Mwanza. Mvutano wa kisheria umeendelea kuibuka katika shauri lililofunguliwa na Wakili Steven Kitale katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya mjibu maombi wa nne, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuwasilisha pingamizi likiwa na hoja mbili.
Wajibu maombi katika shauri hilo namba 17558/2024, lililoitwa mahakamani leo Jumanne Julai 30, 2024 kwa ajili ya kusikilizwa ni Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Baraza la Uongozi la TLS na AG.
Katika shauri hilo, Kitale anahoji uamuzi wa kupandishwa ada za wanachama wa TLS wanaohudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) kutoka Sh118,000 hadi Sh200,000.
Anadai anapoomba mihtasari ya vikao vilivyopitisha ongezeko hilo amekuwa akipigwa danadana jambo lililomkwamisha asitekeleze wajibu wake kwa wanachama.
Pia anaiomba mahakama kutoa amri kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TLS na Baraza la Uongozi la TLS kutoa mihtasari ya vikao vilivyoipitisha Kamati ya Uchaguzi ya TLS na Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi akidai kuna ukiukwaji wa sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi huo.
Shauri hilo lilipoitwa mara ya mwisho Julai 26, 2024 Mahakama iliwataka wajibu maombi kuwasilisha viapo kinzani na majibu ya hoja za mjibu maombi, agizo ambalo wamelitimiza.
Baada ya hapo, AG aliwasilisha pingamizi kabla ya shauri la msingi kuanza kusikilizwa.
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Lameck Merumba ameieleza Mahakama kuwa maombi hayo ni batili kisheria kwa kuwa yamekiuka kanuni na yameambatanishwa na kiapo chenye dosari.
“Mahitaji ya kisheria hayakuzingatiwa kwa sababu kiapo kilichoambatanishwa na maombi hayo hakioani na kiapo cha awali kilichoambatanishwa na shauri la kuomba shauri hilo lifunguliwe,” amedai
“Pia, vifungu vya kuthibitisha yaliyoelezwa katika kiapo cha mleta maombi vimekosewa kutokana na aya zilizopo katika kiapo hicho kutothibitishwa na mambo ya kisheria kuzungumzwa ndani ya kiapo, hivyo tunaiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo,” amedai Merumba anayeshirikiana na Wakili wa Serikali, Felician Daniel katika kesi hiyo.
Jopo la mawakili wa mleta maombi likiongozwa na Godfrey Basasingohe, Godfrey Goyayi, Angelo James na Erick Mutta, limepinga hoja hizo za pingamizi za AG.
Kwa mujibu wa mawakili hao, aya zilizotajwa na wajibu maombi kuwa zinahitaji uthibitisho hazibebi maudhui ya kisheria.
Kuhusu kiapo cha mleta maombi kubeba hoja za kisheria, wakili Mutta ameieleza Mahakama kuwa siyo kweli badala yake zimetoholewa kwenye kiapo cha mleta maombi kilichowasilishwa mahakamani wakati wa ufunguzi wa shauri hilo.
“Zile aya ndogo ambazo mjibu maombi wa nne (AG) anadai zinahitaji uthibitisho zimetumika kuorodhesha vipengele tu, maudhui yanabaki palepale. Hoja ya kiapo kubeba hoja za kisheria siyo kweli kwa sababu mambo yanayosemwa ni hoja zilizochotwa kwenye vielelezo vilivyoambatanishwa kwenye kiapo cha mteja wetu.” ameeleza Mutta.
Baada ya mvutano huo, Jaji Wilbert Chuma aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 9, 2024 atakapotoa uamuzi wa pingamizi hilo.
“Uamuzi wa endapo tutaendelea na usikilizwaji wa shauri la msingi utafahamika baada ya kutoa uamuzi mdogo kuhusu pingamizi lililowasilishwa na mjibu maombi wa nne katika shauri hili,” amesema Jaji Chuma.