Moshi. Mgomo wa wafanyabiashara wa kufunga maduka katika Kituo Kikuu cha Mabasi Mjini Moshi, umemalizika baada ya kukubaliana na Serikali kuyafungua na kusubiri hadi mwaka ujao wa fedha, kwa kuwa suala hilo lipo kisheria.
Wafanyabiashara hao wamegoma leo Jumanne Julai 30, 2024 wakisema, wamelazimika kufunga maduka yao baada ya manispaa kushindwa kutekeleza ahadi waliyoahidi.
Wamesema aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda ambaye kwa sasa ni mkuu wa Mkoa wa Arusha, alipofanya mkutano eneo hilo, wafanyabiashara waliahidiwa kupunguziwa Sh50,000 kwa kila kibanda.
Baada ya wafanyabiashara hao kufunga maduka, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye akiwa ameongozana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo na Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Mwajuma Nasombe aliyekuwa na timu ya wataalamu mbalimbali, walikaa kikao kusikiliza changamoto zao.
Katika kikao hicho, wafanyabiashara hao walilalamikia kodi kubwa na kuomba wapewe punguzo kama walivyoahidiwa, jambo ambalo pia halijafanikiwa.
Hata hivyo, Sumaye amesema hilo halitawezekana kwa kuwa lipo kisheria na kuwasihi wasubiri mwaka wa fedha ujao ili Serikali ione kama kuna haja ya kupunguza kodi hiyo.
“Wafanyabiashara mlikuwa na changamoto ya kodi mkiiomba Serikali iwapunguzie kodi hiyo, lakini baada ya kuwapa elimu na kuwafahamisha kuwa bajeti ya mwaka huu wa fedha ilishapita tutaangalia mchakato mwaka wa fedha ujao,wenyewe mmeridhia kufungua maduka.”
“Suala la kupunguza kodi ya pango ni suala la kisheria hivyo ni lazima lipite kwenye vikao mbalimbali vya manispaa na baada ya hapo ndipo tunaweza kusema michakato ya kisheria imezingatiwa.
“Tunapozungumzia mwaka ujao wa fedha maana yake tutakuwa na nafasi ya kuangalia mchakato huu kama kuna sababu ya kupunguza kodi hiyo, kwa kuangalia hali ya soko, maana hali ilivyo hapa stendi yapo maduka ya Sh600,000 hadi Sh1 milioni lakini ukiangalia hapa manispaa wanatoza kodi ya juu kwa wafanyabiashara wanalipa Sh450,000,” amesema Sumaye.
Akizungumzia malalamiko ya wamachinga kufanya biashara eneo hilo la stendi na kuuza bidhaa kama wanazouza madukani, Sumaye amesema hawawezi kufanya biashara katika eneo hilo peke yao kwa kuwa kila stendi ina machinga na Serikali haiwezi kuwaondoa.
” Serikali hatuwezi kuwaondoa wamachinga stendi na kuwaacha wafanyabiashara wa maduka waweze kuuza, soko ni huria wanaweza wakashindana, tunachoangalia ni wamachinga wasivunje sheria wakaenda kukaa mbele ya maduka, tunahitaji sheria zisimamiwe kwa sababu machinga ni kundi la wafanyabiashara tunalolikumbatia, tunaamini ni machinga leo na kesho wanaweza kuwa na maduka,” amesema Sumaye.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Fredrick Makundi amesema wamesitisha mgomo huo na kuridhia kufungua maduka ili kuiacha Serikali kuendelea na michakato ya kushughulikia changamoto zao.
“Tunashukuru uongozi wa Serikali chini ya mkuu wa wilaya, kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza, tutatekeleza maagizo waliyotupa mpaka pale tutakapopata muafaka, wameahidi changamoto zetu kuzishughulikia, hivyo mgomo tumeusitisha na manispaa nayo imesitisha operesheni zake walizokuwa wakifanya,” amesema Sumaye.