Sintofahamu maduka yakifungwa Stendi ya Moshi

Moshi. Wafanyabiashara wa maduka takribani 150 katika Kituo Kikuu cha Mabasi Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wamefunga maduka yao wakiishinikiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kuwapunguzia kodi ya pango.

Wafanyabiashara hao wamegoma leo Jumanne Julai 30, 2024 wakisema, wamelazimika kufunga maduka yao baada ya manispaa kushindwa kutekeleza ahadi waliyoahidi.

Wamesema aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda ambaye kwa sasa ni mkuu wa Mkoa wa Arusha, alipofanya mkutano eneo hilo, wafanyabiashara waliahidiwa kupunguziwa Sh50,000 kwa kila kibanda.

Hata hivyo,  Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, Shaban Mchomvu amefika stendi hapo na kuzungumza na viongozi wa wafanyabiashara hao ambao hawajafungua maduka na wamedai wanamsubiri  mkuu wa wilaya hiyo, Zephania Sumaye ili kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo.

Baadhi ya maduka yaliyopo katika kituo kikuu cha mabasi Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro yakiwa yamefungwa leo Julai 30, 2024 baada ya wafanyabiashara kugoma kufungua. Picha na Omben Daniel

Januari mwaka huu, baadhi ya wafanyabiashara hao walilalamika kutozwa kodi kubwa katika maduka yaliyopo katika stendi hiyo.

Hata hivyo, Makonda aliwataka madiwani wa manispaa hiyo kukaa kikao cha dharura cha baraza la madiwani katika eneo hilo na kuja na majibu.

Baada ya kukaa kikao, meya wa manispaa hiyo, Zuberi Kidumo alitoa taarifa akisema, “tumekaa hapa kama ulivyotuagiza, nikuhakikishie madiwani wako ni wasikivu na wapo kuhakikisha wananchi wa Moshi vilio vyao vinasikilizwa na maisha yao yanakwenda.

“Tulianza kuwasikiliza awali, katika kodi ya Sh1 milioni tukashuka hadi Sh450,000 lakini kwa mujibu wa sheria, bajeti ikishapitishwa na Bunge huwezi kuibadilisha mpaka upate kibali kutoka kwa katibu mkuu, hivyo basi tumekubaliana hapa tutakwenda kuwabadilishia kwenye bajeti inayokuja, tuwashushie tena ili kuendana na hali halisi ya biashara hapa Moshi.”

Meya Zuberi alisema wataanza kupunguza Sh50,000 kwa kila eneo kuanzia sakafu ya chini, ya kwanza na ya pili katika majengo yaliyopo katika stendi hiyo.

Kofuli zikiwa mlangoni katika moja ya duka lililofungwa katika kituo kikuu cha mabasi Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro leo Julai 30, 2024 baada ya wafanyabiashara kugoma. Picha na Omben Daniel

Wakizungumza leo kwa nyakati tofauti, wafanyabiashara hao wamesema manispaa imeshindwa kutekeleza ahadi yao, jambo lililowafanya kufunga maduka kwa kuwa hali ya uchumi ni ngumu na hawawezi kulipa kodi hiyo kubwa.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mjini Moshi, Fredrick Makundi amesema vibanda (maduka) viko 150 na wamevifunga kutokana na kutopunguziwa kodi waliyoahidiwa mwaka huu mpya wa fedha.

“Kilichotufanya tufunge maduka haya ni kwa sababu punguzo la kodi alilifanya mwenezi wa CCM Taifa (wakati huo) aliyefanya mkutano wake hapa, ndiyo tunayolalamikia kwa kuwa alitupunguzia Sh50,000 kwa kila kibanda na wafanyabiashara tupo 150.”

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts