Rais Samia kubisha hodi Morogoro

Morogoro. Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajia kufanya ziara ya siku sita mkoani hapa na atapata fursa ya kuzungumza na wananchi na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Julai 30, 2024 ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema ziara hiyo itaanza Agosti 2 na ataikamilisha Agosti 6, 2024.

Malima amesema pamoja na kukagua miradi 14 ya maendeleo, Rais Samia atapata fursa ya kuzungumza na wananchi katika maeneo mbalimbali atakayopita.

“Mbali ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, Rais Samia atapata fursa ya kuzungumza na wananchi na atakagua miradi wilayani Gairo, atazungumza na wakazi wa Dumila katika Wilaya ya Kilosa na atazindua kauli mbiu ya Tutunzane Mvomero, inayosaidia kupunguza migogoro kati ya wakulima na wafugaji,” amesema Malima.

Amesema katika ziara hiyo, Rais pia atazindua Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi na kufungua Barabara ya Dumila, Ludewa na Kilosa.

“Kama tunavyojua, treni yetu ya SGR imepata mapokeo makubwa. Watu wengi wameipokea vizuri sana na kwa sasa imehamasisha utalii wa ndani. Hivyo, siku hiyo Rais atasimamia kuifungua rasmi lakini pia atawasalimia wananchi watakao kuwepo katika eneo hilo, na kuzungumza nao kabla ya kuendelea na safari hadi Dodoma,” amesema mkuu huyo wa mkoa.

Hivyo, ametoa wito kwa wananchi wa mkoani Morogoro kujitokeza kwa wingi kumsikiliza maeneo atakayofanya mikutano ya kuwahutubia.

“Lakini sisi wana Morogoro Rais Samia anakuja kutangaza neema na fursa za biashara, uchumi, na uwekezaji zilizopo mkoani kwetu, hii ni fahari kwa hiyo tujitokeze kwa wingi kumpokea,” amesema.

Wakizungumza na Mwananchi Digital kuhusiana na ziara hiyo, baadhi ya wananchi akiwamo Seif Mohamed amesema ujio wa Rais Samia huenda ukasaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwamo ya upatikanaji wa majisafi na salama pamoja na miundombinu ya barabara.

Mohamed ambaye ni mkazi wa Lukobe amesema ujio wake pia ni fursa wananchi kuwasilisha kero kubwa ya barabara inayowakabili katika kata yao.

Mkazi wa Nanenane, Sharifa Baltazari amesema wanakabiliwa na kero kubwa ya ukosefu wa maji.

 “Labda kuja kwa Rais Samia kero hii itamalizwa maana tunapata shida sana,” amesema Baltazari.

 “Ukija Nanenane kuna siku utakuta maji yanatoka, ukija tena utasikia wananchi wanalalamika hawajapata maji hata mwezi mzima. Nina imani Rais akija Morogoro, mambo yatabadilika sana, kero za maji tutazisahau. Tunaomba akifika atafute chanzo cha tatizo na atatue.”

Related Posts