TIMU ya Kigamboni Queens imekiona cha moto katika Ligi ya Kikapu ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) ni baada ya kufungwa na Vijana Queens kwa pointi 119-54.
Mchezo huo ulioshuhudiwa na watazamaji wengi ulifanyika katika Uwanja wa Donbosco Osterbay.
Timu ya Vijana Queens ilianza mchezo katika robo ya kwanza kwa kasi huku ikitumia mbinu ya kupasiana pasi ndefu maarufu kama fast break, jambo lililoifanya Kigamboni Queens ipoteane.
Kupoteana huko kuliwafanya Vijana Queens watumie nafasi hiyo kuongoza katika robo zote tatu kwa pointi 35-11, 30-12 na 34-11.
Katika mchezo huo Khadija Karambo wa Vijana Queens aliongoza kwa kufunga pointi 30 na kati ya hizo alifunga maeneo ya mitupo mitatu mara nne na asisti mara tatu.
Aliyemfuatia alikuwa Tumaini Ndossi aliyefunga pointi 24, kudaka mipira ya ‘rebound’ mara nane na asisti tisa.