Meli iliyobeba magari 300 yatia nanga Bandari ya Tanga

Tanga. Meli ya mizigo ya Kampuni ya Seefront Shipping Service Limited yenye uzito wa tani 14,000 iliyobeba magari 300 ya wafanyabiashara wa nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Burundi, na Rwanda imetia nanga katika Bandari ya Tanga baada ya Serikali kuiboresha bandari hiyo.

Akizungumza baada ya kuwasili kwa meli hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile leo Jumanne Julai 30, 2024, akiwa na viongozi wengine, amesema fedha zilizowekezwa katika maboresho hayo ni nyingi, lengo la Serikali ni kuongeza ubora wa utoaji huduma.

 “Shehena za mizigo zimeongezeka kutoka tani 470,000 kwa mwaka 2019 na kufikia tani milioni moja mpaka sasa,” amesema naibu waziri huyo.

Amesema licha ya ongezeko hilo, meli zinazotumia bandari hiyo kushusha mizigo nazo zimeongezeka kutoka 118 mwaka 2019 na sasa ni meli 307.

“Haya ni mapinduzi makubwa yanayoonesha kwamba fedha zilizowekezwa zinaleta tija. Hongereni kwa usimamizi mzuri, wastani wa kuongeza uhudumiaji wa meli kila mwaka unadhihirisha fedha iliyowekezwa hapa haikutupwa, lakini pia watendaji hawakulala usingizi,” amesema Naibu Waziri David.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema kupitia maboresho hayo tayari wamepokea meli 35 zilizobeba tani 330,173 kwa mwezi huu, wakati walijiwekea lengo la kupokea meli 19. Hivyo, wamevuka lengo kabla ya mwezi haujaisha.

Amesema Julai 2023, walihudumia meli zenye tani 46,000 na Julai mwaka huu tayari wamehudumia tani 96,000, na lengo ni kupokea tani milioni 1.4.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani amesema, “niwaombe wadau wote wenye kampuni za wakala wa meli waendelee kutumia bandari yetu ya Tanga. Ujio wa meli hii ni faraja kubwa kwa mkoa wetu, imani yetu ujio wa meli hii unaendelea kupanua wigo na fursa za kibiashara,” amesema Balozi Buriani.

Meli hiyo imetumia siku 21 kutoka nchini China hadi kufika Tanzania, ikiwa na mzigo wa magari ya mizigo kwenda nchi jirani na Tanzania. 

Related Posts