Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mbeya yaingilia kati mgomo wa walimu

Mbeya. Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) imeingilia kati sakata la walimu wa Shule ya Sekondari Ivumwe kufunga lango kuu la shule hiyo wakishinikiza kulipwa madai yao ya mishahara na posho.

Shule hiyo inamilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mbeya.

Tukio hilo limetokea leo Jumanne, Julai 30, 2024, asubuhi baada ya walimu hao kufika shuleni na kuweka magogo mbele ya lango kuu huku wakiwa na mabango yenye ujumbe ulioandikwa juu ya madai hayo.

Akitoa ufafanuzi wa sakata hilo alipozungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mbeya Mjini, Emmanuel Mwalupindi amesema baada ya kusikia taharuki hiyo amelazimika kufika shuleni hapo.

“Kimsingi baada ya kuona taarifa imeripotiwa mitandaoni nimelazimika kufika kujua kilichotokea shuleni hapo,” amesema Mwalupindi.

Amesema kilichotokea ni ucheleweshwaji wa mshahara wa mwezi mmoja kutokana na matatizo ya mfumo wa malipo.

“Tumekaa kikao na walimu na watumishi, tumelizungumza na kulimaliza. Kwa sasa walimu wameendelea na vipindi kama kawaida, jambo halikuwa kubwa tumelimaliza,” amesema.

Mwenyekiti huyo amewaomba walimu na watumishi wa shule za Serikali na za jumuiya hiyo kufuata utaratibu na sheria ya kudai stahiki zao bila kuzua taharuki kwa jamii.

“Niwatake tu watumishi kufuata taratibu na kutojiingiza kwenye siasa. Kama kuna changamoto ni vema kuwasilisha kwenye eneo husika,” amesema Mwalupindi.

Awali, mmoja wa walimu shuleni hapo ambaye hakutaka jina lake liandikwe amesema hoja yao kubwa ilikuwa ucheleweshwaji wa malipo ya mishahara na posho zao.

“Cha msingi tunahitaji zifanyike jitihada za makusudi kulipwa stahiki zetu, tunafanya kazi kwa moyo wa kujitolea na shule inafanya vizuri, linapokuja suala la malipo yetu inakuwa shida, hata kama ni mshahara wa mwezi mmoja ni wa kwangu nilipwe hiyo ni stahiki yangu, tusipakane mafuta kwa mgongo wa chupa,” amesema mwalimu huyo.

Hata hivyo, Mwananchi ilipomtafuta mkuu wa shule hiyo, Oscar Mwaihaba azungumzie suala hilo, hakupatikana shuleni hapo na alipopigiwa simu amesema yuko kikaoni wanajadili suala hilo.

Related Posts