Mapema wiki hii, mawaziri wa mambo ya nje wa Italia, Austria, Croatia, Jamhuri ya Czech, Cyprus, Ugiriki, Slovenia na Slovakia walisema wako tayari kurekebisha mahusiano yao na Rais wa Syria Bashar Assad.
Katika barua yao ya pamoja, mataifa hayo yalipendekeza kuundwa kwa ofisi ya mjumbe wa Umoja wa Ulaya kwa Syria ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia mikakati ya kuanzishwa tena kwa ubalozi wa Syria mjini Brussels na kuteua “maeneo salama” yapatayo 10 katika sehemu inayodhibitiwa na serikali ya Syria ambako wahamiaji raia wa Syria waliopo Ulaya wangeweza kurejeshwa na kuhifadhiwa.
Ingawa Ujerumani haikuwa miongoni mwa waliotia saini, mojawapo ya mahakama kuu nchini humo iliamua wiki hii kwamba kwa ujumla, hakuna tena hali ya hatari kwa raia kutokana na mzozo wa muda mrefu nchini Syria.
Hata hivyo waangalizi wa haki za binadamu, wachambuzi wa siasa na hata maafisa wa Umoja wa Mataifa, wote wameafikiana kwamba Syria si nchi salama kwa wakazi wala kwa wakimbizi wanaorejea.
Soma pia: Jumuiya ya Kimataifa yaichangia Syria
Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Geir Pedersen ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki hii kuwa Syria bado inasalia katika hali ya migogoro, utata na migawanyiko, huku kukiwa na makundi kadhaa yenye silaha, magaidi, wanamgambo wa kigeni. Pedersen amesisitiza kuwa raia wa syria wanaendelea kukabiliwa na vitendo vya ghasia na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na hata kulazimika kuyahama makazi yao.
‘Kuanzisha upya uhusiano na Ulaya kutaimarisha uhalali wa Assad’
Kitendo cha baadhi ya mataifa ya Ulaya kutaka kurekebisha mahusiano yake na Syria ni cha hivi karibuni zaidi katika mfululizo wa hatua kama hizo zinazochukuliwa na nchi na taasisi zingine. Ulaya ilivunja mahusiano na serikali mjini Damascus kutokana na ukandamizaji wake wa kikatili dhidi ya waandamanaji mnamo mwaka wa 2011 ambao ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea.
Soma pia: Borrell asema utawala wa Bashar al-Assad hauko tayari kwa mabadiliko
Mwaka 2023, Syria ilirejeshwa katika Jumuiya ya nchi za kiarabu inayozijumuisha nchi 22 ambazo pia zilikuwa zimeitenga Syria kwa takriban miaka 12. Mwezi huu, rais al-Assad anapanga kukutana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye kwa miaka mingi amekuwa akiunga mkono upinzani, ambao unaendelea kupambana na majeshi ya serikali ya Syria katika eneo la kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Wachambuzi wameipokeaje hatua hiyo?
Kelly Petillo, mtafiti wa masuala ya Mashariki ya Kati katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni, ameiambia DW kwamba kuanzishwa tena kwa mahusiano kati ya Ulaya na Syria kutaimarisha uhalali wa Assad kama mtawala wa nchi hiyo na kuaminisha madai yake kwamba Syria ni nchi salama.
Hata hivyo mchambuzi huyo anasema kuwa rais Assad si mshindi katika vita hivyo kwani bado kunashuhudiwa migawanyiko ya kisiasa na kieneo nchini humo. Wakati majeshi ya Assad yakidhibiti takriban asilimia 60 ya nchi kutokana na usaidizi wa Urusi na Iran, eneo la kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo limesalia chini ya udhibiti wa Wakurdi, na kaskazini-magharibi ikiwa ni ngome ya mwisho ya upinzani wa Syria. Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024, mashambulizi ya kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS yameongezeka maradufu nchini Syria.
Hata hivyo, hatua hiyo ya Ulaya kurekebisha mahusiano yake na Syria na kuteua maeneo salama watakaporejeshwa wahamiaji, kutamaanisha pia kusitishwa kwa vikwazo ya Umoja Ulaya dhidi ya Syria, ambavyo kwa miaka mingi vimekuwa vikizorotesha hali ya uchumi.
Kulingana na ripoti ya hivi punde ya Ufuatiliaji wa Uchumi wa Syria iliyotolewa na Benki ya Dunia, upungufu wa ufadhili na ufikiaji mdogo wa usaidizi wa kibinadamu vimedhoofisha pakubwa uwezo wa kaya nchini Syria kukidhi mahitaji yao ya msingi hasa katika wakati huu kukishuhudiwa mfumuko wa bei.
(DW)