Kesi ya Kombo wa Chadema aliyedaiwa kutekwa kuendelea tena leo

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, aliyepotea kwa mwezi mzima kisha baadaye akapandishwa kizimbani na Jeshi la Polisi Tanga, Kombo Mbwana, leo Julai 30, 2024 inaendelea katika Mahakama ya Wilaya ya Tanga.

Kesi hiyo ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024, ilipangwa leo Jumanne Julai 30, 2024 kwa ajili ya kutajwa kuangalia kama upelelezi umekamilika, pamoja na utaratibu wa dhamana kama mshtakiwa huyo atakuwa ametimiza masharti.

Tayari mshtakiwa huyo ameshafikishwa mahakamani kwa ajili ya kuendelea na taratibu hizo.

Amefikishwa mahakamani hapo akiwa ndani ya gari la polisi kisha akashushwa na kupelekwa katika mahabusu ya mahakamani hiyo yeye na washtakiwa wengine, na sasa anasubiri kesi yake kuitwa baada ya maandalizi kukamilika.

Katika kesi hiyo mshtakiwa Kombo Mbwana anakabiliwa na mashtaka matatu chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Katika shtaka la kwanza anadaiwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume na kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 9, 2024 katika mtaa wa Hassan Ngwilizi ndani ya Wilaya na Mkoa wa Tanga.

Anadaiwa kuwa siku hiyo alikutwa akimiliki laini ya Tigo yenye namba (ICCID) 8925502042093621824, iliyosajiliwa kwa jina la Shukru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.

Shtaka la pili anadaiwa kushindwa kisajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine, na shtaka la tatu anadaiwa kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini ya simu.

Kombo alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 16, 2024, na kusomewa mashtaka hayo, ambayo hata hivyo aliyakana.

Dhamana yake ilikuwa wazi Kwa kuwa mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.

Hakimu Mfawidhi Moses Maroa anayesikiliza kesi hiyo alimpa masharti ya dhamana ambayo alipaswa kuyatimiza kwanza kabla ya kiachiwa kwa dhamana.

Masharti hayo ni kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa wanakokaa pamoja na vitambulisho vya Taifa (Nida).

Hata hivyo alishindwa kutimiza masharti hayo na akapelekwa mahabusu.

Wakili wake Deogratius Mahinyila amelieleza Mwananchi kuwa kwa leo wamejiandaa kukamilisha masharti ya dhamana.

Amesema siku ya kwanza walishindwa kutimiza masharti ya dhamana kulingana na mazingira yaliyojitokeza.

Amesema siku hiyo mteja wao akifikishwa mahakamani na kupandishwa kizimbani ambako alisomewa mashtaka hayo saa 11 jioni wakati ambapo ndugu zake hawakuwepo kwa kuwa hawakuwa na taarifa, na kwamba hata Hakimu hakuwepo.

“Hata Hakimu alikuwa amekwishaondoka hivyo ilibidi wampigie simu ndipo akaja kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa mashtaka. Kwa hiyo kwa kuwa hata ndugu zake hawakuwepo ilikuwa ni vigumu kuwapatia wadhamini,” amesema Wakili Mahinyila.

Amesema kesho yake, Julai 17, 2024 ndugu zake walianza kufuatilia utaratibu wa dhamana na kuandaa nyaraka zinazohitajika na kwamba wao mawakili walifika mahakamani Julai 18, kuomba hati ya mshtakiwa kutolewa mahabusu na kufikishwa mahakamani kwa ajili ya dhamana.

Amesema licha ya mahakama kutoa hati hiyo mara mbili mfululizo, lakini bado Jeshi la Polisi halikuweza kumfikisha mahakamani mshtakiwa huyo kwa ajili ya dhamana.

Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kijiji cha Kwamsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kupelekwa mahali ambako hata ndugu zake hawakupafahamu.

Aliwekwa kizuizini kwa takribani mwezi mmoja kasoro siku moja, mpaka Julai 14, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard alipotangaza kuwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi.

Alisema kuwa anashikiliwa kwa tuhuma za kutumia vifaa vya Kielektroniki na laini za mitandao mbalimbali zisizo na usajili na kutekeleza uhalifu huo, kinyume na Sheria, ndipo Julai 6, 2024 akapandishwa kizimbani.

Related Posts