Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kushuhudia mageuzi matano katika sekta ya biashara ikiwemo kuongeza ushindani wa mauzo ya bidhaa nje ya nchi, Kuimarisha uwezeshaji na kurahisisha biashara.
Mambo mengine yanayotarajiwa ni kuchochea uongezaji wa thamani ya kila bidhaa inayozalishwa nchini, kuimarisha uwezeshaji, kurahisisha biashara na kuimarisha ushirikiano na majirani.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Julai 29, 2024 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko katika hafla ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Biashara ya mwaka 2023 iliyoboreshwa kutoka Sera ya mwaka 2003 ambayo ilionekana kupitwa na wakati.
Dk Biteko amesema katika uelekeo wa kujenga Tanzania ambayo inachochewa na ukuaji wa viwanda, sera inalenga kuongeza ushindani wa mauzo ya nje ya nchi kutokana na kuweka mkazo kwenye kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa.
“Hili litafanyika kwa kupanua wigo wa bidhaa zinazouzwa, kufikia masoko mapya na kujumuisha uwekezaji mkubwa katika miundombinu teknolojia na mawasiliano bora,” amesema Dk Biteko.
Amesema jambo hilo litachochea ongezeko la uzalishaji na kuufanya kuwa wenye ushindani.
“Siyo mtu aamini kuwa ukiwa mwenyeji una sababu ya kupendelewa sana hata kama una bidhaa mbaya ambayo haikidhi viwango, ichukuliwe hivyo hivyo hapana,” amesema Dk Biteko.
Amesema biashara ina sura pana isiyokuwa na kabila, lugha, mpaka wa kijiografia hivyo kumpa mtu uwezo wa kuifanya akiwa na hela hata kama hajui lugha inayozungumzwa eneo husika.
“Unajua Kichina au hujui ukiwa na hela utafanya biashara, haina bendera ya kukutambulisha wala sarafu maalumu bali unachohitaji ni kuwa na kitu cha kubadilishana katika soko, ushindani ni muhimu, kila aliyejiandaa kushindana ndiye atashinda ambaye hakujiandaa ataishia kuwa mlalamishi, tushindane, tusijione wanyonge tujione tuna uwezo wa kuingia katika masoko yoyote,” amesema Dk Biteko.
Kuhusu kuongeza thamani ya kila bidhaa inayozalishwa nchini amesema sera inasisitiza umuhimu wa viwanda vya ndani ikiwa na lengo la kuzalisha ajira, kuongeza mapato ndani na nje ya nchi, fedha za kigeni, kupunguza utegemezi kwenye mauzo ya malighafi na kukuza matumizi ya teknolojia.
“Ikiwa ni korosho, madini basi yaongezwe thamani badala ya kuwa Taifa ambalo linazalisha malighafi kwa ajili ya wengine,” amesema Dk Biteko.
kuimarisha uwezeshaji na kurahisisha biashara pia ni jambo tarajiwa ambalo litachochewa na kuondosha vikwazo vya kibiashara, kuimarisha mahusiano na kuratibu taratibu.
“Sasa hapa kwa watu wa Serikali, heshima yako uliye kwenye dawati ni kuhakikisha mteja anayekuja kwako amefanya biashara na kupata faida si kuonyesha ugumu kutokana na mamlaka uliyokuwa nayo,” amesema Dk Biteko huku akimtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo kutowafumbia macho.
Pia sera hiyo inatarajia kuimarisha ushirikiano na majirani, kutengeneza biashara endelevu jumuishi na shirikishi, huku akisisitiza kama Taifa limejizatiti kuhakikisha kuwa manufaa yanayotokana na biashara yanawafikia watu wote.
“Ninaamini kupitia sera hii tutapata matokeo chanya kama tutaisimamia vyema,” amesema Dk Biteko.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile amesema uwe utaratibu ndani ya Serikali wa kupitia sera na kuziboresha badala ya kusubiri Bunge lielekeze au wadau kulia na kupiga kelele.
“Hivyo ni vyema mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu uwaambie mawaziri wako wawe wanakaa na kufanya mapitio katika mambo ambayo yanaingiliana katika wizara zao.”
Katika mapitio ya Sera, Mkurugenzi wa Trade Mark Afrika, Elibariki Shammy amesema tayari wameanza kutoa usaidizi wa kufanya mapitio ya sera ya uwekezaji Tanzania, inayolenga kuangalia mambo yanayopaswa kubadilishwa kuendana na wakati uliopo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Raphael Maganga amesema moja ya jambo lililowafurahisha ni viwanda na biashara kupewa nguvu na mifumo ya kisheria ili iweze kusimamia masuala ya kibiashara kwa ujumla, tofauti na sasa ambapo TPSF ilikuwa chini ya uratibu wa wizara tatu.
“Tulikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji iliyokuwa ikisimamia mazingira ya uwekezaji na Wizara ya Viwanda na Biashara na sasa wizara moja ndiyo inaratibu shughuli hizo,” amesema Maganga.