Vigogo ACT-Wazalendo, Chadema Lindi watimkia CCM

Lindi. Aliyekuwa mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali amejiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi uliofanyika mjini Lindi, leo Jumanne, Julai 30, 2024.

Wanachama wengine wa vyama mbalimbali wamejiunga na chama hicho, akiwamo mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mchinga, Sapanga Hamis Sapanga.

Hadi wakati anajiunga na CCM, Bobali amekuwa mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa wa Lindi.

Kabla ya hapo, Bobali alikuwa mbunge kati ya mwaka 2015 – 2020. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, Bobali alikuwa ACT-Wazalendo na alishindwa na CCM.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Bobali ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (Juvicuf), amesema ameamua kwenda CCM baada ya kuona mambo aliyokuwa akiyapigania, yametekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Leo nahitimisha miaka 20 ya kuwa nje ya CCM. Katika kipindi hicho, wale wenzangu waliniamini kwa nafasi mbalimbali, nilikuwa ofisa utafiti, ofisa uchaguzi na mwenyekiti wa Juvicuf.

“Nilikwenda kugombea ubunge Mchinga, nikashinda, nikawa Waziri Kivuli wa Maji. Mwaka huu ACT Wazalendo walinichagua kuwa mwenyekiti Mkoa wa Lindi na pia nikiwa Msemaji wa Sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,” amesema Bobali.

Amesema kama kuna wanasiasa wa upinzani wagumu, yeye ni mmoja wao lakini ameamua kuhamia CCM baada ya kuona kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia kwenye maeneo mbalimbali.

“Nilipokuwa mbunge nilikuwa napambania kuwa na mfumo maalumu wa korosho ili kuwasaidia wakulima. Leo wakulima wa korosho, tunapewa pembejeo za kilimo bila kutoa hata Sh10,” amesema Bobali.

Amesema Serikali ilikuwa inapoteza mapato mengi kutokana na kukosekana kwa bandari ya uvuvi; na meli zilizokuwa zinavua kwenye bahari kuu, zilikuwa zinageuza na kwenda mataifa mengine na Serikali ilikuwa hainufaiki na rasilimali hizo.

“Rais Samia alipoingia madarakani, ameanza kujenga bandari ya uvuvi yenye thamani ya Sh266 bilioni, tena bandari yenyewe inajengwa Kilwa mkoani Lindi,” amesema Bobali.

Amesisitiza kuwa sasa anakwenda kufanya kazi yake kuzunguka kwenye kila kijiji, kila kata mkoani Lindi kuyaeleza mambo aliyoyaona kwenye uongozi wa Rais Samia.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Mchinga, Sapanga Hamis Sapanga amesema amehama na viongozi wenzake kwenda CCM akiwemo mwenyekiti wa wanawake wa Chadema mkoa wa Lindi, kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya CCM.

“Hapa Lindi mpinzani mwenye fujo nilikuwa mimi, sasa nimehamia CCM, hapa Lindi sasa hakuna upinzani. Ninakwenda kufanya kazi na viongozi wa CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo,” amesema Sapanga.

Akizungumza baada ya wanachama hao wapya wa CCM kukabidhi kadi zao, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Nchimbi amewapongeza kwa uamuzi wao wa kujiunga na chama hicho katika kuwaletea wananchi maendeleo katika Mkoa wa Lindi na Taifa kwa ujumla.

“Niwahakikishe ndugu zangu kwamba tutawapatia ushirikiano wa kutosha katika uendeshaji wa chama chetu,” amesema Dk Nchimbi kwenye mkutano huo.

Related Posts