Walimu shule ya Jumuiya ya Wazazi CCM Mbeya wagoma

Mbeya. Walimu wa Shule ya Sekondari Ivumwe jijini Mbeya, wamegoma kuendelea na kazi huku wakiziba geti la kuingia shuleni humo kwa magogo wakishinikiza kulipwa fedha za mishahara na malimbikizo ya posho.

Hayo yamejiri leo Jumanne Julai 30, 2024 katika shule hiyo inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Mbeya.

Mmoja ya walimu hao akizungumza kwa niaba ya wengine kwa sharti la kutotajwa jina lake, amesema mgomo huo ni endelevu na utafika ukomo baada ya kulipwa madai yao.

Walimu wa Shule ya Sekondari Ivumwe jijini Mbeya wakiwa na mabango nje ya shule hiyo. Picha na Hawa Mathias

“Tunadai stahiki zetu ikiwamo mishahara na malimbikizo ya posho zetu. Tumevumilia kwa kipindi kirefu tutarejea kazini baada ya kuelezwa hatima yetu,”amesema.

Mwananchi imemtafuta mkuu wa shule hiyo, Oscar Mwaihaba kuzungumzia madai hayo, lakini amesema atafutwe baadaye kwa sasa yupo kwenye kikao.

Kufuatia sakata hilo, Jeshi la Polisi limelazimika kuingilia kati kuondoa magogo yaliyowekwa kwenye geti la shule hiyo sambamba na kufanya mazungumzo na walimu na watumishi ili kurejesha amani.

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts