Arusha. Mwanaharakati Onesmo Ole Ngurumwa, amepata ushindi katika rufaa aliyofungua Mahakama ya Rufani, akipinga kuondolewa mahakamani kesi yake ya kikatiba dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Alifungua kesi akipinga vifungu 13 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) akidai vinakiuka Katiba.
Kesi hiyo iliondolewa Mahakama Kuu ilipotoa uamuzi wa pingamizi lililowasilishwa na AG akitaka iondolewe kwa kuwa ni mbaya kisheria.
Mahakama ya Rufani imeagiza kesi hiyo namba 36 ya mwaka 2019 irejeshwe Mahakama Kuu mbele ya jaji mmoja, ili aamue pingamizi za awali zilizotolewa katika majibu ya ombi na hatua zaidi kwa mujibu wa sheria, kwa kuwa uamuzi wa awali ulikuwa kinyume cha sheria na batili kwa kukosa mamlaka.
Rufaa hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Salaam uliotolewa mwaka 2020 ambao ulitupilia mbali kesi hiyo kwa misingi kuwa aina ya maombi na kiini cha msingi katika maombi hayo, kilishaamriwa katika kesi ya awali.
Katika kesi hiyo alikuwa akipinga vifungu vya CPA vinavyoruhusu washtakiwa kushtakiwa kwenyemahakama za chini ambazo hazina mamlaka kisheria kusikiliza mashauri yanayosikilizwa na Mahakama Kuu.
Vifungu vya CPA vinavyolalamikiwa ni namba 178, 243, 244, 245, 246, 247, 248, 249, 250, 256, 257, 258 na 259 ikidaiwa vinakiuka Katiba na haki za binadamu, ikiwemo haki ya kusikilizwa kwa usawa, usawa mbele ya sheria ambazo zipo katika ibara ya 13 (1) (2) na (6) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani limetoa uamuzi jana Jumatatu Julai 29, 2024 katika kikao kilichoketi Dar es Salaam. Majaji hao ni Augustine Mwarija, Sam Rumanyika na Lameck Mlacha.
Jaji Mlacha katika uamuzi huo amesema ugawaji upya wa kesi lazima ufanywe kwa mujibu wa sheria la sivyo shauri na uamuzi utakuwa na matokeo sawa na kilichofanywa na jopo la majaji watatu, kumpangia kesi mmoja wao, kusikiliza na kuamua pingamizi la awali ikiwa ni kinyume cha sheria na batili kwa kukosa mamlaka.
Amesema rufaa inaruhusiwa kwa maelekezo kwamba, ombi lirejeshwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kumpa jaji mmoja kuamua pingamizi za awali zilizotolewa katika majibu ya ombi na hatua zaidi kwa mujibu wa sheria.
Hoja za rufaa hiyo namba 165/2021 zilizowasilishwa na wakili Mpale Mpoki akishirikiana na wakili Daimu Halfan, ni kwamba Mahakama Kuu ilikosea kutupilia mbali kesi hiyo kwa kigezo kuwa kiini na aina ya kesi hiyo ilikwishaamriwa katika kesi nyingine.
Alieleza katika kesi iliyotajwa, ilipinga vifungu viwili pekee wakati mteja wake anapinga vifungu 13.
Hoja nyingine ni majaji watatu wa Mahakama Kuu kukosea kumpangia jaji mmoja kati yao kusikiliza pingamizi lililosababisha kesi hiyo kutupwa kinyume cha utaratibu.
Amesema ilitakiwa Jaji Kiongozi ndiye apange jaji mmoja kwa ajili ya kusikiliza pingamizi.
Ole Ngurumwa anapinga uhalali wa vifungu hivyo vya CPA vinavyotoa hitaji la kufanya uchunguzi wa awali na mashauri katika mahakama ya chini kabla ya kesi kusikilizwa, akidai ni kinyume cha Katiba na batili.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama, anadai masharti ya vifungu hivyo yanachelewesha kusikilizwa kwa mashauri kinyume cha ibara ya 13 (6) (a), yanabagua na kukiuka ibara ya 13 (1) na kukiuka kanuni za mashauri ya haki yaliyomo katika ibara ya 13(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Inadaiwa usikilizwaji wa awali unaoendeshwa na Mahakama Kuu chini ya kifungu cha 192 cha CPA unaweza kuwa mbadala wa uchunguzi wa awali.
Katika aya ya saba ya hati ya kiapo, inaelezwa masharti hayo ni ya kibaguzi na yanakiuka haki ya kusikilizwa kesi kwa haki, kwa sababu mshtakiwa hawezi kujibu shtaka au kueleza chochote kuhusu shtaka kabla ya kuanza kwa shauri husika.
Inadaiwa masharti hayo hayatoi nafasi kwa mshtakiwa kuomba dhamana, hivyo ni ukiukwaji wa haki ya kusikilizwa ambayo ni moja ya mihimili ya kupata haki katika mahakama ya sheria.
Mjibu maombi aliwasilisha pingamizi likiwa na hoja nne likiambatana na hati ya kiapo kilichodai kuna dosari isiyoweza kutibika kisheria.
Pia alidai ombi hilo linakiuka kifungu cha 3 na 4 cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu na kwamba maombi yaliyomo hayakubaliki kisheria.
Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Machi 18, 2020. Hata hivyo, hayakusikilizwa siku hiyo.
Kumbukumbu za mahakama zinaonyesha Juni 16, 2020 wakili wa Serikali aliomba shauri hilo liwekwe mbele ya jaji mmoja ili kuamua pingamizi za awali.
Jaji alikubali pingamizi la awali na kutupilia mbali ombi hilo ambalo mleta maombi alikata rufaa.
Katika rufaa hiyo, AG aliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Narindwa Sekimanga na Wakili wa Serikali, Leyani Mbise.
Jaji Mlacha akisoma uamuzi amesema kulikuwa na kosa la utaratibu, akieleza ilipangiwa jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu kabla ya masuala ya awali ya sheria kuamuliwa na jaji mmoja wa Mahakama Kuu.
Amesema mahakama hiyo ilitakiwa kuona kuwa kulikuwa na makosa ya utaratibu, hivyo maamuzi yaliyotolewa yalikuwa batili kwani kanuni hazimruhusu jaji kumpa mwenzake kesi.
Jaji Mlacha amesema walipata muda wa kuchunguza kumbukumbu na kuzingatia mawasilisho yaliyotolewa kwa msingi huo na wanadhani ni vema kuanza na sheria.
Amesema wakili Mpoki alikuwa sahihi alipowasilisha kwamba kesi lazima ikabidhiwe kwa jaji mmoja kabla ya kukabidhiwa kwa jopo.
Amesema wanakubaliana na wakili huyo kwamba kwa busara, shauri likishawasilishwa ni lazima lipelekwe kwa jaji mmoja ili kuthibitisha iwapo lina uwezo na linapaswa kuwapo mbele ya Mahakama Kuu.
“Hilo likikamilika, ombi hilo litarudishwa kwa Jaji Kiongozi au Jaji Mfawidhi kwa ajili ya kukabidhiwa kwa jopo. Sheria haitoi nafasi ya kukasimu madaraka kwa jopo la majaji watatu au jaji yeyote bali ifanywe na Jaji Kiongozi au Jaji Mfawidhi,” amesema.
Amesema mahakama haiwezi kwa uhalali kufumbia macho uharamu unaoonekana wazi katika kesi fulani kwa sababu ina wajibu wa kuhakikisha matumizi sahihi ya sheria hizo na mahakama za chini.
Jaji Mlacha amesema ugawaji upya wa kesi lazima ufanywe kwa mujibu wa sheria na kilichofanywa na jopo la majaji watatu, kumpangia kesi mmoja wao, kusikiliza na kuamua pingamizi la awali kilikuwa kinyume cha sheria, na batili kwa kukosa mamlaka.
“Hilo likifanyika, hatuoni sababu ya kujadili msingi wa kwanza, kulingana na matokeo na uamuzi wetu juu ya msingi wa pili, kesi na uamuzi wa Mahakama Kuu uliofanywa katika shauri namba 36/2019 umebatilishwa na kufutwa na uamuzi huo kutenguliwa,” amesema.
“Rufaa hii inaruhusiwa kwa maelekezo kwamba ombi hilo lirejeshwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kumpa jaji mmoja kuamua mapingamizi ya awali yaliyotolewa katika majibu ya ombi na hatua zaidi kwa mujibu wa sheria, hili likiwa ni shauri lenye masilahi ya umma hatutatoa agizo la gharama,” ameongeza kusema.