Dar es Salaam. Jopo la mawakili wa Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina limefungua kesi tatu za kikatiba Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ikiwamo ya kupinga uamuzi uliomsimamisha mbunge huyo kuhudhuria vikao 15 vya Bunge.
Kesi hiyo imefunguliwa dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, ambaye kwa sasa ni Dk Tulia Ackson na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, aliye madarakani sasa ni Dk Eliezer Feleshi.
Kwa mujibu wa mawakili hao, adhabu hiyo dhidi ya mteja wao ni kinyume cha sheria na kanuni za Bunge.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30, 2024 mmoja wa mawakili hao wanaodaiwa kuwa 100 watakaomwakilisha Mpina, Edson Kilatu amesema kesi nyingine ni dhidi ya walalamikiwa wanane, akipinga anachodai uagizaji sukari nje ya nchi kinyume cha sheria.
Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Waziri wa Kilimo, ambaye hivi sasa ni Hussein Bashe, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye kwa sasa ni Yusuph Mwenda na waliosalia ni kampuni zilizopewa vibali vya kuagiza sukari ikidaiwa ni kinyume cha sheria.
Kesi nyingine inawahusu wakulima 24 wa miwa katika Bonde la Kilombero, mkoani Morogoro dhidi ya Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wanalalamikia mabadiliko ya Sheria Namba 6 ya Fedha ya Mwaka 2024 ambayo imefanya mabadiliko ya kifungu cha 14 kwa kuongeza kifungu 14(a), akidai kinaiondolea Bodi ya Sukari mamlaka ya kuzuia uingizaji holela wa sukari jambo analodai linahatarisha ustawi wa wakulima.
Wakili Kilatu amesema, “Tumefungua kesi hizo na tumeshalipia tunasubiri tupatiwe namba, tupangiwe jaji na kupewa hati ya wito kuwapelekea walalamikiwa kwenye kesi hizi.”
Akizungumzia kesi kuhusu waziri wa kilimo na wenzake, amesema msingi wake ni Ibara za 26 na 27 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo ibara ya 26 inaelekeza kila raia ana haki ya kuchukua hatua kwa kufuata utaratibu pale anapoona Katiba inavunjwa.
Ibara ya 27 amesema inatoa ruhusa kwa anayeona uchumi unachezewa au kuathiriwa achukue hatua ya kuulinda.
Wakili kiongozi wa jopo hilo, Dk Rugemeleza Nshala amesema zaidi ya mawakili 100 wamejitokeza kusimamia kesi hiyo, akieleza wengine wanaohitaji milango ipo wazi.
“Wananchi wanaruhusiwa kuchangia kesi hizi kusaidia taratibu mbalimbali kukamilika, kesi si ya Mpina peke yake kila Mtanzania anapaswa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia Katiba, suala la sukari si la wananchi wa Kisesa ni la Watanzania wote,” amesema.
Mpina amesema kama mlalamikaji katika kesi hizo mbili atatoa ushirikiano wa kutosha kwa mawakili kuzifanikisha mahakamani.
“Kesi hii ni ya kipekee katika historia ya Tanzania na ni kielelezo cha uwazi, uwajibikaji, utawala wa sheria, na demokrasia,” amesema.
Mpina amesema pamoja na kufukuzwa bungeni hawezi kutetereka na ataendelea kwenda mbele bila kukata tamaa.
Kabla ya azimio la Bunge la kumfungia Mpina, Spika Dk Tulia aliagiza apeleke ushahidi bungeni alipomtuhumu Waziri wa Kilimo, Bashe akidai alilidanganya Bunge kuhusu uagizaji wa sukari kutoka nje.
Baada ya kuwasilisha ushahidi huo, Mpina alizungumza na waandishi wa habari kuuelezea.
Juni 18, 2024 Spika alimpeleka mbele Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki Maadili na Madaraka ya Bunge akidaiwa kudharau kiti cha Spika na mwenendo wa shughuli za Bunge, kwa kupeleka ushahidi nje ambao ulikuwa bado haujafanyiwa kazi na Spika na Bunge.
Kamati iliwasilisha taarifa bungeni Juni 24, 2024 na Bunge kuazimia kumpa adhabu ya kufungiwa kuhudhuria vikao 15 vya bunge.