Mutale apewa mbinu Msimbazi, ajiita ‘Mwamba wa Zambia’

WINGA mpya wa Simba, Joshua Mutale kwa sasa anajiita Mwamba wa Zambia, kitu kilichowaibua baadhi ya mastaa wa zamani wa timu hiyo kumpa mbinu ya kufanya vitu vikubwa vitakavyoendana na jina hilo linalotumiwa na nyota mpya wa Simba.

Mojawapo wa video katika mitandao ya kijamii ya Simba inamuonyesha Mutale akijiita Mwamba la Zambia, lakini kabla yake ndani ya kikosi hicho alikuwepo Clatous Chama aliyepo Yanga kwa sasa ambaye alikuwa anajiita Mwamba wa Lusaka.

Kabla ya kujiita Mwamba wa Zambia, Mutale aliwahi kukiri kwamba, Chama na Moses Phiri ndio sababu ya Simba kuamini  wachezaji kutoka Zambia kutokana na kazi walizozifanya ndani ya kikosi hicho zinazompa chachu ya kupambana kuandika za kwake zitakazowafanya wengine waendelee kupata nafasi ya kuja kucheza Tanzania.

Straika wa zamani wa timu hiyo, Athuman Machupa alisema ili Mutale ajijengee ufalme ndani ya klabu hiyo, kiwango chake kiwe na mchango mkubwa akimsisitiza kwamba azingatie nidhamu na kujituma.

“Soka haliongopi linachezwa sehemu za wazi ambapo kila mtu anaona anachokifanya. Kama Chama alitikisa na jina lake la Mwamba wa Lusaka, Phiri la jenerari, naamini kwa umri wake (Mutale) kama atazingatia nidhamu na kujituma ataishi kwenye ndoto ya jina lake kuwa kubwa,” alisema.

Mchezaji mwingine wa zamani wa timu hiyo, Frank Kasanga ‘Bwalya’ alisema: “Bado hatujaona wachezaji wapya wanavyocheza, ila kwa mechi ambazo nimewahi kumuona ni mchezaji mzuri. Jambo la msingi ajitambue, katika soka nidhamu ndio kila kitu. Akifanya hivyo atafanya makubwa na Wanasimba watamwita Mwamba wa Zambia.”

Mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Danny Mrwanda alisema: “Heshima yake Mutale ni rahisi kujengeka endapo tu atafanya majukumu yake ipasavyo, kwani soka halina njia za mkato.”

Mrwanda alisema mchezaji huyo akifanya kazi nzuri mashabiki wanaweza wakampa jina lingine zaidi ya hil la Mwamba wa Zambia, akisisitiza kiwango chake kitampa heshima anayotaka.

Wakati Mutale anaitambulisha a.k.a aliwaomba mashabiki wa Simba kuwaunga mkono katika majukumu yao.

“Wapenzi wa Simba, mtuunge mkono, kwani Simba ni nguvu moja.”

Related Posts