soko la ajira la kimataifa,”anasema.

Mwambafula anabainisha kuwa mara zote amekuwa akiona wanafunzi kutoka nchi za Asia na Ulaya wakihangaika kufaulu masomo ya nadharia lakini kwenye vitendo wako mbali na wanafanya maajabu, huku uwekezaji mkubwa ukiwa umejikita katika tafiti pasipo kuangalia ukubwa wa gharama anayoitumia mwanafunzi.

Naye Siima Katanga, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Guangzhou nchini China, anasema:

“Uwekezaji wa China katika elimu ya amali unalenga kuhakikisha kuwa wahitimu wanakuwa na ujuzi wa kiufundi unaohitajika katika soko la ajira.’’

Anaongeza: ‘’Hali hii imeifanya China kuwa kiongozi katika viwanda na teknolojia, ambapo wahitimu wa vyuo vya amali wanachukua nafasi muhimu katika maendeleo hayo.

Kwa upande wake, Florence Mugarula, ambaye aliishi jijini Birmingham anasisitiza kuwa Ulaya imefanikiwa kuwekeza zaidi kwenye vyuo vya kati, ambapo kusomea shahada ya kwanza na uzamili mara nyingi si kipaumbele.

‘’Badala yake, vijana wanapendelea kusomea kazi na kuonyesha ujuzi mahususi. Hii inaonesha tofauti kubwa na hali ilivyo Tanzania, ambapo elimu ya juu bado inatiliwa mkazo zaidi kuliko elimu ya amali,’’ anaeleza.

 Elimu ya amali inaweza kubadilisha sura ya mfumo wa elimu nchini Tanzania, hasa kama tutachukua mifano kutoka nchi zilizoendelea, ambapo waliosomea stadi za elimu ya amali wanapewa umuhimu mkubwa katika soko la ajira.

Ingawa elimu hii inakumbana na changamoto nyingi kama vile upatikanaji wa vifaa vya kisasa na mtazamo hasi wa wazazi, kuna matumaini makubwa kuwa inaweza kuleta mabadiliko tunayoyataka chini.

Serikali na wadau wanapaswa kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha kuwa elimu ya amali inapata msaada unaohitajika.

Hii inajumuisha kutoa vifaa vya kisasa, kuimarisha mafunzo ya walimu, na kuboresha miundombinu ya kufundishia.

 Aidha, ni muhimu kwa jamii kubadilisha mtazamo wao kuhusu elimu ya amali na kuona thamani yake katika kujenga uchumi imara na kuleta maendeleo ya kijamii.

Katika hatua za kuboresha elimu ya amali, Serikali imeweka mipango ya kujenga vituo vipya vya mafunzo ya amali na kuimarisha programu zilizopo.

Uwekezaji huu ni muhimu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kisasa.

Serikali pia inahamasisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuongeza ubora wa mafunzo yanayotolewa. Kwa kuzingatia mifano kutoka nchi zilizoendelea na juhudi za ndani ya nchi, elimu ya amali inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

Hivyo, ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunajenga msingi imara kwa elimu ya amali, ili kuleta matokeo bora kwa kizazi kijacho.

Aidha, ikiwa elimu ya amali itatekelezwa kwa ufanisi, inaweza kutoa nafasi nyingi za ajira, kupunguza umasikini, na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wengi

Related Posts