Dar es Salaam. Kutokana na idadi kubwa ya madaktari kuwapo kijiweni, Serikali imesema ipo katika mchakato wa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo, ikigusia kuwa itaanza kudhibiti wale wanaofanya kazi eneo zaidi ya moja.
Zaidi ya madaktari 5,000 waliohitimu na kuwa na sifa za kuajiriwa, bado wanaendelea kusota mtaani kwa kukosa ajira rasmi, huku wakikadiriwa kutumia zaidi ya Sh450 bilioni kusomea fani hiyo.
Hayo yamesemwa leo Jumanne, Julai 30, 2024 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati wa kongamano la kumbukizi ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa linalofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri Ummy amesema madaktari wameruhusiwa kuanzisha hospitali zao baada ya muda wa kazi, lakini kinachoonekana sasa daktari mmoja anafanya kazi zaidi ya vituo viwili hivyo kuminya ajira za madaktari wengine waliopo mtaani.
“Kama kwenye mpira wachezaji wa nje wasizidi kadhaa, inakuja na kwenye sekta ya afya kama una hospitali tutakupa maelekezo, asilimia kadhaa ya unaowaajiri wasiwe kwenye ajira za kudumu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sasa tunafanya uchambuzi tutakuja kwako baada ya kuwa tumemaliza huu uchambuzi,” amesema Waziri Ummy akimfahamisha Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi na kuongeza:
“Mfano wauguzi tunao barabarani, madaktari wa kutosha changamoto ni uwezo wa nchi kuajiri. Tumeanza mazungumzo ya ndani ya wizara, tunaona tunaweza kuzalisha wauguzi 2000 kwa mwaka wakati tuna uwezo wa kuajiri 300 kwa mwaka.
“Na suala la madaktari tunaangalia je tuendelee kuzalisha 1500 wakati tukitangaza ajira hatuchukui zaidi ya 200 hata sekta binafsi hawachukui zaidi ya 200 kwa hiyo ni suala ambalo tunaliangalia,” amesema.
Kufuatia hoja hiyo ya Ummy kuwabana madaktari, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Deus Ndilanha amesema madaktari hawawezi kuzungumzia suala hilo kwa sasa kwa kuwa bado lipo kwenye maandiko ya awali.
“Wadau hatujakaa tukakubaliana, kama ndiyo mawazo ya wizara ni sawa lakini haijaja huku kwa wadau bado. Kulikuwa na hilo wazo, kuna wakati waliwahi kuleta andiko fulani wakisema kliniki inatakiwa kuwa na madaktari walioajiriwa wanne pekee na wengine wawe wasio na ajira mahala pengine. Ni andiko la awali hatuwezi kulizungumzia zaidi sasa, lakini tunafahamu kuna hiyo kitu,” amesema Dk Ndilanha.
Mmoja wa madaktari nchini ambaye aliwahi kuhudumu katika Wizara ya Afya (hakutaka jina lake litajwe) amesema Serikali imekuwa ikinunua vifaa vya bei ghali ilhali hakuna wataalamu wa kutosha wa kuviendesha akitoa mfano wa MRI au CT Scan.
“Ni vema Serikali sasa ikaacha kununua hivi vifaa na badala yake hizi fedha wakaajiri wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kutoa huduma kwa Watanzania. Vifaa hivi ni ghali lakini mwishowe vinabaki kama maonyesho. Unaweza kuwaajiri madaktari 250 kwa mwaka kwa fedha ya MRI moja na wakatoa huduma nzuri kwa wagonjwa,” ameshauri.
Hata hivyo, akizungumza katika kongamano hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imehakikisha fursa za masomo ya elimu ya juu zinapatikana, kwa kuendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa wakiwemo madaktari.
“Lakini pia, wanafunzi wanaosomea kozi za afya wamekuwa wakipewa kipaumbele wakati wote kwa kupewa mikopo ya asilimia 100. Vilevile, suala la kuendeleza rasilimali watu limeendelea kuwa kipaumbele cha Serikali kwa kuongeza bajeti ya sekta ya elimu kila mwaka ili kufanikisha ujenzi wa rasilimali watu yenye ujuzi, stadi muhimu na wanaoweza kumudu mahitaji ya ndani na ushindani wa kimataifa,” amesema.
Akielezea kuhusu ajira na upangaji wa watumishi wa kada za afya, Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita, watumishi 30,000 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi vikiwemo vya vijijini.
“Baadhi ya watumishi hao ni pamoja na madaktari, wauguzi pamoja na wakunga. Hii ni hatua kubwa ya maendeleo katika utoaji wa huduma za afya nchini,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa upatikanaji wa rasilmali watu, vifaa tiba na dawa vinaendelea kuwa vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema suala la uendelezaji wa rasilmali watu kwenye sekta ya afya ni la muhimu, lakini akasisitiza haja ya kupigia debe utalii wa matibabu ili miundombinu inayoboreshwa iweze kuhudumia watu wanaokuja kutoka nje ya nchi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa taasisi Mkapa, Dk Ellen Mkondya-Senkoro amesema mkutano huo umehudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Akielezea mafanikio ya taasisi, amesema kupitia utoaji wa huduma za afya, wameweza kuwafikia wananchi zaidi ya milioni 32 na wametoa ajira zaidi ya 13,000 kwenye sekta ya afya.