Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji wa Tanzania, Profesa Kitila Mkumbo amesema kama ilivyo azma ya Serikali kuvutia uwekezaji, tayari wamezipokea kampuni kutoka China zilizotua nchini kutaka kuwekeza.
Profesa Mkumbo amesema ameshazungumza na kampuni hizo ili kuzishawishi kuwekeza ikiwamo kwenye viwanda, kilimo, utalii, madini na misitu.
Profesa Mkumbo amebainisha hayo leo Jumanne, Julai 30, 2024 kwenye Kongamano la Wawekezaji na Wafanyabiashara lililoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Ubalozi wa Tanzania nchini China.
Amewataka Watanzania kushirikiana na wawekezaji hao wa kigeni ili wapate mitaji pamoja na teknolojia:”Tumeweka utaratibu mzuri kama Mtanzania unayo ardhi basi utashirikiana na mgeni ambaye anamtaji ili muwekeze.”
Hata hivyo, si mara ya kwanza kwa wawekezaji hao kuja kutafuta fursa, kwa mara ya mwisho wawekezaji 100 waliokuja kutafuta fursa za kuwekeza kumi kati yao walikubali kubaki nchini na kuwekeza.
“Bidhaa nyingi zinatoka China na sisi kama nchi tuna viwango vyetu tulivyoviweka vya bidhaa zinazozalishwa na kuingizwa na kampuni za kichina zinakuwa na ubora,” amesema alipoulizwa kuhusu ubora wa bidhaa za Kichina zitakazozalishwa na wawekezaji hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri amesema ujio wa kampuni hizo za uwekezaji ni fursa nchini.
“Wakishirikiana na Watanzania watazalisha bidhaa zinazohitajika ndani ya nchi ikiwamo za usindikaji wa mazao ya kilimo, na bidhaa za ujenzi,” amesema.
Amesema Watanzania wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kwa kushirikiana na wawekezaji hao na zitapatikana bidhaa za kuuza nje na kuanzisha kampuni, kodi zitalipwa na ajira zitapatikana.
“Pia, kwa miaka ya karibuni kuna ongezeko la ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji mfano mwaka ulipita TIC imesajili miradi 707 ni ongezeko la asilimia 91 kutoka miradi 362 kutoka mwaka wa 2022/23 na kati ya hiyo 707, miradi 58 ina mkono wa Watanzania,” amesema.
Balozi wa Tanzania nchini China, Khamis Omar, amesema ujumbe aliokuja nao wa wawekezaji hao kati yao kuna kampuni kubwa 13 zinazomilikiwa na Serikali Kuu ya China.
“Wanatafuta fursa za kuwekeza barani Afrika na mlango wao wa kwanza ni Tanzania wanataka baada ya hapa kwenda Ethiopia ila tumeshawaeleza hapa kuna fursa nyingi,” amebainisha.
Kuna wawekezaji ambao tayari wameshawekeza akitolea mfano Kongani ya Viwanda ya SinoTan iliyopo Pwani wanayotumia katika kutoa ushuhuda kwa wawekezaji wenzao wanaotaka kuja kuwekeza Tanzania.
Pia, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushirikiano kati ya Tanzania na China, Betty Xu, amesema kazi yao ni kuziruhusu kampuni za kiuwekezaji kuja Tanzania kujionea fursa zilizopo ili kuwekeza.
“Niwashukuru Serikali ya Tanzania kupitia balozi wake na kituo cha TIC na wote wanaofanikisha kuja Tanzania kwa ajili ya kuwekeza ili kuzidi kukuza uchumi,” amesema.
Kongamano hilo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China.