Lindi. Makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi wameeleza kusikitishwa na taarifa za kujiuzulu kwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho-Bara, Abdulrahman Kinana huku wakitumaini kumpata mrithi wake mwenye sifa na busara za kiuongozi kama yeye.
Kinana alijiuzulu wadhifa huo jana Jumatatu Julai 29, 2024; huku taarifa kwa umma iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, ikisema mwenyekiti wa chama, Rais Samia Suluhu Hassan amekubali ombi lake hilo.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumanne Julai 30, 2024 mkoani Lindi, makada wa CCM wameeleza Kinana alikuwa kiongozi mwenye busara na hekima na mara nyingi amekuwa akikivusha chama kwenye nyakati ngumu.
Kada wa CCM kutoka Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Shaweji Mwinja amesema anamkumbuka Kinana tangu alipokuwa Waziri wa Ulinzi, akiwa mmoja wa viongozi wachapa kazi hodari.
Akiwa ndani ya CCM, Mwinja amesema Kinana ni kiongozi mwadilifu, hajawahi kumwona akiwa na kashfa yoyote na amekisaidia chama kwenye nyakati ngumu na kukivusha salama.
“Ni kiongozi bora ambaye alistahili kutumikia katika nafasi hizo alizotumikia CCM. Sijui nini kimemsukuma kufanya hivyo, lakini tunakubali uamuzi wake.”
Kuhusu anayefaa kuwa mrithi wake, Mwinja hakutaka kutaja jina lakini amesema chama hicho kina watu wengi wenye sifa za kushika nafasi hiyo na anaamini kamati kuu itawapatika wanaCCM kiongozi bora.
“Chama hakiwezi kuyumba kwa sababu kina hazina ya watu wengi, muda si mrefu atapatikana kiongozi mwingine mwenye sifa za kushika nafasi hiyo,” amesema kada huyo wa CCM.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Chenjele iliyopo Wilaya ya Ruangwa, Abdallah Chionda amesema amepokea kwa masikitiko ya kujiuzulu kwa makamu mwenyekiti wa CCM.
“Hatujazipokea vizuri taarifa hizi za kiongozi wetu, lakini kwa kuwa ni suala binafsi, tunaheshimu,” amesema kiongozi huyo wakati akizungumza na Mwananchi Lindi Mjini.
Amesema watamkumbuka kwa umakini wake katika kuongoza chama na amehimili kila hali iliyojitokeza kwenye chama, anatarajia kwamba watakaofuata wataiga mfano wake.
“Kamati Kuu ina watu mahiri, watapata mtu makini wa kuendeleza kazi aliyokuwa akiifanya. Chama kina watu wengi wenye hekima, busara na maarifa, sina mashaka kwamba tutapata mtu wa aina yake,” amesema Chionda.
Mkazi wa Lindi Mjini, Salama Nassoro amesema uamuzi wa Kinana kujiuzulu ni mgumu kwa wanachama na viongozi wa juu wa chama, hata hivyo, amesema ni muhimu kuheshimu uamuzi wake na kuhakikisha kwamba makamu mwenyekiti ajaye anakuwa na sifa ya uadilifu, hekima na busara za kiuongozi.
“Siwezi kujua anayekuja ni nani lakini ningependa awe kama Kinana au hata zaidi yake. Watu wenye sifa za kushika nafasi hiyo wapo, ninawachoomba tupate mrithi wake mwenye sifa za kiuongozi,” amesema Salama.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Lindi Vijijini, Nassib Makombe amesema atamkumbuka Kinana kwa nasaha zake kama mwalimu wa siasa kwa vijana wengi wa vizazi vyote kikiwamo hiki cha sasa.
“Kwa kuwa mwenyekiti wetu, Rais Samia amekubali ombi lake, na sisi pia tumepokea uamuzi wake kwa moyo wote. CCM bado iko imara na ina mifumo yake ya kushughulikia masuala kama haya, na nina imani kuwa hivi karibuni tutampata mrithi wake,” amesema Makombe