Dar es Salaam. Nani mrithi wa nafasi ya makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara? Hili ndilo swali linaloulizwa na wengi baada ya aliyekuwa na wadhifa huo, Abdulrahman Kinana kujiuzulu.
Taarifa ya kujiuzulu kwa Kinana ilitolewa juzi na CCM, ikinukuu sehemu ya barua ya Rais Samia Suluhu Hassan, mwenyekiti wa chama hicho, akijibu “kukubali kwa moyo mzito” ombi la mwanasiasa huyo mkongwe.
“Nilipokuomba utusaidie kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti nilikuahidi utakaa kwa muda mfupi kama ulivyoomba na kwa kweli nilipenda uendelee kutusaidia.
“Lakini kwa kuwa umeomba sana na ahadi ni deni, nalazimika kwa moyo mzito kuridhia kujiuzulu kwako,” imeeleza taarifa ya CCM ikinukuu barua ya Rais Samia kujibu ombi la Kinana.
Uamuzi wa Kinana umeibua kiu ya wadau wa siasa, makada na wafuasi wa chama hicho, kujua nani atakayerithi mikoba ya mwanasiasa huyo.
Shauku ya wadau hao inapozwa na taarifa za ndani ambazo Mwananchi linazo kuwa, miongoni mwa wanasiasa walio karibu kuirithi nafasi hiyo, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Pinda ambaye ambaye tangu amestaafu uwaziri mkuu mwaka 2015 ameendelea kuwemo kwenye vikao vya juu ya CCM kwa njia ya uteuzi, na hadi sasa akiwa mjumbe wa Kamati Kuu, anatajwa kuwa mtu sahihi wa kuvaa viatu vya Kinana.
Haiba na matendo yake tangu akiwa mbunge wa Mpanda Mashariki, Naibu Waziri na Waziri wa Tamisemi kisha Waziri Mkuu, anapewa turufu kubwa.
Miongoni mwa wanaotajwa, Pinda anapewa nafasi kubwa kushika wadhifa huo. Habari za ndani kutoka kwenye chanzo cha kuaminika ndani ya CCM, zinasema Pinda ana haiba ya kipekee na tabia yake ya kutojikweza ambayo imemfanya kukubalika kwa wengi.
Inaelezewa kuwa katika kipindi cha karibuni, amekuwa akitumika kama mshauri kwenye masuala mbalimbali ndani ya chama.
“Ni mtu ambaye hana makundi ndani ya chama, anasikiliza na kushauri ndio sababu anapewa nafasi kubwa kumrithi Kinana. Chama kinakwenda kwenye uchaguzi, ni muhimu kuwa na kiongozi mwenye Kariba yake.
“Ni mpole, muwazi lakini ana msimamo pale anapokuwa akitimiza majukumu yake. Sasa mtu wa aina yake ndiye sahihi kuwa makamu mwenyekiti,” kimesema chanzo hicho.
Chanzo kingine ndani ya chama kikongwe, kimeeleza kuwa Pinda atakuwa chachu ya kuunganisha makundi ndani ya CCM ambayo kwa sasa yameanza kuonyesha makucha.
Kilisema mbali na kuunganisha makundi, Pinda atakuwa chachu katika kukukiwezesha chama hicho kuvuna kura kwenye mikoa ya Katavi, Rukwa ambako amekuwa akiheshimika kutokana na mchango wake katika maendeleo.
“Mama ametoka ziara kwenye mikoa ya Katavi na Rukwa na wote mmeona nini kimetokea kule, Pinda alikuwepo na nafasi yake ilionekana licha ya kuwa ni mstaafu yule. Kinachosubiriwa ni siku tu, lakini kwa hakika ni Pinda,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, Pinda hakutajwa peke yake, pia wamo aliyewahi kuwa waziri kwa muda mrefu Steven Wasira, Waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye na mwenyekiti mstaafu wa Jumuiya ya Wazazi, Abdallah Bulembo, miongoni mwa wanaohusishwa na kurithi wadhifa huo wa pili kwa ukubwa ndani ya CCM.
Utaratibu kumrithi Kinana
Kutokana na uzito wa nafsi ya makamu mwenyekiti wa CCM, utaratibu wa kuirithi si lelemama, chama hicho kitalazimika ama kuitisha mkutano mkuu wa taifa wa dharura au kisubiri mkutamo mkuu wa kawaida, ambao ndiyo wenye wajibu wa kumchagua mwenyekiti na makamu wenyeviti wawili, wa Bara na wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Ibara ya 99 (3) Mkutano Mkuu wa Taifa wa kawaida wenye wajumbe takriban 2,000, hufanyika mara tatu katika kipindi cha miaka mitano.
Lakini, mkutano wa dharura unaweza kufanyika wakati wowote ukiitishwa na mwenyekiti wa CCM au ukiombwa na theluthi mbili ya wajumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya chama hicho.
Taarifa ambazo Mwananchi limedokezwa ni kuwa mwezi ujao huenda ukaitishwa mkutano mkuu maalumu (wa dharura) kujaza nafasi hiyo.
“Nafasi hii ni nyeti, inapaswa kujazwa haraka hasa tunapokwenda kwenye uchaguzi mkuu, mkutano mkuu utaitishwa mwezi ujao ili kuijaza nafasi hiyo,” kimesema chanzo chetu na kuomba jina lihifadhiwe.
Uzito wa nafasi hiyo pia unawekwa na kanuni za Maadili na Uongozi cha CCM, zinazomtambua makamu mwenyekiti (Bara), kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Udhibiti ya Kamati ya Usalama na Maadili Taifa.
Kamati hiyo inaundwa na wajumbe wanne, ikiongozwa na makamu mwenyekiti Bara kama mwenyekiti, wengine ni mkurugenzi wa maadili ngazi ya taifa kama katibu na wajumbe wawili wa Kamati Kuu kutoka Zanzibar na Bara.
Kamati hiyo ndiyo yenye wajibu wa kusikiliza, kuhoji na kupendekeza adhabu kwa watuhumiwa wenye mashtaka yanayopelekwa kwa uamuzi, kwenye vikao vya ngazi za juu.
Hivyo kuondoka kwa Kinana kunakipa fursa chama hicho kujiimarisha kuelekea chaguzi zijazo, ikiwa ni pamoja na kumpata makamu imara, asiye na mawaa atakayesimamia masuala ya kimaadili kuelekea uchaguzi unaokuja.
Hatua inakuja ikiwa ni takribani miezi sita tangu Halmashauri Kuu ya CCM ilipomthibitisha Dk Emmauel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu, John Mongella kuwa Naibu Katibu Mkuu-Bara na Amos Makalla kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo.
Mabadiliko hayo ya sekretarieti yalifanyika Januari 15, 2024 baada ya Daniel Chongolo aliyekuwa kujiuzulu. Kwa sasa Chongolo ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Mbali na masuala ya maadili na kumsaidia mwenyekiti kukisimamia chama, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema atakuwa na kazi ya kulikabili fukuto linalodaiwa kuwepo ndani ya chama hicho, likihusisha kujitokeza kwa mtandao wa wawania uongozi wa juu ndani ya Serikali.
Kabobe amekwenda mbali akihusisha fukuto hilo na panga pangua inayoendelea kwenye baraza la mawaziri na vyombo vya dola kuwa ni mbinu za kukabiliana na mtandao huo.
Amesema ni jukumu la makamu mwenyekiti anayekuja kukabiliana na hali hiyo.
“Kwahiyo lazima makamu mwenyekiti ajaye ajue haya mambo matatu na kuweka mikakati ya namna ya kuyakabili,” amesema na kusisitiza kuwa uzito huo nafasi unatokana na mwenyekiti wa chama hicho huwa na kofia ya urais ambako anatumia muda mwingi kwenye nafasi hiyo na hivyo, makamu mwenyekiti ndiye anayepaswa kusimamia zaidi shughuli za chama.
“Lazima CCM ijipange kwenye hilo na sina shaka maana ni chama kikongwe chenye watu wazoefu sana ndani na nje yake. Kumpata mvaaji wa viatu vya Kinana haiwezi kuwa kazi kubwa,” amesema.
Pamoja na sababu zilizotajwa, kujiuzulu kwa Kinana bado kunatazamwa kwa jicho zaidi ya moja. Kwa mtazamo wake, Dk Kabobe amesema uamuzi huo mbali na kuchochewa na dhamira ya kupumzika kutokana na umri wake (miaka 73), lakini huenda anataka kuruhusu mabadiliko ndani ya chama hicho.
Amesema Kinana ni mwanasiasa mkongwe na mahiri, aliyekuwa kwenye siasa za ushindani tangu mwaka 1995 akiwa meneja wa kampeni wa Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa.
“Anaijua siasa, anaijua CCM vizuri, kuondoka kwake kunakupa tafsiri mbili; Kupumzika maana katumika muda mrefu na umri umekwenda na kuruhusu mabadiliko ndani ya chama ili kijipange vema zaidi kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani,” amesema.
Hoja zinazofanana na hizo, zilitolewa pia na mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohamed Bakari aliyetaja umri na upepo wa kisiasa wa wakati husika.
Kuhusu umri, mwanazuoni huyo alifafanua katika siasa mtu binafsi anapofikia umri fulani anaamua kwa utashi wake kupumzika katika nafasi za uongozi.
“Kinana ana miaka zaidi ya 70, amekitumikia chama na Serikali kwa muda mrefu na unafika wakati mtu anaona huna sababu ya kuendelea. Badala ya kusubiri apumzishwe anajitathmini anaona apumzike mwenyewe,” amesema.
Kupumzika huko, Profesa Bakari amesema hakuna maana ya kukaa pembeni kabisa, bali ni kujiondoa kwenye nafasi ya uongozi, huku akiendelea kutumika na chama kama mshauri.
Sababu nyingine kwa mujibu wa mwanazuoni huyo ni hali ya siasa ya wakati husika, akisema pengine kujiuzulu kwake kumechochewa na ukaribu alionao na January Makamba na Nape Nnauye ambao Julai 21, walitenguliwa katika nyadhifa zao za uwaziri.
“Kinana anatajwa kuwa karibu na kina Makamba na Nape na aliwalea kiuongozi, pengine kunakuwa na hali ya kutiliana shaka, kwa hiyo mtu kama yeye anasoma alama za nyakati, anaamua kuondoka kabla ya kuondolewa ili kulinda heshima yake,” ameeleza.
Kuondoka kwa Kinana katika uongozi wa CCM, amesema unakifanya chama hicho kuzikosa busara zake akiwa ndani ya uongozi, lakini vijana waliopo watakosa la kujifunza kutoka kwake.
Upande mwingine, amesema kuondoka kwake ni fursa kwa vijana ambao watakuwa na nguvu zaidi au wazee walio na umri wa chini yake kuipata nafasi hiyo.
“Anavyoondoka kiongozi mmoja anaingia kiongozi mwingine na kwa asili ya CCM kuondoka si pigo atakuja mtu ataendelea palepale alipoishia yeye,” amesema.
Pinda alizaliwa Agosti 12, mwaka 1948 mkoani Katavi na baadaye alipata elimu ya msingi katika Shule za Kakuni na Kaengesa mkoani Rukwa kuanzia mwaka 1957 hadi 1964.
Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari St. Francis ambayo kwa sasa inafahamika kama Pugu kwa ajili ya elimu ya sekondari mwaka 1965 hadi 1968, kisha Shule ya Sekondari Musoma kwa ajili ya kidato cha tano na sita.
Shahada yake ya kwanza ilikuwa katika sheria, aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1971 hadi 1974.
Alipohitimu shahada yake aliajiriwa kuwa mwanasheria katika Wizara ya Sheria alikohudumu kwa miaka minne, kabla ya kuhamishiwa Ikulu akiwa Katibu Msaidizi wa Rais wa wakati huo, Julius Nyerere.
Mwanzo wake maisha ya siasa ulikuwa mwaka 2000 alipogombea na kushinda ubunge wa Mpanda Mashariki, wadhifa uliompa uteuzi wa Naibu Waziri wa Tamisemi.
Baadaye alipanda cheo na kuwa waziri kamili katika wizara hiyo hiyo ya Tamisemi hadi wakati wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete na baadaye mwaka 2008 aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu akimrithi Edward Lowassa aliyejiuzulu.
Kama ilivyo kwa Pinda, jina la Wasira limeendelea kung’ara ndani ya CCM, licha ya umri wa miaka 79 na amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kwa muda mrefu na mara ya mwisho mwaka 2022 alichaguliwa na mkutano mkuu kwa 680 kuwa mjumbe wa NEC.
Akiwa amezaliwa Bunda mkoani Mara, alipohitimu kidato cha nne, Wasira alianza kukitumikia Chama cha Tanu akiwa Katibu wa Wilaya mwaka 1967 hadi 1973 na mwaka 1975 hadi 1982 alihudumu nafasi ya mkuu wa Mkoa wa Mara.
Baadaye mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Ubalozi wa Tanzania Washington DC na aliporejea nchini kabla ya kuteuliwa na Rais wa kati huo, Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani mwaka 1990 hadi 1991.
Kati ya mwaka 1993 hadi 1995 alisoma tena Shahada ya Uzamili ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Amerika.
Akiwa na umri wa miaka 25, Wasira alianza kutumikia wadhifa wa ubunge, hii ilikuwa mwaka 1970 aliposhinda ubunge wa Mwibara na akaongoza hadi mwaka 1975 huku Nyerere akimteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.
Mwaka 1985, Wasira aligombea na kushinda ubunge wa Bunda na kisha aliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuwa Naibu Waziri wa Serikali za Mitaa na baadaye Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo mwaka 1989 hadi 1990.
Mwaka 1995, Wasira alipoangushwa kwenye kura za maoni za ndani ya CCM na Jaji Joseph Warioba, aliamua kwenda NCCR Mageuzi na akachaguliwa kwa kura 18,815 dhidi ya 17,527 za Warioba. Warioba alikata rufaa Mahakama Kuu nayo ikatengua ubunge wa Wasira mwaka 1996 baada ya kujiridhisha kuwa kulikuwa na rafu nyingi zilizofanyika.
Uchaguzi mdogo ulipofanyika mwaka 1999 Wasira hakushiriki na baadaye aliamua kurejea CCM.
Alirejea katika ulingo wa siasa mwaka 2005 na kushinda kura za maoni ndani ya CCM na akapitishwa kugombea ubunge wa Bunda alikopita bila kupingwa. Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Maji Januari 2006 hadi Oktoba 2006, baadaye Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika hadi mwaka 2010. Amewahi kuwa Waziri wa Tamisemi na alikuwa miongoni mwa watia nia ya urais kupitia CCM mwaka 2015.
Huku pia ni waziri mkuu mstaafu. Alizaliwa mwaka 1950 wilayani Hanang, alihudumu kwa nafasi ya ubunge tangu mwaka 1983 hadi mwaka 2005, kadhalika amekuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri akiongoza wizara ya Kilimo, Mifugo na Ushirika.
Mwaka 1995 hadi 2005 Sumaye alikuwa Waziri Mkuu na ndiye anayeshika rekodi ya kuhudumu kwenye wadhifa huo kwa muda mrefu zaidi.
Sumaye naye alikuwa mmoja wa watia nia ya urais mwaka 2015 na hakufanikiwa kuchaguliwa katika mchakato wa ndani ya chama chake, baadaye alikihama CCM na kuhamia Chadema.
Alishiriki kampeni za urais ndani ya Chadema akimnadi Edward Lowassa na baadaye mwaka 2019 alitangaza kuachana na siasa za vyama. Hiyo ilikuwa baada ya kushindwa uenyekiti wa Kanda ya Pwani wa Chadema.
Haukuisha hata mwaka, Sumaye alitangaza kurejea ndani ya chama chake cha zamani, CCM hadi sasa.
Katika siasa za CCM Bulembo alipata umaarufu zaidi mwaka 2012 aliposhinda uchaguzi wa ndani wa chama hicho wa nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi.
Uchaguzi huo ulifanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Athuman Mhina aliyefariki dunia mwaka 2011 na kuacha wazi wadhifa huo kwa takriban mwaka mzima.
Umaarufu zaidi katika siasa uliota mizizi mwaka 2015 alipoteuliwa kuwa Meneja wa Kampeni za aliyekuwa mgombea urais wa CCM wa wakati huo, John Magufuli.
Baada ya uchaguzi, Bulembo aliteuliwa kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi aliyohudumu mwaka 2015 hadi 2020.
Ukiachana na nafasi hiyo, Juni 13, mwaka huu Bulembo aliteuliwa na Rais Samia kuwa mshauri wake katika Siasa na Uhusiano wa Jamii.
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.